Upanuzi wa barabara ya Bamaga - Shekilano umeanza na kuendelea kwa kasi kama kamera ya Globu ya Jamii ilivyoweza kuzinasa taswira kadhaa wakati ujenzi huo ukiendelea. Pichani ni katapila likiwa katika zoezi la kusawazisha vifusi vilivyomwagwa barabarani hapo mchana wa leo. Barabara hii ina urefu wa kilomita 3.7. Picha na Emmanuel Massaka.
Muonekano wa Barabara ya Shekilango inayoendela kujengwa.
ASILI YA JINA LA BARABARA YA SHEKILANGO
Watanzania wengi wamewahi kuisikia au kuitumia moja ya barabara maarufu jijini Dar Es Salaam iitwayo "Shekilango Road". Barabara hii, kwa wale ambao hawaifahamu, inaanzia maungio ya "Morogoro road" karibu kabisa na nyumba za NHC zilizo mkabala na kiwanda cha Urafiki ikielekea na kukutana na barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kituo cha Bamaga, karibu na makao makuu ya TBC.
Ingawa wengi wanaifahamu barabara hii, hata hivyo wengi pia, hasa vijana wa Dot.com, hawaelewi jina hili limetokea wapi na wengine wanafikiri limetokana na aina ya miti iliyokuwa ikipatikana maeneo hayo!. La hasha!.
2. Jina Shekilango Road limetokana na nini?
Jina "Shekilango Road" limetokana na jina la marehemu Mhe. HUSSEIN RAMADHANI SHEKILANGO. Huyu alikuwa ni Mbunge wa Korogwe (1975-1980)
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye kabla ya ubunge alikuwa Meneja Mkuu wa "National Milling Cooperation".
3. Mh. Shekilango Alipewa Kazi Maalum Uganda na Mwalimu Nyerere.
Baba wa Taifa, Rais JULIUS KAMBARAGE NYERERE alimpa Mh. SHEKILANGO jukumu maalum la kuwa mratibu kati ya serikali ya Uganda na Tanzania baada ya kumalizika vita vya Kagera. Hii ilikuwa ni heshma kubwa kwa Mh. SHEKILANGO. Ikumbukwe kuwa mara tu baada ya vita hivyo, kilipita kipindi cha mpito cha utawala wa Mh. YUSUPH KIRONDWE LULE na Mh. GODFREY LUKONGWA BINAISA kilichokuwa na sintofahamu na machafuko makubwa.
Hivyo, Mwalimu alimteua Mh. SHEKILANGO chini ya usaidizi wa Mh. Balozi FARAJI A. KILUMANGA, aliyekuwa balozi wetu nchini Uganda, kuisaidia serikali ya Uganda isimame. Kazi hii waliifanya kuanzia Juni 1979.
4. Mh. Shikilango apanga miadi kukutana na Mwalimu Arusha:
Siku ya Jumapili, tarehe 11.5.1980, Mh. Waziri SHEKILANGO na Mh. Balozi KILIMUNGA walikuwa na miadi ya kukutana na Mwalimu jijini Arusha kwavile Rais NYERERE alikuwa kwenye ziara ya kiserikali jijini humo.
Viongozi hawa walikuwa wakienda kumtaarifu Baba wa Taifa juu ya hali ya usalama ya Uganda baada ya mfarakano kati ya Rais BINAISA na General DAVID OYITE OJOK aliyekuwa Mnadhim Mkuu wa Jeshi UG, mfarakano ulioonesha dalili zote za kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.
5. Mh. Shekilango Akwea "Pipa" kwenda "Geneva ya Afrika"
Asubuhi na mapema siku hiyo ya Jumapili, tarehe 11.5.1980, Mh. SHEKILANGO aliongoza msafara wa maofisa wa serikali ya Tanzania uliokuwa ukitoka Uganda kuelekea Arusha kwa ndege ndogo aina ya Casena 402 yenye uwezo wa kuchukua watu 8.
Watu waliokuwemo kwenye msafara huo walikuwa 7:
1. Mh. Waziri HUSSEIN SHEKILANGO
2. Balozi FARAJI KILUMANGA
3. Mwanadiplomasia IDD MSECHU
4. Cpl. PETRO KALEGI MAGUNDA
5. Pte STEVE MTAWA
6.Luteni MALLYA
7. Luteni LUOGA
6. Mh. Shekilango na Msafara wake Wafariki kwa Ajali ya Ndege
Mwalimu NYERERE akiwa jijini Arusha akisubiri kuhabarishwa na Mh. SHEKILANGO kuhusu hali ilivyo nchini Uganda, alishangaa kuona muda wa miadi ukiwa umepita sana bila ya viongozi hao kufika ili kuonana naye.
