KESI za wanaume kutelekeza familia zao zimejitokeza kwa wingi Kata ya
Saranga eneo la Kimara Temboni jijini Dar es Salaam kwenye kituo maalumu
cha muda kilichoendeshwa kutoa huduma za pamoja kwa waathirika wa
vitendo vya ukatili wa kijinsia ‘One Stop Center’.
Akizungumza
katika kituo hicho kilichoratibiwa na Kituo cha Usuluhishi – CRC,
kilichopo chini ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA),
Mwanasheria wa Kituo cha CRC, Bi. Suzan Charles alisema idadi kubwa ya
wateja waliowahudumia kwa siku mbili ni akinamama waliotelekezwa na
waume zao au wanaume waliowazalisha.
Zoezi
hilo la utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa waathiriwa wa
matukio ya ukatili wa kijinsia 'One Stop Center’ lililoendeshwa kuanzia
Desemba 11 na 12 eneo la Kimara Temboni jijini Dar es Salaam tangu
majira ya asubuhi hadi jioni lilishirikisha huduma za msaada wa
kisheria, Ushauri nasihi pamoja na Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi.
Akifafanua
zaidi Mwanasheria wa CRC, Bi. Suzan Charles alisema licha ya uwepo
tatizo la utelekezaji watoto, lakini walikuwepo pia akinamama wajawazito
ambao nao walitelekezwa wakiwa na hali hiyo jambo ambalo lilikuwa na
changamoto kubwa kwao, kwani hali zao ni dhaifu hawawezi hata kufanya
kazi kujipatia kipato kwa sasa.
Kwa
upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Kituo cha Kituo cha CRC, Bi.
Violeth Chonya mbali na kutoa ushauri wa wateja waliojitokeza
walishirikiana na vitengo husika vya serikali katika kuwaita
wanaolalamikiwa kutelekeza familia na kuangalia namna ya kutatua kesi
hizo.
Alisema
wateja waliokuja kupata huduma katika kituo hicho pia wamekuwa wakitoa
elimu ya uzazi kwa kushirikiana na idara ya afya ili wana jamii
kujitambua na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali.
"..Unajua
masuala mengine kwa wateja waliotutembelea kwa siku hizi mbili
tumebaini akinamama wengi hawana elimu ya kutosha juu ya masuala ya
uzazi, unakuta mama hapewi huduma zozote za msingi toka kwa mwenza wake
lakini bado anaendelea kuzaa huku analalamika kutosaidiwa matunzo...hapa
utabaini kabisa mama hataki kuongeza idadi ya watoto ila ameshindwa
kuzuia mimba anaendelea kuzaa," alisema Bi. Violeth Chonya.
"Naamini
mtu kama huyu akipatiwa elimu ya masuala ya uzazi anaweza kuamua kupata
mtoto pale tu anapoitaji na kuacha kulundika idadi ya watoto huku
akiendelea kukumbana na changamoto ya huduma toka ama kwa mume au wenza
wake..," alisema Afisa Ustawi wa Jamii huyo wa Kituo cha KCRC.
Alisema
kumekuwa na muamko mkubwa kwa jamii ya Kata ya Saranga, Temboni kuja
kupata huduma zilizokuwa zikitolewa kituoni hapo jambo ambalo linaonesha
upo uhitaji mkubwa ya kutengenezwa kwa vituo hivyo, ili vihudumie jamii
kwa karibu.
Huduma zikitolewa kwenye Kata ya Saranga eneo la Kimara Temboni jijini Dar es Salaam kwenye kituo maalumu cha muda kilichoendeshwa kutoa huduma za pamoja kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ‘One Stop Center’.
Huduma zikitolewa kwenye Kata ya Saranga eneo la Kimara Temboni jijini Dar es Salaam kwenye kituo maalumu cha muda kilichoendeshwa kutoa huduma za pamoja kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ‘One Stop Center’
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...