"JAMII"
Showing posts with label JAMII. Show all posts




Dar es Salaam, 12 Septemba, 2025

KWA mujibu wa Kifungu cha 13(a) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ina wajibu wa kutoa ithibati na vitambulisho rasmi kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo vya taaluma, sambamba na kusimamia uzingatiaji wa maadili ya uandishi wa habari nchini.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Bodi imepokea na kufuatilia taarifa zinazozagaa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, zinazodai kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuwa waandishi wa habari kwa tuhuma za kuendesha televisheni za mtandaoni (Online TV) zisizosajiliwa kisheria.

Bodi inapenda kutoa ufafanuzi rasmi kwamba watu waliotajwa kwa majina ya Ezekiel Mollel (Manara TV) na Baraka Lucas (Jambo TV) SIO waandishi wa habari kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 19(1) cha Sheria hiyo, imeelezwa wazi kuwa:

“Mtu hataruhusiwa kufanya kazi za uandishi wa habari isipokuwa awe amethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.”

Taarifa za Bodi zinaonyesha kuwa watu hao hawajawahi kujisajili katika mfumo rasmi wa usajili wa waandishi wa habari ujulikanao kama TAI HABARI, kwa ajili ya kuomba ithibati na kupata Vitambulisho vya Uandishi wa Habari (Press Cards) vinavyotolewa kisheria.
Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria, hawana hadhi ya kisheria ya kutambulika kama waandishi wa habari.

Waandishi wa habari waliokidhi vigezo na kupatiwa ithibati na vitambulisho halali wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa uhuru, heshima na kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya habari. Wale ambao bado hawajakidhi vigezo wanahimizwa kujiendeleza kielimu ili waweze kushiriki ipasavyo katika taaluma hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Bodi inatoa wito kwa vyombo vya habari, wanahabari, na wadau wote wa sekta ya habari kuendelea kushirikiana na Bodi ya Ithibati katika kuhakikisha kuwa sekta ya habari nchini inasimamiwa kitaaluma, kwa kuzingatia:

Maadili ya taaluma ya uandishi wa habari,
Maslahi mapana ya Taifa,

Na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi.




Na Mwamvua Mwinyi, Pwani, Septemba 12, 2025
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imerejesha kiasi cha shilingi 1,376,250 kwa wananchi wa Kitongoji cha Nyakahamba, kata ya Kerege, wilayani Bagamoyo, waliotozwa kinyume cha utaratibu na Mwenyekiti wa Kitongoji kwa ajili ya kulipia huduma ya maji, licha ya kuwa mkandarasi wa mradi tayari alikuwa amelipwa.

Akitoa taarifa kuhusu ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Domina Mukama, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, alisema urejeshwaji huo wa fedha ni sehemu ya mafanikio ya jitihada za taasisi hiyo katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo.

Kwa mujibu wa Mukama, ufuatiliaji huo ulifanyika katika mradi wa upanuzi wa vituo vya kuchotea maji katika Kitongoji cha Nyakahamba, wenye thamani ya shilingi milioni 60.

“Kazi zilizopaswa kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ulazaji wa mabomba, ufungaji wa ‘fittings’, na ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji."

Hata hivyo, wananchi walilalamikia kutozwa fedha kinyume cha utaratibu,” alisema Mukama.

Alibainisha, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa wananchi hawakustahili kulipia huduma ya maji, kwani mkandarasi alikuwa tayari amelipwa gharama zote za kipindi cha majaribio, kabla ya mradi kukabidhiwa kwa RUWASA (Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini), kata ya Mapinga, kwa ajili ya uendeshaji rasmi.

Mukama alisema, fedha hizo zilizorejeshwa zitatumika kusaidia wananchi kulipia huduma ya maji pindi mradi utakapoanza rasmi baada ya kukabidhiwa kwa RUWASA.

Alieleza kuwa, hadi kufikia kipindi hicho TAKUKURU imefuatilia jumla ya sh. bilioni 32.7 zilizotumika katika miradi 40 ya maendeleo kutoka sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, na barabara.

Katika hatua nyingine, Mukama alieleza TAKUKURU Pwani ilipokea jumla ya taarifa 29 za malalamiko kati ya taarifa hizo 16 hazikuhusu vitendo vya rushwa, huku taarifa 13 zikiwa zinahusiana moja kwa moja na vitendo vya rushwa na zinaendelea kushughulikiwa katika hatua za uchunguzi.

