BURIANI MWANANGU AMINA CHIFUPA: PRINCESS WA TANZANIA

Na Ummie-Mahfoudha Alley Hamid

Kifo hakina wakati, huruma wala subira, huja kwa saa na muda uliopangwa na mwenyewe Subhana wa Taala Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwanaadamu hawezi kukipangua. Ya laiti ingelikuwa uwezekano huo upo, basi tungalipangua vifo vya wengi ambao ni vipenzi vyetu kikiwemo hichi cha juzi cha mbunge wa Viti Maalum CCM anaewawakilisha vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Amina Chifupa Mpakanjia.

Wa kale walisema chema hakidumu. Nimeuthibitisha ukweli wa usemi huu kwa kifo cha binti huyu. Marehemu Amina alikuwa na sifa zote za kupendeza. Alikuwa kijana, mrembo, mtanashati, mcheshi, msomi kwa kiasi chake na zaidi ya yote alikuwa mtu wa watu.

Si muda mrefu tangu nimjuwe Marehemu. Nilimsikia sauti yake wakati akiwa mtangazaji wa redio, na nikamjuwa kupitia magazeti na runinga. Nikaja kumjuwa baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa vijana kupitia chama tawala cha CCM. Kabla ya kumjuwa fika, nilikuwa najisemea ki moyo moyo, “Hmmmm, binti kama huyu mwenye sifa zote hizi, kweli atakuwa na uwezo wa kuongea na watu wa hali ya chini anaowawakilisha? Hivi huyu si anaringa na kujiona kuwa hakuna wa kumgusa?” Hakika dhana ni dhambi na kweli nilipata dhambi kwani nilivyomdhania ikawa ni tofauti na nilivyomjua. Ukweli nilijikumbuka mimi enzi zangu nilipokuwa natikisa na namna watu walivyokuwa wanaona najivuna

Nilimwmjuwa Amina kwa muda wa miaka chini ya miwili ya ubunge wake. Aliniita “mama” nikamwitika “mwanangu”. Alikuwa ni mtu “Simpol” kwa lugha ya mjini. Alikuwa mchangamfu na pia alikuwa ni mtu mwenye sikio la kusikiliza watu na shida zao ingawa shida nyengine zilikuwa si rahisi kwake kuzitatua.

Umaarufu, ujana, urembo, wema wake ulimfanya alengwe shabaha na kila chombo cha habari, iwe kwa wema au utelezi alioufanya. Ujana wake ulimfanya awe au afanye mambo mengi ambayo yanafanywa na yalifanywa na wengi ambao walio na umri wake. Binaadamu tunasahau kuwa “ujana ni moshi” na mwishowe hupita tu. Tunasahau kuwa tumepitia hatua zote hizo na zaidi ya hizo katika ujana wetu.

Alifanya mambo ya kawaida ya ujana na urembo, alikuwa mlevi? Sikumfahamu hivyo, mvuta sigara au bangi? Sikumjuwa hivyo, mtumiaji wa madawa ya kulevya? Sikumuona na sidhani kama alikuwa hivyo. Lipi geni alilokuwa nalo Marehemu Amina hata kusakamwa na kudhalillishwa hadi kufikia kupoteza roho yake changa?

Tujiambie na tujiulize, hivi sisi tukiwa kama waandishi wa habari, ni lazima tuwe na habari mbaya (negative) ndio tuandike au ndio ziuzike? Hatuwezi kuwa na upande mzuri (positive) side of issues? Kwa nini muandishi wa habari mwenzetu anaeanza maisha na malengo yake awe ndio chanzo chetu cha habari mbovu zilizopo na zisizokuwepo? Vijarida vya udaku haviuziki bila ya kuwepo uwongo usokifuniko?

Nasema hivi kwa sababu nimesikitishwa na muandishi Eric Shigongo wa gazeti la IJUMAA ambalo slogan yake ni “We belong to God” yaani wao ni waja wa Mungu, na namna alivyomsakama mwana wa watu na kusahau hiyo slogan yake ya kuwa yeye ni mja wa Mungu na Marehemu Amina pia ni mja wa Mungu. Amemuekea makala spesheli ya kumdoboa na kumnazi’i kadmnas bila kimeme. Anamkashifu na kuashiria kuwa Marehemu amefika kumfata kwake na kujitakisha!

