Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Joseph Kakunda (wa pili kulia) akikata utepe kuzindua rasmi Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Kilimanjaro huku Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto), Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Mh. Anna Mghwira (wa pili kushoto) pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Aisha S. Amour (kulia) wakishuhudia tukio hilo katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NSSF mjini Moshi.

MKOA wa Klimanjaro, umepongezwa kwa kuitikia agizo la Rais John Magufuli la kutaka kila mkoa ubainishe fursa za uwekezaji zilizopo na kuandaa mwongozo wa uwekezaji.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Joseph Kakunda katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Kilimanjaro uliondaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Akimwakilisha Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Selemani Jafo, Naibu Waziri huyo alisema kwamba agizo la Rais ambalo limelenga kuweka mikakati mahsusi ya kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Akitoa salamu za pongezi kwa Mkuu wa mkoa, Mh. Anna Mghwira Naibu Waziri Kakunda alisema wakati mkoa wa Kilimanjaro unatekeleza maagizo, serikali kuu nayo inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuvutia wawekezaji mbalimbali. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mh. Joseph Kakunda akitoa hotuba wakati wa kuzindua Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa wa Kilimanjaro kwa niaba ya Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo, Mh. Selemani Jafo (hayupo pichani) kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jengo la NSSF mjini Moshi, mkoani humo.

Akizungumzia Mwongozo huo Naibu Waziri alisema kwamba kazi ya kubaini fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali yenye faida siyo tu kwa wawekezaji pekee bali pia kwa taifa letu kupitia kodi na upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa kila eneo la nchi.

Alisema kazi iliyofanywa na mkoa huo ina maana kubwa kwa kuwa sasa inakuwa rahisi kwa wawekezaji wawe wa ndani au nje kujua namna ya kuwekeza katika mkoa wa Kilimnjaro kwa kuzingatia mahitaji yao na namna rasilimali watu na miundombinu ilivyo.

Alisema agizo la Rais la utengenezaji wa mwongozo unakwenda sanjari na ubainishaji na uandazi wa maeneo ya uwekezaji ili yanapotakiwa yapatikane hima. Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Mh. Anna Mghwira akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mh. Joseph Kakunda (katikati) kutoa hotuba ya uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji wa mkoa huo uliondaliwa na ESRF kwa ufadhili wa UNDP katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF mjini Moshi. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Aisha S. Amour. 

Aliutaka mkoa huo kuutangaza mwongozo wao kwani biashara ni matangazo katika maeneo mbalimbali ya kimataifa na ya wawekezaji katika masoko ya hisa kwa njia ya kielektroniki ili wavune utayari wao wa kukaribisha uwekezaji.

Kakunda alisema kwamba mkoa huo kwa asili unaweza kabisa kuvutia wawekezaji. Kinachostahili kufanywa kwa sasa ni kuhakikisha kauli mbiu ya Kilimanjaro ya Viwanda, inawezekana chukua hatua inatekelezwa kwa vitendo.

Akizungumza kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Mh. Anna Mghwira alisema kwamba Mwongozo huo utafanyiwa kazi na matunda yake yataonekana wakati taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Alisema mkoa huo una rasilimali za kutosha kuwezesha wawekezaji mbalimbali kutekeleza adhma ya kuwa na viwanda vidogo na vya kati vinavyotumia rasilimali kutoka mkoani.

Aliwashukuru wataalam wa ESRF waliwezesha kupatikana kwa muongozo huo na wafadhili ambao ni UNDP.

Naye Dk Tausi Mbaga Kida, Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) ambayo ndiyo ilipewa jukumu na Mkoa wa Kilimanjaro kufanya utafiti na uchambuzi wa kina ili kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa, aliupongeza mkoa wa Kilimanjaro kwa kuona umuhimu wa kuwa na mwongozo wa uwekezaji.

Aidha katika hotuba yake hiyo alisema kuwa taasisi yake ilitengeneza sehemu tatu za taarifa ambazo zote zililenga kutoa uwanda mpana kwa wawekezaji kuwa na taarifa muhimu za uwekezaji katika mkoa wa Kilimanjaro.
 Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Tausi Mbaga Kida akitoa taarifa kuhusu uandaaji wa Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa wa Kilimanjaro ulioandaliwa na taasisi yake kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) katika hafla iliyofanyika mjini Moshi kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF. 


Alisema katika hotuba yake kwamba ESRF ilifanikiwa kuandaa ripoti tatu ambazo ni Ripoti ya Fursafiche katika Viwanda (Industrialization Potentials Report), Ripoti ya Fursa za Uwekezaji (Investment Opportunities Report) pamoja na Mwongozo wa Uwekezaji ambao Mkoa umezindua rasmi leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...