Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam

SERIKALI ya Denmark imeahidi kuwashawishi wawekezaji wakubwa kutoka nchini humo kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Bandari, Gesi na Mafuta.

Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makao Makuu ya Wizara hiyo.

Bw. Hermann alielezea kufurahishwa kwake na namna Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo ya haraka ya kiuchumi pamoja na kuimarisha uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, na kusema kuwa nchi yake inaunga mkono juhudi hizo.

Alisema kuwa nchi yake itasaidia juhudi hizo kwa kuzishawishi kampuni kubwa zenye mitaji na uwezo wa kiteknolojia kutoka sekta binafsi ili zije ziwekeze hapa nchini na hivyo kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.

Amesisitiza pia umuhimu wa serikali kuwekeza juhudi kubwa katika kuendeleza kilimo kwa kuwa sekta hiyo inaweza kuchochea na kutoa mchango mkubwa na wa haraka wa ustawi na maendeleo ya wananchi.

Aidha, Bw. Hermann, ambaye aliambatana na Balozi wa Denmark hapa nchini, Bw. Einar Jensen, amesifu utendaji mzuri wa Rais Mhe. Dkt. John Magufuli katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi ikiwemo rushwa na kuishauri Serikali kuweka mfumo wa vita hiyo utakaokuwa endelevu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa kwanza kulia), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Ujumbe kutoka Serikali ya Denmark ukiongozwa na Waziri wa Nchi-Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana kwa mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera, Bw. Martin Hermann (kulia) akiwa na ujumbe wake wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam, ambapo nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano utakaojikita katika masuala ya uwekezaji na biashara kwa faida ya pande zote mbili. Kushoto ni Balozi wa Denmark hapa nchini Bw. Einar Jansen.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, wakifuatilia kwa umakini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nchi anayeshughulika na masuala ya Sera wa Denmark, Bw. Martin Hermann (hawapo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera kutoka Denmark, Bw. Martin Hermann (kushoto) akimkabidhi Dkt. Mpango, nyaraka za kampuni zinazoonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika Sekta ya Gesi na Mafuta wakati akiongoza ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (katikati) akiangalia nyaraka alizokabidhiwa na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann, wakati wa mazungumzo kati yao yaliyojikita katika masuala ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kulia kwa Waziri Dkt. Mpango, ni Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatib Kazungu.

HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...