Katika upande wa mashtaka alisema kesi mpya 14 zilifunguliwa mahakamani, na kesi 24 zinaendelea kusikilizwa,kati ya kesi 17 zilizotolewa uamuzi, kesi 15 ziliamuliwa kwa upande wa Jamhuri kushinda, huku kesi 2 Jamhuri ikishindwa.
Meza kuu wakati wa semina ya utoaji elimu ya sheria ya bima kwa mahakimu wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam. Semina hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, 2025.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Awamu Mbagwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya utoaji elimu ya sheria ya bima kwa mahakimu wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam. Semina hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, 2025.
Kamishna wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya utoaji elimu ya sheria ya bima kwa mahakimu wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam. Semina hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, 2025.

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
KAIMU Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Awamu Mbagwa, ametoa wito kwa watumishi wa Mahakama kutumia ipasavyo fursa ya elimu ya bima ili kuongeza uelewa utakaosaidia katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Septemba 12, 2025 wakati wa semina ya utoaji elimu ya sheria ya bima kwa mahakimu wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jaji Mbagwa amesema elimu ya bima ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za mashauri yanayohusiana na bima, hususan migogoro ya fidia baada ya ajali, majanga au hasara za kibiashara.

“Napenda kutoa wito kwa watumishi wote wa Mahakama kutumia fursa hii kujifunza kwa makini, kuuliza maswali na kushiriki kikamilifu katika mijadala. Elimu hii itatufaa sisi binafsi, familia zetu na taasisi tunazozihudumia,” alisema Jaji Mbagwa.

Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Mahakama katika kuwapatia mafunzo hayo, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza weledi wa Majaji na Mahakimu katika kushughulikia mashauri ya bima kwa haki na kwa mujibu wa sheria.

Jaji Mbagwa alihitimisha hotuba yake kwa kupongeza wadau mbalimbali wa Mahakama walioshiriki katika semina hiyo na kusisitiza kuwa elimu ya bima ni msingi wa uaminifu, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kamishna wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware amesema kuwa mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na Mahakama ili kuhakikisha migogoro ya bima inatatuliwa kwa haki na haraka, jambo litakaloimarisha imani ya wananchi kwa sekta hiyo.

“TIRA imejipanga kutoa elimu endelevu kwa wadau wake wote ili kuhakikisha sekta ya bima inakua kwa uwazi na kwa manufaa ya wananchi. Ushirikiano na Mahakama ni wa muhimu kwa sababu migogoro mingi ya bima huishia mahakamani, hivyo uelewa wa pamoja utasaidia kulinda haki za wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa ukuaji wa sekta ya bima nchini unahitaji usimamizi madhubuti na uelewa mpana wa sheria, jambo linalofanikishwa kupitia mafunzo hayo.

TIRA imeendesha semina ya elimu ya Sheria ya Bima kwa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo ni kuwajengea uelewa mpana kuhusu masuala ya bima na kuongeza ufanisi katika kushughulikia mashauri yanayohusiana na sekta hiyo.

Kupitia semina hiyo, TIRA imelenga kuimarisha ushirikiano na mhimili wa mahakama ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria za bima unafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa manufaa ya wananchi.













Matukio mbalimbali katika semina ya utoaji elimu ya sheria ya bima kwa mahakimu wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Picha za pamoja mara baada ya ufunguzi wa semina ya utoaji elimu ya sheria ya bima kwa mahakimu wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wa Mkoa wa Dar es Salaam.



KAMPUNI ya Sukari Kilombero imefanya Mkutano wa programu ya Managers in Training (MIT) 2025, kusherehekea miaka 23 tangu kuanzishwa kwa Programu hii ambao ni mahususi kwa ajili ya kulea na kutoa mafunzo kwa viongozi na wataalamu mbalimbali kwenye sekta ya sukari pamoja na Sekta nyingine nchini Tanzania.

