Na Shamimu Nyaki - WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe
ameipongeza timu ya vijana chini ya miaka 17 “Serengeti Boys” kwa hatua nzuri
waliyofikia katika kiwango cha Soka la Afrika kwa kushika nafasi ya pili katika
kundi B walilokuwa wanacheza wakati wa michuano ya AFCON iliyomaliziki hivi
karibuni Mjini Gabon.
Pongezi hizo zimetolewa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuipokea
timu hiyo katika viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Mwalimu Nyerere ambapo
Waziri Mwakyembe aliwataka walimu na wachezaji hao kuendelea kujiandaa
kwa ajili ya mashindano mengine yaliyo mbele yao.
“Nimefurahi kwa hatua mliyoifikia na watanzani wote wanawapongeza kwa kuwa
mmeshindana kwa uwezo wenu na kuirudisha Tanzania katika ramani ya soka
baada ya kukaa nje ya michezo ya AFCON kwa takribani miaka 30 alisema” Mhe
Mwakyembe.
Aidha aliongeza kuwa hapo walipofika wao ni mashujaa na Serikali inaahidi
kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa vipaji hivyo vinaendelezwa kwa ajili ya
ngazi nyingine za kisoka.
Naye Kocha wa Serengeti Boys Kim Paulsen ameiomba Serikali na wadau wa
michezo nchini kuendelea kuisadia timu hiyo katika maandalizi mbalimbali ili
kuipa motisha zaidi katika kufanikisha ndoto ya Tanzania katika mchezo wa soka.
Kwa upande wake kapteni wa timu ya Serengeti Boys Bw. Dickson Job
amewashukuru watanzania kwa mchango mkubwa walioutoa kwao katika
maandalizi mpaka hapo walipofikia ingawa hawakufanikiwa kurudi na ushindi.
“Mchezo una matokeo matatu kushinda, kushindwa au kutoka sare ingawa
hatukutarajia kushindwa kwa kuwa tulitamani sana kurudi na ushindi kama
ambavyo tuliwaahidi watanzania ila mwaka huu bahati haikuwa yetu ila tunaahidi
kuendeleza mapambano katika hatua zijazo” alisema Bw. Job
Timu ya Serengeti Boys imerejea nyumbani baada ya kumalizika kwa michuano ya
AFCON ambapo watapumzika na kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na
michuano inayofuata ya chini ya miaka 20 inayounda timu ya Ngorongoro Heroes.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akimpa
mkono wa kumkaribisha nyumbani mchezaji wa Serengeti Boys Bw. Abdul Sulemani (kushoto) katika
hafla ya kuwapokea wachezaji hao waliorejea nchini kutoka katika michuano ya AFCON nchini Gabon
jana Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati
waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Serengeti Boys pamoja na viongozi wa timu
hiyo katika hafla ya kuwakaribisha baada ya kurejea kutoka katika michuano ya AFCON nchini Gabon
jana Jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 17 “Serengeti Boys” wakimsikiliza Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo katika picha) katika hafla ya
kuwakaribisha baada ya kurejea kutoka katika michuano ya AFCON nchini Gabon jana Jijini Dar es
Salaam.
(Picha na: Lorietha Laurence - WHUSM).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...