Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Jordan Rugimbana mwishoni mwa wiki amekutana na Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing na kuzungumzia masuala ya kukuza uwekezaji na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.

Mheshimiwa Rugimbana amemwelezea Balozi wa China kuwa ameunda kikosi kazi cha Masuala ya Uwekezaji ambacho kina kazi ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, kutambua wawekezaji waliopo na changamoto zinazowakabili na njia bora za kuzitatua kwa lengo la kuboresha mazingira na kukuza uwekezaji kwenye Mkoa wa Dodoma.

Amesema kwa sasa anataka kuanzisha eneo maalum la uwekezaji kwenye Mkoa wa Dodoma ambapo kitaundwa kituo chenye kutoa huduma zote zinazohitajika kwenye uwekezaji na kutakuwa na taasisi zote zinazohusika na utoaji wa huduma hizo ambapo mwekezaji akifika kituoni hapo hana haja ya kuondoka kwenda kutafuta huduma sehemu nyingine, mahitaji yake yote yatatatuliwa hapohapo kituoni na mara moja ataanza shughuli yake ya uwekezaji.

Pamoja na masuala hayo ya uwekezaji, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alimshirikisha Balozi wa China juu ya mpango wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya wa serikali hapa mkoani Dodoma wenye lengo la kukamilisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu na kuhakikisha serikali inahamia Makao Makuu Dodoma.

Kwa upande wake Balozi Dkt. Lu Youqing alimshukuru Mkuu wa Mkoa Dodoma kwa jinsi ambavyo uongozi wake wa Mkoa ulivyoweka utaratibu wa makusudi wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuanza kushughulikia changamoto zinazowakabili wawekezaji kwa kushirikiana nao na kusema kuwa anapata taarifa nyingi kutoka kwa wawekezaji wa kichina wanaoendesha shughuli mbalimbali Mkoani Dodoma juu ya namna ambavyo uongozi wa Mkoa unashirikiana na wawekezaji hao kutatua changamoto zilizopo.

Vilevile, Balozi wa China alimhakikishia Mheshimiwa Rugimbana kuwa atasaidia kuzikutanisha Mamlaka zinazoshughulikia ujenzi wa mji mpya wa serikali na serikali kuhamia Dodoma na mamlaka ya Manispaa ya Jiji la Beijing China ambayo inauzoefu na imefanikiwa kujenga mji mpya mbali na ule wa zamani kwa kipindi cha miaka miwili tu, lengo likiwa kubadilishana uzoefu katika kutekeleza mradi huo wenye manufaa makubwa kiuchumi hapa Tanzania.
Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana akizungumza na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing mwishoni mwa wiki mjini Dodoma, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya uwekezaji na ushirikiano.
Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing na ujumbe alioambatana nao wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Dodoma (hayupo pichani) wakati walipomtembelea mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake mwishoni mwa wiki kuzungumzia masuala ya uwekezaji na ushirikiano.
Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing akiagana na Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyohusu masuala ya uwekezaji na ushirikiano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...