Mama Maria Nyerere, Mjane wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa na mwanae Mhe. Makongoro Nyerere na msaidizi wake akifurahia mandhari wakati walipotembelea Daraja la Nyerere Kigamboni jijini Dar es salaam leo April 27, 2016. 
Mama Maria, ambaye hakujali mvua kubwa iliyokuwa inanyesha, alionekana mwenye furaha kufika darajani hapo akisema kuwa  ndoto ya miaka mingi iliyoanzishwa na hayati mumewe imetimia. Pia alimshukuru sana Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kuagiza daraja lipewe jina la Mwalimu na siyo yeye, jambo ambalo amesema limemfariji sana kwani vizazi vya sasa na vijavyo vitamkumbuka mwasisi wa Taifa hili la Tanzania.
Mama Maria Nyerere na msaidizi wake pamoja na Mwanae Mh. Makongoro Nyerere wakitembelea  Daraja hilo leo kwa furaha na fahari.

Mke wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Maria Nyerere ametembelea Daraja la Nyerere linalounganisha eneo la Kigambaoni na Kurasini Jijini Dar es salaam na kuipongeza serikali na wananchi wote wa Tanzania kwa kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo kubwa na la kisasa kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.

Mama Maria Nyerere aliyeongozana na Mwanae Mheshimiwa Makongoro Nyerere amesema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 254.12 kumekamilisha mpango wa miaka mingi ulioanzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa na nia ya kujenga daraja katika eneo hilo la mkondo wa bahari lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti haikuwezekana.
Aidha, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere kwa heshimu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na amebainisha kuwa uamuzi huo utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua juhudi zilizofanywa na mmewe katika ujenzi wa nchi.
"Mimi ninamshukuru sana Rais kwa maana ilikuwa lipewe jina lake, lakini yeye Mungu akamjaalia akasema kwamba hapana tukumbuke tulikotoka, kwa hiyo najisikia vizuri sana, na familia nayo inajisikia vizuri sana, lakini zaidi na watanzania wanajisikia vizuri sana, kwa maana watakuwa wanaulizana Nyerere alikuwa ni nani?" Amesisitiza Mama Maria Nyerere.
Daraja la Nyerere lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 32, njia sita za magari na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5, lilifunguliwa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Aprili, 2016 na linakuwa kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la Dar es salaam.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
27 Aprili, 2016

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. The mdudu, Asante sana MAMA na family yako kwa ujumla tupo pamoja katika harakati za kuijenga Tanzania yetu

    ReplyDelete
  2. Nilitegemea kuona msongamano wa magari,!

    ReplyDelete
  3. Watanzania tuleni mihogo, ili nchi nzima ienee madaraja makubwa na flyovers. MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU MBARIKI RAIS JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI.

    ReplyDelete
  4. Nyerere Bridge: A beautiful piece of work, and we will keep it that way all day, all night.

    ReplyDelete
  5. Nimefurahi kweli daraja hilo kupewa jina la Baba wa Taifa. Namshukuru Rais wetu kufanikisha hilo. Namshukuru Mama wa Taifa letu kupokea zawadi hiyo kwa ukunjufu. Ninafarijika pia kuona mifumo ya kiuchumi na kijamii mbali mbali ya Baba wa Taifa aliyoianzisha na kuilea inazaa matunda ya kujenga Taifa letu, mfano wa NSSF, NHC n.k.

    Hizo ndio sera za CCM. Magufuli hoyee, CCM hoyee!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...