Kwenye mkutano huo ambao ulihudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa kampuni mbalimbali na viongozi chipukizi, Bi. Diana Mwakitwange, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Kilombero Sugar, alisema kuwa programu hii ni uthibitisho tosha kuwa kampuni hiyo itaendelea kukuza na kulea viongozi wapya ambao wanatarajiwa kuendeleza sekta ya sukari nchini na nyingine kwa miaka mingi ijayo

“Lengo la Programu hii sio tu kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa kampuni mbalimbali lakini pia ni kutengeneza viongozi ambao wataongoza nchi hii kwa miaka na vizazi vijavyo” alisema

Akimwakilisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambaye kwenye mkutano huo aliwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa TVET. Dkt. Mgaya aliipongeza Kilombero Sugar kwa uwekezaji wake wa kimkakati kwenye rasilimali watu:

“Programu hii sio tu kwamba inaonesha mafanikio ya Kilombero Sugar lakini pia ni hazina ya taifa. Kila mhitimu aliyepata mafunzo kutoka kwenye programu hii atakuwa ni mwenye ubunifu zaidi, ufanisi zaidi na ni fahari ya taifa”

Aidha Mgaya alionyesha ni kwa jinsi gani programu hii ya kutoa mafunzo kwa uongozi, inavyoisaidia Tanzania kufanikiwa zaidi kwenye sekta viwanda, soko la ajira na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Bw. Guy Williams, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero, akizungumzia kuhusu programu hiyo alisema:

“Uongozi sio kitu cha kurithi bali ni kitu ambacho kinafundishika. Kwa miaka 23, tumetoa mafunzo mameneja chipukizi zaidi ya 80 na wengi wao kwa sasa wameshika nafasi za juu kwenye kampuni mbalimbali”

Alitoa wito kwa Wizara husika kuongeza kutoa ushirikiano ili kuziba pengo la ujuzi na maarifa kwenye sekta ya sukari kwa kutenga sehemu ya Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi kuimarisha Taasisi ya Sukari ya Taifa (NSI).

Ambroce Heri, mshindi wa kwanza mwanafunzi wa kutoka Idara ya Kilimo cha Mashamba, alisema:

“Program hii umebadilisha mtazamo wangu sio tu kuhusu kilimo, bali pia kuhusu uongozi na jinsi ya kusaidia jamii.”

Mkutano huo pia uliangazia umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya sukari na taasisi za elimu. Hadi sasa, wahitimu 85 wamepitia wameshapata mafunzo w kutoka kwenye programu hiyo huku 27 kati ya hao wanafanya kazi kwenye kampuni ya Kilombero Sugar,

Aidha Wizara iliunga mkono juhudi za Kilombero Sugar za kuunganisha elimu ya nadharia na matumizi yake kwa vitendo kwenye sekta ya sukari nchini.

Mwishoni mwa mkutano, wadau waliahidi kuendeleza mpango programu hiyo, kuongeza ushirikiano na taasisi za elimu na kuangalia fani nyingine ambazo zinahitaji programu kama hizi.




Picha ya pamoja mara baada ya wafanyakazi wa Serene Beach Resort na Masai Adventure Safari wakifanya usafi katika ufukwe wa Bahari jijini Dar es Salaam leo Septemba 11, 2025.

TAKA za plastiki zimeelezwa kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi na uzuri wa mandhari ya Tanzania, huku wadau wa mazingira wakisisitiza kuwa suluhisho la kudumu lipo mikononi mwa jamii yenyewe.

Kampuni ya utalii ya Masai Adventure Safari kwa kushirikiana na Serene Beach Resort, leo Septemba 11, 2025, wamefanya shughuli ya usafi wa fukwe jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa jamii kushirikiana kulinda mazingira dhidi ya taka za plastiki.

Mkurugenzi wa Masai Adventure Safari, Bi. Erika Tola, alisema Tanzania ni nchi nzuri yenye mandhari ya kipekee, lakini taka za plastiki zinazotapakaa zinatishia uzuri wa asili na afya za wananchi.

“Nilipofika Tanzania niliona taka nyingi za plastiki. Ni jambo la kusikitisha kwa sababu plastiki inapoingia baharini, samaki huimeza, kisha baadaye tunapokula samaki tunakula plastiki pia. Hali hii inaleta hatari ya maradhi makubwa ikiwemo saratani,” alisema.

