Wawakilishi wa mkutano wa kimataifa kutoka nchi za Afrika zinazotumia lugha ya kiingereza wakiwa katika picha ya pamoja wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Julius Ningu mara baada ya ufunguzi wa mkutano unaojadili udhibiti wa taka hatarishi kwa nchi za Afrika leo jijini Dar es salaam.


Na Aron Msigwa,
Dar es salaam.

Nchi nyingi za bara la Afrika zinakabiliwa na tatizo la udhibiti na uhifadhi wa taka zenye sumu hali inayoathiri maisha ya wanyama na mimea .

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Julius Ningu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa udhibiti wa taka hatarishi na zenye madhara kwa binadamu, mkutano uliowashirikisha wawakilishi kutoka nchi za Afrika zinazotumia lugha ya kiingereza.

Amesema juhudi za uhifadhi wa mazingira barani Afrika na kwingineko duniani hivi sasa zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uzalishaji wa kiwango kikubwa cha taka zenye kemikali na sumu kutoka viwandani na shughuli nyingine za kibinadamu ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri mazingira na maisha ya binadamu.

“Ingawa nchi nyingi barani Afrika hazina maendeleo makubwa kiviwanda , bado zinakabiliwa na tatizo la uzalishaji mkubwa taka hatarishi kutokana na shughuli za viwanda vikubwa na vidogo, karakana, shughuli za usafirishaji , taka za hospitali, maabara za tafiti mbalimbali ,shughuli za ujenzi na shughuli mbalimbali za kijeshi, shughuli za uchimbaji wa madini na kilimo.

Amefafanua kuwa uzoefu na taarifa mbalimbali duniani zinaonesha kuwa taka zenye sumu zimekuwa chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa madhara ya afya kwa binadamu na kusababisha matatizo ya ukuaji kwa watoto, magonjwa ya saratani na matatizo ya uzazi.

Ameongeza kuwa matatizo makubwa ya uhifadhi wa taka zenye sumu kwa nchi nyingi barani Afrika yanachangiwa na hali iliyopo ya kuhifadhi kwa wakati mmoja bila kutenganisha taka zenye sumu na zile zisizo na sumu hali inayotokana na ukosefu wa njia mbadala za uhifadhi, ukosefu wa vifaa na mwamko mdogo kuhusu uhifadhi wa taka hizo kutoka kwa wananchi.

Ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kubadilishana uzoefu wa namna bora ya udhibiti na uhifadhi wa taka zenye sumu ili kupunguza na kukabiliana na madhara yanayoendelea kutokea huku akitoa angalizo kwa nchi za Afrika kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa zinatumia njia salama katika uzalishaji na wakati mwingine kubadilisha taka zinazozalishwa kwa ajili ya matumizi mengine kama uzalishaji wa mbolea jambo ambalo litapunguza uzagaaji wa kiwango kikubwa cha taka.

Akizungumza kuhusu Tanzania Dkt. Ningu amesema serikali inaendelea kutekeleza sheria ya Uhifadhi wa Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni mbalimbali za uhifadhi wa taka ngumu na kukabiliana na tatizo la uzalishaji wa taka zenye madhara kwa afya ya binadamu.

Ameongeza kuwa serikali inandaa mwongozo elekezi utakatumika katika uhifadhi wa mazingira kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kuanzia ngazi za wilaya hadi taifa na kuwatumia wataalamu wa mazingira wa nje na ndani ya nchini kuimarisha usafi katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhifadhi wa Mazingira na Udhibiti wa Taka Hatarishi Barani Afrika Dkt. Taelo Letsela amesema mkutano huo ni fursa pekee kwani unatoa nafasi kwa washiriki kubadilishana uzoefu kutoka katika nchi zao na hatimaye kujengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika na dunia nzima.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Kaka Michuzi, hawa jamaa wanatakiwa wakae ofisini wafanye kazi. Hizi warsha na semina zimekuwa nyingi sana jamani. Hivi hatuoni aibu kweli?

    ReplyDelete
  2. Mwakilishi wa Baraza la Mazingira yupo hapo?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...