Baada ya muda kupita, Mwalimu aliletewa habari za kuhuzunisha na kusikitisha sana na hakuamini maskio yake alipoelezwa kwamba ndege hiyo ndogo iliyokuwa imembeba Mh. SHEKILANGO na msafara wake ilianguka wakati tayari ilikuwa imeishaingia anga ya mkoani Arusha!.
Ndege hiyo ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) iliyokuwa ikiruka kati ya mita 5000 na 7000 kutoka usawa wa bahari ikielekea KIA ilipata ajali na kuanguka kati ya saa 4 na 5 asubuhi katika kijiji cha Engwiki wilaya ya Monduli, Arusha.
Vijana wawili kutoka kijiji cha Engwiki, Bw. MUNDEREI ANGERUKAI na Bw. NUSERIEKI NJONJOLOI ndio waliokuwa mashuhuda wa kwanza wa ajali hiyo waliosaidia kupatikana kwa ndege hiyo iliyolipuka baada ya kugonga kilima cha Kolomoniki kutokana na ukungu mkubwa uliokuws umetamalaki eneo hilo. Askari wa Chuo cha Uongozi wa Kijeshi Monduli walitumia masaa 5 kuitafuta ndege hiyo na vijana hao wawili hatimaye waliweza kuwaonesha ndege hiyo jioni ya Jumapili hiyo ya huzuni ambapo abiria wote walifariki na miili yao kuchukuliwa.
7. Mh. Shekilango azikwa na mamia Korogwe:
Mh. Waziri SHEKILANGO aliyekuwa kipenzi cha wana-Korogwe alizikwa Jitengeni, Mombo, Korogwe , Tanga ambapo mazishi hayo yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu ulioweka rekodi ya aina yake wilayani Korogwe. Katika kumuenzi, shule moja wilayani Korogwe imepewa jina lake pia.
8. Barabara ya "Sinza kwa Wajanja" yapewa jina la Shekilango:
Kwa kuwa wakati huo ujenzi wa barabara ya Sinza ndio ulikuwa umeanza, Uongozi wa jiji la Dar Es Salaam ukaamua kumuenzi marehemu SHEKILANGO kwa kuipa barabara hiyo jina lake. Ingawa wakazi wa Sinza ambao wengi ni wapangaji huji-mwambafy na kuita eneo hilo "Sinza kwa Wajanja", lakini miaka ya zamani Sinza ilikuwa ni uswekeni na eneo lote hilo la Sinza yalikuwa ni mashamba ya mipunga ambao ulikuwa ukistawi sana kwani maji hayako mbali chini ya ardhi na ndio maana hadi leo mvua ikinyesha kidogo tu Sinza , eneo lote huwa ni mafuriko matupu!.
9. Mh. Shekilango aacha Mjane Ngangari:
Marehemu SHEKILANGO, aliyekuwa "amekwenda hewani" aliacha watoto ambao walikuwa wakifahamika kwa urahisi kutokana na urefu wao, pamoja na mkewe Mama ZAPPORA. Marehemu SHIKILANGO alikuwa akiishi Sea View, Dar Es Salaam kwa muda mrefu na baadae familia yake ikahamia kwenye nyumba yao iliyopo Kinondoni Bwawani Kiwanja Na.401 Kitalu 42.
Mama ZAPPORA aliyezaliwa mwaka 1938 alikuwa ni mwalimu hodari sana na amefundisha shule nyingi hapa nchini. Aidha, alikuwa "Headmistress" shule za wasichana Zanaki, Kisutu, Jangwani, Forodhani, Msalato na Iringa girls sec school. Mama ZAPPORA, ambaye ni mmoja wa ma-Headmistress walioweka rekodi ya kuongoza shule nyingi nchini, alifariki tarehe 1.9.2018. Licha ya marehemu SHEKILANGO kufariki, lakini mwanamke huyu ngangari aliweza kuwalea wanae vizuri.
Hivi ndivyo marehemu Waziri HUSSEIN SHEKILANGO alivyofariki na kupelekea barabara maarufu ya Sinza kupewa jina hilo kwa heshimna yake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...