Ameongeza kuwa plastiki inapochomwa, moshi wake una madhara makubwa kiafya, na hivyo jamii inapaswa kushirikiana kukusanya na kuchakata plastiki ili kulinda mazingira na afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Masai Adventure Safari, Jakobo Kibori, aliwataka wananchi kuwa mabalozi wa mazingira kwa kuhakikisha plastiki inahifadhiwa vizuri na sio kutupwa ovyo.

“Mimi na wewe tuwe balozi wa mazingira. Unaponunua maji au kinywaji chochote kilichomo kwenye chupa ya plastiki, tusitupilie ovyo hata kama ni porini, kwenye fukwe au barabarani. Tuhifadhi plastiki mpaka inapochukuliwa na wahusika kwa ajili ya kuchakatwa. Kufukia plastiki fukweni si suluhisho, bali ni kuongeza tatizo,” alisema Kibori.

Aidha, Afisa Uhusiano wa Serene Beach Resort, Anna Khaday, alitoa wito kwa serikali kuhakikisha elimu ya kudhibiti taka za plastiki inatolewa kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili kuongeza uelewa wa jamii.

“Sisi Serene Beach Resort tumeshaweka mikakati ya kudumu kwa kuweka vifaa vya kuhifadhia taka ngumu, hasa plastiki. Tukipewa elimu ya kutosha, itawezekana kabisa kudhibiti taka hizi ambazo ni hatari kwa afya za binadamu na kuheshimu mazingira yetu,” alisema Khaday.












Matukio mbalimbali ya wafanyakazi wa Serene Beach Resort na Masai Adventure Safari wakifanya usafi katika ufukwe wa Bahari jijini Dar es Salaam leo Septemba 11, 2025.
Mwenyekiti wa Jukwa la Watendaji Tanzania (CEOrt Roundtable) Mr David Tarimo akiongea wakati wa mjadala wa kupokea ripoti ya mapendekezo ya maeneo ambayo Tanzania inaweza kujipatia mapato zaidi katika pato la taifa( DGP)  kupitia mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazotokana na madini hapa nchini katika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji ( CEO) wa Jukwaa la Wakurugenzi nchini ( CEOrt Roundtable ) Bi Santina Benson ( kati kati) akibadilishana mawazo na Balozi wa Uingereza hapa nchini Bi Marianne Young wakati wa mjadala ulioandaliwa na jukwaa hilo kujadili ripoti inayoonesha maeneo ambayo Tanzania inaweza kuingia kipato kikubwa kupitia mnyororo wa thamani wa madini ya kimkakati.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam | 10 Septemba 2025
Tanzania iko katika hatua ya mageuzi ya viwanda ambayo huenda ikafungua fursa ya mapato ya ziada ya hadi dola bilioni 11.7 kwa mwaka pamoja na kuzalisha ajira zaidi ya 25,000, kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa katika mkutano wa ngazi ya juu wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 9 Septemba 2025.

Kupitia kaulimbiu “Kufanikisha Uzalishaji Afrika: Mnyororo wa Thamani wa Madini hadi Uzalishaji,” kikao hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa sekta binafsi, watunga sera waandamizi, wawakilishi wa kidiplomasia, na washirika wa kimkakati katika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili namna Tanzania inavyoweza kupanda juu kwenye mnyororo wa thamani wa madini kwa kuchakata madini ndani ya nchi badala ya kuyauza ghafi.

Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofadhiliwa na Uingereza kupitia mpango wa Manufacturing Africa, uliotekelezwa na kampuni za McKinsey & Company na BDO, kwa ushirikiano na ASNL Advisory. Ripoti hiyo imebaini fursa 14 zenye matokeo makubwa ya uwekezaji katika aina 11 ya madini nikiwemo dhahabu, grafiti, madini adimu, nikeli, shaba, kobalti, chokaa na fosfati.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inaweza kuongeza mapato yake ya kiuchumi na ushindani wa viwanda kwa kubadilisha madini ghafi kuwa bidhaa zenye thamani kama saruji, vigae, glasi, dhahabu iliyosafishwa, vito vya dhahabu, na madini ya betri ambayo ni muhimu katika mabadiliko ya dunia kuelekea uchumi wa kijani.

Akizungumza katika tukio hilo lililodhaminiwa na Kioo Limited, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Bi. Marianne Young, alisema kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na madini mengi yenye thamani ambayo yatawanufaisha wananchi wake, huku akithibitisha kuwa Uingereza itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za kuimarisha viwanda kupitia mnyororo wa thamani wa madini.

