*Alionesha ujasiri wa hali ya juu kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya nchini inakoma

*Alifariki Dunia Juni 26 ambayo ndio Siku ya Maadhimisho ya Dawa za Kulevya Duniani

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii 


JUNI 26 ya kila mwaka hufanyika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani.

Kwa mwaka huu nchini Tanzania maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa katika Viwanja vya Tangamano jijini Tanga na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.

Kwa kutumia maadhimisho hayo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya itatumia maadhimisho hayo kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya.

Pia ndio kipindi ambacho Mamlaka inatumia nafasi hiyo kuelezea hatua inazochukua katika kukomesha biashara hiyo ya dawa za kulevya.

Tunafahamu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa sehemu kubwa imefanikiwa kudhibiti biashara hiyo.Kuna sababu nyingi lakini kubwa ni utayari wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kwa kuamua biadhara ya dawa za kulevya sasa basi.

Hata hivyo wakati tunaadhimisho Siku ya Dawa za Kulevya Duniani, hakika tunakumbuka mchango mkubwa wa aliyekuwa Mbunge Amina Chifupa Mpakanjia ambaye enzi za uhai wake alisimama kidete kuhakikisha anapiga vita biashara ya dawa hizo nchini kwetu.

Amina Chifupa kwasababu alijitoa mhanga licha ya kuwa na umri mdogo na katika Bunge la mwaka 2005 lakini alionesha namna anavyochukizwa na biashara ya dawa za kulevya.Hata hivyo wakati Jumanne ya Juni 26 mwaka huu wakati tuaadhimisha Siku ya Dawa za Kulevya, pia tunaadhimisha miaka 13 tangu kufarki kwa Amina Chifupa. Alifariki Dunia Juni 26 mwaka 2007.

Kwa lugha nyingine Amina Chifupa alifariki Dunia ikiwa ndio siku ya Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya. Binafsi naamini kuna siri kubwa hapa ambayo Mwenyezi Mungu ameificha kuhusu Amina Chifupa.Kama ambavyo nimeeleza enzi za uhai wake alisimama imara kukemea dawa za kulevya lakini kifo chkake kikawa ndio tarehe ya Siku ya Dawa za Kulevya.

Hivyo wakati Juni 26 tunaadhimisha Siku ya Dawa za Kulevya Duniani , tunayo nafasi ya kukumbuka mchango wa Amina Chifupa.Tunafahamu ni miaka 13 sasa mapambano ya dawa za kulevya yanaendelea bila uwepo wake.

Hata hivyo naomba nimwambie Amina Chifupa huko aliko kwamba sauti ambayo aliipaza miaka 13 iliyopita kuhusu biashara ya dawa za kulevya na madhara yake imepata Mamlaka sahihi ya kuisemea na hakika kwa sasa hali ni nzuri kwa kiwango kikubwa.Lala Amina Chifupa kwani Watanzania wanaendelea pale ulipoishia.Tunakuezi kwa vitendo.

Kwa kukumbusha tu Juni 26 ya mwaka 2007, ilikuwa hivi ...."Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na mumewe Mohamed Mpakanjia zinasema Mheshimiwa Amina Chifupa- Mpakanjia aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam amefariki dunia majira ya saa tatu kasorobo - Juni 26, 2007...."

Ndio ilikuwa habari kuu iliyotawala katika vyombo vyote vya habari nchini na kuitikisa Tanzania na kusababisha Watanzania wengi kutoamini amini macho na masikio yao wakati TV, Magazeti, Redio na mitandao vilipokuwa vikitangaza habari hiyo ya kusikitisha na kustua ya kufariki dunia kwa Amina Chifupa.

Amina Chifupa, aliyekuwa mtangazaji maarufu na mahiri sana wa kituo redio cha Clouds 88.5FM, hasa kwa vipindi vyake vya "Chei Chei Shangazi" na "Afrika Bambaataa", aliingia bungeni baada ya kushinda nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kupitia tiketi ya Umoja wa Vijana wa CCM. 

Katika kipindi chake cha kifupi cha takribani miaka miwili Bungeni, alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na hoja zake nzito sio tu za kutetea maslahi ya vijana na kukemea rushwa, bali pia kwa kuamua 'kumshika nyati mapembe' kwa kupambana na janga la dawa za kulevya kwa nguvu zake zote. 

Tunaweza sema kwa kujiamini hadi sasa hajatokea tena mbunge aliye shupavu kama Amina Chifupa katika kukemea na kusema kwa sauti kuhusu janga hilo la Dawa zyeye wa aliyekemea na kusema kwa sauti janga hilo kwa Taifa.

