NA ESTOM SANGA-TASAF.

Umoja wa nchi zinazozalisha Mafuta kwa wingi OPEC- umeupatia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kiasi cha Dola za kimarekani milioni 12 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kupunguza Umasikini Awamu ya Tatu katika mikoa ya Njombe na Arusha.

Akifungua kikao kazi cha mradi wa kupunguza Umasikini awamu ya tatu (TPRP III ) kwa wasimamizi wa halmashauri za wilaya za mikoa ya Njombe na Arusha kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga, amesema kiasi hicho cha fedha kimetolewa ili kuendeleza miradi ya wananchi kwa jamii zenye upungufu wa huduma za jamii ,uhaba wa kipato na kujiongezea kipato.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkurugenzi wa miradi wa TASAF,Bwana Amadeus Kamagenge, bwana Mwamanga amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa fedha hizo zinazowanufaisha walengwa na kusaidia kufanikisha mkakati wa serikali wa kupambana na umasikini nchini.

Aidha Bwana Mwamanga amesema takribani miradi 407 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji baada ya kupatiwa fedha na kuwaagiza watendaji hao wa halmashauri kuongeza kasi ya kuibua miradi mingine kwenye maeneo yao ili kusaidia jitihada za serikali za kusogeza huduma za kijamii hususani elimu na afya karibu zaidi na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.

Bwana Mwamanga pia ametoa wito maalumu kwa viongozi wa halmashauri za wilaya katika mikoa ya Njombe na Arusha kuendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao hususani ile inayohitaji mchango wa jamii husika ili miradi hiyo iweze kuwa endelevu na yenye manufaa kwa wananchi.

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ambao pamoja na mambo mengine unajenga miundombinu hususani ile inayolenga moja kwa moja kaya za walengwa wa Mpango kwa kuongeza kasi ya kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi. 
 Mkurugenzi wa miradi wa TASAF ,Bw. Amadeus Kamagenge (aliyesimama) akifungua kikao kazi cha Mradi wa kupunguza Umasikini awamu ya Tatu,katika ukumbi wa mikutano wa TASAF jijini Dar es salaam.,Kulia kwake ni Mkurugenzi wa fedha, Bi. Chiku Thabiti,kushoto kwake ni meneja wa miradi ya miundombinu wa TASAF Mhandisi Elisifa Kinasha. 
 Meneja wa miradi ya miundombinu wa TASAF,Mhandisi  Elisifa Kinasha (aliyesimama) akitoa maelezo ya kikao kazi cha Mradi wa kupunguza umasikini awamu ya tatu kwa wasimamizi wa halmashauri za wilaya za mikoa ya Arusha na Njombe yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijini Dar es salaam.

 Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha mradi wa kupunguza  umasikini awamu ya tatu (TPRP) kwa wasimamizi wa halmashauri za wilaya za mikoa ya Arusha na Njombe.Kikao kazi hicho kinafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijini Dar es salaam.

 Washiriki wa kikao kazi cha mradi wa kupunguza  umasikini awamu ya tatu (TPRP) kwa wasimamizi wa halmashauri za wilaya za mikoa ya Arusha na Njombe wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi hicho  kinachofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za makao makuu ya TASAF jijini Dar es salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...