“Majadiliano haya yanakuja wakati muhimu sana kwa Tanzania. Kwa utajiri mkubwa wa madini ulionao, nchi hii inaweza kuwa kitovu cha uzalishaji kwa ukanda huu na mshiriki muhimu katika uchumi wa kijani duniani,” alisema Bi. Young.

“Kupitia ushirikiano wa pamoja na mpango wa Uzalishaji Afrika ‘Manufacturing Africa’, Uingereza imejidhatiti kushirikiana na sekta binafsi na serikali ya Tanzania ili kubadilisha fursa hii kuwa ajira endelevu, ukuaji jumuishi, na ustawi wa muda mrefu.”, amesema.

Amelisifu jukwa la Watendaji Wakuu (CEOrt) hapa nchini kwa kuandaa majadiliano yenye tija ambayo yanaonyesha namna rasilimali za madini zinavyoweza kuchochea ndoto ya Tanzania ya kuwa taifa la viwanda, na kusaidia juhudi za serikali.

Mwenyekiti wa CEOrt, David Tarimo, alisisitiza umuhimu wa Tanzania kutoka kwenye utegemezi wa kuuza madini ghafi na kuelekea kwenye uchakataji wa ndani kama njia ya kufanikisha ukuaji wa kiuchumi wa kudumu na jumuishi.

“Sekta ya madini inachangia takribani asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP), huku dhahabu peke yake ikichangia karibu asilimia 80 ya mauzo ya madini nje ya nchi. Tunaona fursa zaidi ya hapa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vya uchakataji vinavyolenga masoko ya nje,” alisema Tarimo.

“Kwa kipindi cha robo karne tangu kuanzishwa kwake, CEOrt imekuwa ikileta pamoja viongozi kupitia sekta binafsi kushiriki katika mchakato wa maboresho ya sera na kipaumbele cha kitaifa. Kikao hiki kinaonyesha kuwa sekta binafsi na serikali wanaweza kuendelea kushirikiana kujenga taifa lenye ushindani zaidi.”

“Ikiwa tutaimarisha uboreshaji wa mnyororo wa thamani wa madini, tutaongeza mapato na pia kujenga kitovu cha uzalishaji kinacholingana na mustakabali wa uchumi wa kijani Afrika. Utajiri wa madini wa Tanzania unaweza kuendesha maendeleo kwa miaka 25 ijayo kulingana na Dira ya Maendeleo ya 2050, ikiwa tutapa kipaumbele kwenye ongezeko la thamani,” aliongeza.

Wajumbe wa jukwaa la CEOrt linalojumuisha zaidi ya kampuni 200 za sekta binafsi walitoa wito kwa kuandaliwa miradi ya uwekezaji wa viwanda vya mnyororo wa thamani wenye tija, huku wakitaka kuendelezwa kwa ushirikiano na serikali ili kuendeleza mchakato huu wa mageuzi ya viwanda.

Mjadala wa wazi uliosimamiwa na Bi. Anna Rabin, Mkurugenzi Mtendaji wa Above Ground Advisory na Balozi wa Heshima wa Australia nchini Tanzania, uliangazia namna sekta binafsi inaweza kunufaika na fursa katika viwanda vinavyohusiana na madini.

Washiriki walionyesha ongezeko la mahitaji ya bidhaa kama saruji, vito vya dhahabu, vigae, na vifaa vya betri katika soko la kikanda na kimataifa, huku wakihimiza sera thabiti na mazingira bora ya uwekezaji yanayounga mkono ongezeko la thamani ya madini.

Leonard Mususa, mjumbe wa CEOrt na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Breweries Limited, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na hatua madhubuti katika kufanikisha ajenda ya kuchakata madini ndani ya nchi.

“Tanzania iko kwenye nafasi nzuri kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda vinavyotokana na madini,” alisema.

“Lakini ili kufanikisha hili, tunahitaji miradi yenye tija, sera thabiti, na maendeleo ya wajasiriamali wa ndani.”

“Kwa kuunganisha mtaji, ushirikiano, na utetezi wa sera, Tanzania inaweza kupata thamani kubwa zaidi kutokana na utajiri wake wa madini,” aliongeza.