Kwa bahati mbaya Amina Chifupa aliaga dunia Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kupambana na Madawa ya Kulevya Duniani, Juni 26. Hivyo ndio tunavyoweza kueleza wakati Tanzania inaadhimisha siku hiyo , inaadhimishwa bila uwepo wake.

Nachoweza kueleza ni hivi wakati tunaadhimisha Siku ya Dawa za Kulevya Dunani , tufahamu inakwenda sambamba na kabisa na Siku aliyofariki Dunia Amia Chifupa aliaga Dunia.Ni vema tukakumbuka machache kutoka kwake kuhusu harakati zake za kupambana na dawa za kulevya nchini.

Daima atakumbukwa kwa kujitolea kupambana na matajiri waliokuwa wanaofadhili au kujihusisha na uingizaji wa dawa za kulevya nchini.Alikuwa ni mbunge mdogo zaidi katika historia ya chombo hicho cha kutunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi yetu kwa kipidi hicho.

Pia atakumbukwa kwa namna alivyosimama kidete na kutamka bayana angewataja hadharani vigogo wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na alienda mbali zaidi kwa kutamka hata kama angekuwa mume wake anahusika naye angemtaja. Hakika Amina Chifupa alikuwa jasiri kiasi hata alifikia uamuzi wa kuwasilisha majina ya vigogo waliokuwa wakifanya biashara hiyo ya "Unga" katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam.

Aliamua kujitoa mhanga kutetea kizazi cha vijana kinachoteketea kwa kutumia dawa za kulevya ilihali waoingiza wanazidi kuwa matajiri tishio na baadhi yao wana nguvu ya ushawishi katika nyanja mbalimbali serikalini.

Ukweli Amina alikuwa ni hazina kwa Taifa na mfano kwa vijana wenye umri mdogo kama wake kwamba inawezekana kujitoa pasipo woga kulitetea taifa na kuwaweka wazi wote wanaotumia utajiri wao, vyeo vyao kufanya au kuwezesha uhalifu hususani katika suala zima la dawa za kulevya. 

Hata hivyo cha kusikitisha ndoto yake hiyo na nyinginezo zilikatizwa ghafla na mauti yaliyomkuta saa tatu za usiku wa Juni 26, mwaka 2007 ambayo ilikuwa ni siku ya Jumanne katika hospitali kuu ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es salaam.

Wakati tunaadhimisha Siku ya Dawa za Kulevya, naomba kutumia nafasi hii kukusha historia ya Amina Chifupa kwa kueleza kuwa 

alizaliwa Mei 20, mwaka 1981 jijini Dar es Salaam, na alisoma Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni, Dar (1988-1994) kabla ya kujiunga na masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Wasichana ya Kisutu, Dar (1995-1998). 

Elimu yake ya Sekondari aliipata katika Shule ya Makongo (1999-2001) kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal (2001-2003) ambako alifuzu Diploma ya Uandishi wa Habari.

Ilipofika mwaka 1999 alianza kazi ya utangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM cha jijini Dar na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mama Shughuli. 

Katika medani ya siasa alikuwa kada wa CCM, Kamanda wa CCM wa Umoja wa Vijana katika tawi la Mikocheni A jijini Dar, Katibu wa Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Dar, Mama Mlezi wa UVCCM na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) matawi ya Bunju na Mbagala.

Mwaka 2005 aliteuliwa kuwa mbunge akiwakilisha kundi la vijana kupitia CCM ambako alidumu na cheo hicho kwa muda mfupi hadi mauti yalipomkuta Juni 26, 2007.

Amina Chifupa alizikwa Juni 28, 2007 kijijini Lupembe katika Wilaya ya Njombe mkoa wa Iringa (sasa ni mkoa a Njombe) karibu kabisa na eneo alilokuwa akiishi bibi yake. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi maarufu wakiiongozwa na aliyekuwa Spika wa Bunge wa wakati huo Samwel Sita, ambaye pia ni marehemu.

Miaka mitatu baadaye, aliyekuwa mume wa marehemu Amina Chifupa, Mohamed 'Medi' Mpakanjia, naye alifariki dunia. Wawili hao walijaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume anayeitwa Abdulrahman anayejulikana zaidi kama Rahman.

Baba mzazi wa marehemu Amina Chifupa, Mzee Hamisi Chifupa aalifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 27, 2017 nyumbani kwa mwanaye wa kike, Upanga, jijini Dar es Salaam.

Mola aiweka mahali pema peponi roho ya marehemu Amina Chifupa wa Mpakanjia. WOTE NA TUSEME.... AMINA!

Pia Michuzi Blog na Michuzi TV inaungana na Watanzania wengine kuendelea kukuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho marehemu Amina Chifupa Mahala Pema ,Peponi .AMINA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...