Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) zinatarajia kuvuna takribani Dola Milioni 2.1 kupitia mauzo ya leseni 45 za uvuvi wa bahari kuu zilizonunuliwa na wawekezaji kutoka nchi za China na Hispania.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya mauzo ya leseni hizo iliyofanyika septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa eneo la bahari kuu kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 220,000 ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazitumiki ipasavyo.

“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa sana kwetu hivyo ni lazima tuwe wabunifu katika utekelezaji wa maelekezo yake ambayo amekuwa akitutaka tuhakikishe rasilimali hii ya maji ya bahari inatumika kikamilifu kuwanufaisha Watanzania wote” Amesema Mhe. Ulega.

Aidha, Mhe. Ulega amebainisha kuwa eneo la bahari linalomilikiwa na Tanzania bara na Zanzibar lina uwezo wa kuhimili mpaka meli 100 hivyo ametoa rai kwa wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza kwenye Uvuvi wa bahari kuu kufanya hivyo ambapo amewahakikishia hali ya usalama na mazingira rafiki ya kufanya shughuli zao wakati wote.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Wizara yake kupitia mamlaka ya usimamizi wa Uvuvi wa bahari kuu (DSFA) itasimamia na kutekeleza vipengele vyote vilivyopo kwenye leseni hizo.

Hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na  Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha eneo la bahari kuu linatumika vizuri ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...