Bw. Terence Ngole, Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, alitumia nafasi hiyo kuonyesha kuwa serikali imejipanga kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi ili kusukuma mbele uchakataji wa ndani na utofauti wa uchumi.

“Tumeendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi kuona namna sekta ya madini inaweza kuchangia zaidi katika Pato la Taifa, kupunguza utegemezi wa kuuza ghafi, kuimarisha msingi wa viwanda, na kutoa ajira kwa vijana wengi nchini,” alisema.

“Tunajivunia ushirikiano wetu wa muda mrefu na CEOrt na tunaamini kuwa kwa pamoja tunaweza kutekeleza mapendekezo haya na kugeuza utajiri wa madini wa Tanzania kuwa msingi wa ustawi wa kweli kupitia ongezeko la thamani na uzalishaji wa ndani,” alihitimisha.




Sehemu ya wadau mbalimbali walioshiriki katika mjadala huo.


Kutoka  kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu  Mizengo Kayanza Peter Pinda katikati ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro  na Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.

Na Khadija Kalili Michuzi TV
KATIBU MKUU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dkt.Asha -Rose Mtengeti Migiro amezindua mafunzo ya Uzamili na Uzamivu kwa Viongozi ambayo yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha Mkoani Pwani.

Akizungumza leo tarehe 09 Septemba 2025 ambapo pia alikua mgeni rasmi amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa njia ya kubadilishana wataalamu watakaotoka nchini China na wangine watatoka hapa kwa lengo la kwenda kubadilishana uzoefu.

"Ninafuraha sana leo kwa kuzindua program hii itakayokua endelevu kati ya nchi hizi mbili rafiki yaliyoasisiwana Viongozi wetu wa Jamhuri ya Watu wa China kwa kupitia Chama Chao Cha CPC na Chama Cha Mapinduzi (CCM)" amesema Katibu Mkuu Dkt. Migiro.

"Kwa kupitia program hii tutakwenda kujifunza wenzetu wanafanya nini na kwa wakati huutumeoa tutor fursa hii kwa viongozi wakuu ambao watakuja kurithisha kizazi cha sasa na kijacho" amesisitiza Dkt.Migiro.

Awali Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Chen Minjian akizungumza wakati wa uzinduzi wa Program hiyo ametoa pongezi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Katibu Mkuu mwanamke wa kwanza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dkt. Migiro huku amempa pongezi nyingi Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kwa uongozi wake wenye mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo.

Viongozi wengine waliohudhuria uzinduzi wa Programu hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Mazengo Kayanza Peter Pinda ,Dean of the school of Global Leadership Chong Yang na Dean of Institute for financial studies Renmin University of China Wang Wen .

Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Mzee Philip Mangula, Mukama , Mheshimiwa Balozi wa Afrika Kusini Naluthando Mayende Malope na wengine kutoka balozi zilizopo katika nchi sita marafiki.

Aidha Wang Wen amemsimfia na kumpa pongezi Dkt. Migiro kuwa mwanamke we kwanza kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Chama kikubwa barani Afrika.

Wakati huohuo Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu Mazengo Kayanza Peter Pinda amesema kuwa ni jambo la kujivunia kwa Vyama sita marafiki kuona Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere inaendelea kukuwa siku baada ya siku tangu ilipoanzishwa hadi sasa huku akitoa ahadi kwa wawakilishi wa CPC ambao ndiyo wadhamini wakuu kwamba wataendelea kupewa taarifa zote muhimu za Shule hiyo.

Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Profesa Marcellina Mvula Chijoriga amesema kuwa wanajivunia uzinduzi wa Programu hizo mbili ambapo wanafunzi kumi ni wa Uzamili 'PhD ' huku wengine 22 wa Uzamivu ambapo washiriki wote wametoka katika Vyama Sita Marafiki vya Ukombozi Kusini Mwa Afrika .

"Tunatarajia kupata ujuzi kutoka Chuo Kikuu Cha Renmin ambacho ni kikongwe kwani kimeanzishwa 1937" amesema Profesa Chijoriga.
Wafanyakazi katika kiwanda cha kuchakata viungo Cha Horizon Group wakitayarisha mazao hayo katika mji wa Kaduna. Nigeria. Wakulima wa Viungo nchini Tanzania, Nigeria na Madagascar watanufaika na mipango kabambe wa maboresho ya mazao hayo ili kukidhi viwango vya kimataifa na kukuza mauzo.

