Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ameendesha oparesheni ya usafi na Mazingira kukagua usafi na miti iliyotelekezwa na kuwawajibisha wananchi ambao miti yao imekufa kwa kulipa faini ya shilingi 50,000/= kwa kila mti na kuwataka wapande miti mingine. 

Mkuu huyo wa wilaya amefanya oparesheni hiyo Februari 24,2018 katika mitaa mbalimbali mjini Shinyanga ambapo kila mwananchi ambaye miti iliyopandwa kwenye eneo lake imekufa aliwajibishwa kwa kufanya uzembe na kusababisha miti ife. 

Katika opareshini hiyo kila mwananchi aliyepigwa faini alikuwa anapatiwa risiti ya malipo na aliyeshindwa kulipa alikuwa anapandishwa kwenye gari la polisi kwa hatua zaidi za kisheria. Akizungumza wakati wa oparesheni hiyo Matiro ambaye alikuwa ameambatana na maafisa mbalimbali na askari polisi alisema hataki kuona miti iliyopandwa kupitia kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa Septemba 23,2017 yenye kauli mbiu ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ inakufa kwa uzembe kwani walikubaliana kila mwananchi atunze miti hiyo. 

“Miezi mitano iliyopita tulianzisha kampeni ya upandaji miti wilayani hapa ili kuboresha mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha jangwa,tukapanda miti na kumtaka kila mwananchi atunze iliyopo kwenye eneo lake”,alieleza Matiro. “Nimeanza kukagua miti hii ili nione imefikia hatua gani,kama mti uliopo kwenye eneo lako lazima tukuwajibishe,wote tuliokuta miti imekauka tumewapiga faini ya shilingi 50,000/=”,aliongeza. 

Matiro alisema wilaya hiyo imepiga marufuku kwa mifugo kuzurura mitaani,ikikamatwa kwa kila mfugo faini ni kati ya shilingi 50,000/= na 100,000/=,iwe ng’ombe,mbuzi,kondoo au punda, tukikuta mti umekauka faini ni shilingi 50,000/=. Afisa Misitu wa Manispaa ya Shinyanga,Emmanuel Nyamwihura alisema wanatoza faini hizo kwa mujibu wa sheria ya Usafi na Mazingira ya Mwaka 2014. 
Mmoja wa wananchi katika kata ya Ibinzamata akijitetea kwa kuonesha dumu la maji alilokuwa analitumia kumwagilia maji mti wake uliokufa.Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro. Kushoto ni Afisa Misitu wa Manispaa ya Shinyanga,Emmanuel Nyamwihura - Picha zote na Kadama Malunde1 blog 
Wananchi ambao miti iliyopandwa mbele ya makazi au biashara zao imekufa wakipanda kwenye gari la polisi. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimpongeza mwananchi ambaye miti yake imekua vizuri. 
Mwananchi akionesha mti wake uliokufa kabla ya kulipa faini ya shilingi 50,000/=. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...