WAKULIMA wa mazao ya viungo Tanzania wamepata neema mpya kufuatia uamuzi wa kampuni ya Aavishkaar Capital kuwekeza Dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya ukuzaji na uchakataji wa mazao hayo ili kukidhi mahitaji ya soko.

Fedha hizo zitawasaidia wakulima zaidi ya 3,000 katika nchi za Tanzania, Nigeria na Madagascar kupitia kampuni ya Horizon Group inayofanya kazi na wakulima wa viungo.

Aavishkaar, inayofanya kazi chini ya mwamvuli wa Aavishkaar Group, imetangaza uwekezaji huo barani Africa kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji na Maendeleo inayomilikiwa na Serikali ya Ujerumani, KfW.

Uwekezaji huo umewezeshwa na Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF) ambao ilitoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 5 kwa Horizon Group Africa. Huu ni uwekezaji mkubwa wa nne kufanywa na GSCSF barani Afrika.

Kampuni ya Horizon Group hujihusisha na utafufutaji na uchakataji wa viungo na kuviuza katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU), Asia na Marekani. Kampuni hiyo inafanya kazi kupitia vituo vyake nchini Tanzania, Nigeria na Madagascar, ikinunua na kusaidia katika uzalishaji na uchakataji wa tangawizi, bizari (manjano), iliki, mdalasini, karafuu na pilipili manga.

Mkopo huo utaelekezwa zaidi katika kukuza mtaji wa Horizon Group, hususan katika ununuzi wa malighafi ili kukidhi viwango na mahitaji wa soko la kimataifa.

Kampuni ya Horizon Group ilianzishwa nchini Nigeria mwaka 2006 ikijihusisha na biashara ya mazao mbali mbali ya kilimo, vyakula vya kusindika na Samani. Mwaka 2017, kampuni hiyo iliamua kujikita katika kutafuta, kuchakata na kusafirisha viungo kutoka katika nchi za Tanzania, Nigeria na Madagascar zinazoongoza kwa uzalishaji wa mazao hayo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba nchi hizi zina faida ya kuwa na nguvu katika ushindani wa soko la viungo kama vile tangawizi, iliki, mdalasini, karafuu, bizari (manjano) na pilipili manga kwa kuwa na hali ya hewa na udongo unaoruhusu kilimo cha viungo. Kihistoria, zimekuwa pia miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa viungo.

Kampuni hiyo inajihusisha na uchakataji wa viungo vya ogani na vile vinavyozalishwa kwa kutumia mbolea za kisasa, dawa za kukuzia na kuulia wadudu. Kuongezeka kwa uelewa wa watu na kukua kwa mahitaji ya vyakula vya ogani duniani vimesaidia kukua kwa soko la viungo vya ogani, hivyo kuiwezesha Horizon Group kupata bei bora na faida.

Horizon ina uhusiano wa moja kwa moja na wakulima zaidi ta 3,000 huku ikifanya uangalizi mkubwa kwenye uendeshaji wa shughuli zao za kilimo. Kampuni hiyo huwapatia wakulima mafunzo ya mbinu bora za kukuza kilimo cha ogani. Zaidi ya hayo, imefanikiwa kuwaunganisha wakulima katika vikundi vya ushirika ili kuhakikisha na kuwezesha kupata ithibati ya ogani na ufuatiliaji kamili.

“Tunafurahi kufanya kazi na Aavishkaar Capital tunapoanza awamu nyingine ya safari yetu ya kukua. Uzoefu wao katika kukuza biashara, kuimarisha mifumo ya uongozi, kuwezesha upatikanaji wa soko, na kufungua mitaji utakuwa wa manufaa tunapoijenga Horizon kuwa kampuni inayoongoza katika uchakataji wa viungo,” alisema Jomy Antony, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Horizon Group.

Akitoa maoni yake kuhusu uwekezaji huo, Darren Lobo, mkurugenzi katika kampuni ya Aavishkaar Capiital, alisema: “Tumefurahi kufanya kazi na timu ya kipekee ya Horizon Group, ambayo inaleta uzoefu wa zaidi ya miaka 80 ya utaalamu katika uzalishaji na uuzaji wa viungo, ili kujenga moja ya kampuni kubwa ya kuchakata viungo Afrika.”

“Kiongozi wa Divisheni katika benki ya KfW, Dr Markus Aschendorf, aliongeza: Uwekezaji wetu katika Horizon Group kupitia Mfuko wa Dunia wa kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF) unaakisi dhamira yetu ya kuimarisha mnyororo endelevu wa ugavi Afrika na Asia. Tunaamini kwamba mtaji unaotumika kwa lengo utachochea uwekezaji unaozingatia masuala ya mazingira, jamii na uongozi huku ukifungua ukuaji shirikishi. “
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhani akizungumza leo Septemba 08, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha Tume na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 mkoani Dodoma ambapo aliwataka kutekeleza jukumu walilopewa kwa ufanisi na weledi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhani akizungumza leo Septemba 08, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha Tume na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 mkoani Dodoma ambapo aliwataka kutekeleza jukumu walilopewa kwa ufanisi na weledi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhani akizungumza leo Septemba 08, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha Tume na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 mkoani Dodoma ambapo aliwataka kutekeleza jukumu walilopewa kwa ufanisi na weledi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume, Ndugu Giviness Aswile akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi.
Meza kuu ikiwa katika kikao kazi hicho.
*******
Na. Mwandishi Wetu.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imezitaka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na weledi.


Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhani leo tarehe 08 Septemba, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha Tume na taasisi na asasi hizo kilichofanyika Mkoani Dodoma.

”Ni vyema mkafahamu kuwa kifungu cha 10(1)(g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 22 na 23 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024, zimeipa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu hiyo...


Hivyo, kazi mnayoenda kuifanya ni moja ya majukumu ya kisheria ya Tume na mnapaswa kuifanya kwa weledi na ufanisi mkubwa,” amesema.


Ndugu Kailima ameongeza kuwa, Tume inatarajia kuona kuwa, taasisi na asasi za kiraia zinatoa elimu iliyolengwa haswa kwa kutoa kipaumbele kwenye mambo ambayo yatawapa wananchi, wagombea na vyama vya siasa kwa ujumla uelewa wa namna ya kushiriki kwenye kampeni kwa amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kupata uelewa mzuri wa utaratibu wa kupiga kura.

”Hatutarajii kabisa mtoe elimu ambayo italeta mkanganyiko kwenye jamii na kuiingiza nchi kwenye machafuko kama ilivyotokea katika maeneo mengine hapa Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema.
Amesisitiza kuwa taasisi na asasi hizo haziruhusiwi kuwapa watu wengine au taaisi au asasi nyingine vibali walivyopewa na kwamba vibali hivyo ni lazima vitumiwe na walengwa tu.

”Nyie ndio mabalozi wa Tume, hivyo, mhakikishe katika kipindi chote cha utekelezaji wa jukumu lenu la kutoa elimu, mnazingatia Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ambayo Tume imekuwa ikiyatoa mara kwa mara,” amesema.


Kikao kazi hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa Tume na wawakilishi wa taasisi na asasi 164 zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.


Mada zilizowasilishwa ni pamoja na Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025, Sheria za Uchaguzi, Kura ya Rais Portal (Kura ya Rais Popote) na Mchakato wa Uchaguzi.
Baadhi ya wawakilishi kutoka Serikalini wakifuatilia mada katika kikao kazi hicho cha Tume na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Tume wakifuatilia mada katika kikao kazi hicho cha Tume na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.



Sehemu ya washiriki kutoka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Sehemu ya washiriki kutoka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Sehemu ya washiriki kutoka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu), Dkt. Rose Likangaga akiwasilisha mada kuhusu Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Ndugu Saida Hilal akiwasilisha mada kuhusu Mchakato wa Uchaguzi.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria kutoka Tume, Adv. Cyprian Mbugano akiwapitisha washiriki wa kikao kazi katika sheria mbalimbali za uchaguzi.
Mkurugenzi wa Daftari na TEHAMA wa Tume, Ndugu. Stanslaus Mwita akiwasilisha mada kuhusu Kura ya Rais Portal (Kura ya Rais Popote).


Washiriki kutoka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wakifuatilia mada.

Washiriki kutoka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wakifuatilia mada.
Washiriki kutoka taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wakifuatilia mada.