Shigongo amemkejeli Marehemu eti asijifananishe na Mhe. Migiro na Mhe. Meghji. Kwa nini iwe vibaya kuwa na malengo? Hata Waheshimiwa hao walimhusudu Margaret Thatcher, Golda Meyer, Bandaranaike, Madeline Albright, Indira Ghandi na Bi Titi hawa wakiwa wachache tu kati ya wengi. Hakuna aliezaliwa na ujuzi usio weza kufikiwa na wengine. Hakuna kati yetu aliejuwa tu bila kuiga au kuweka malengo. Amemkejeli kwa bezo eti hata nae awe katika NEC na awe Mwenyekiti UVCCM. Mbona huyu Mwenyekiti wa sasa nae ni mjumbe wa NEC? Kwa nini kilicho “Good for the goose” kisiwe “Good for the gander?” Au hii ni kwa sababu ya jinsia yake? Kwa Marehemu alijiwekea malengo kuwa “Even the Sky was not the limit” because there is Outer Space after the sky, and may be that is where she wanted to set the limit.

Nathubutu kusema kuwa nilivyomjuwa Marehemu kwa muda mfupi na tukawa karibu sana kiasi cha kuwa wiki haipiti bila kujuliana hali siamini kama alikwenda kwa Shigongo na kukaa kwa saa sita kupindukia usiku wa manane kwa lengo la kutumia ujanajike wake. Maalesh, na iwe kweli kenda kwa lengo hilo, kwani Marehemu Amina atakuwa wa kwanza kujitakisha? Eric Shigongo hajapata kutaka au kutakwa na mwanamke? Anasema alimshikisha Marehemu kitabu kitakatifu ili aape kama aliwahi kutakiwa na Shigongo, na Marehemu akakataa kukishika; jee Shigongo anajuwa sharia za Kiislamu na sababu zinazomfanya mwanamke wa Kiislamu kukataa kushika Mas-hafu kwa sababu na nyakati fulani fulani?

Shigongo ameendelea na makala zake za kashfa juu ya uhusiano wa Marehemu na Mheshimiwa mmoja bungeni, jee tumuite yey ni mtafiti wa habari za ndani za wabunge wote walio bungeni? Ni kweli anajuwa mahusiano binafsi ya baina wabunge wote au alimkandia Marehemu tu? Kama anazijuwa habari zote mbona asiziandike kwa mapana na marefu na akakazania za Marehemu tu? Mbona asitoe habari za kina za huyo mbunge wa kiume na kumuandama Marehemu peke yake? Wangereza wanasema “It takes two to tango and it takes two to quarrel”. Au hii ni ile dhana ya mfumo dume uliotutawala kuwa mwanamke ndie anaefaa kuitwa M……a (siwezi kuliandika hili neno) na mwanamme anafaa uitwa “KIJOGOO”. Kama kazi hii ni ya wawili, vipi iwe sifa kwa mmoja na kashfa kwa mwengine? Shigongo anaogopa mwanmme mwenziwe na akamuonea Marehemu. Au ana ajenda ya siri?

Nimemjuwa Marehemu Amina kwa muda mfupi, na nikajuwa ni mtu mkweli, muaminifu, mwenye ithibati, asiekwenda kinyume na kauli yake. Nasema hivi kwa uthibitisho kamili nilionao binafsi. Miezi michache nyuma alitowa kauli yake kwa mtu mmoja kwamba angempa msaada fulani. Baadhi ya watu hawakupenda Marehemu afanye vile na akawekwa kiti moto na majopo si mawili si matatu, ya watu wazito sana ili aende kinyume na kauli yake ile. Marehemu Amina aliwasikiliza, na baadae akawajibu kuwa hangeweza kwenda kinyume na kauli yake na kwamba kama alivyoahidi, atampa mtu yule msaada wake.

Hapa niliweza kuona tafauti baina ya Marehemu Amina na wanawake na wanaume wengine wengi, wakiwemo vijana kama yeye waliotokea huko Umoja wa vijana CCM, na wanawake na wanaume wakongwe waliokomaa waliotokea katika vilele vikubwa vya Chama. Tafauti ilikuwa wengi wao walitia ulimi puani na kwenda kinyume na walivyotamka, wengine wakawa washiriki wa kumuweka Marehemu kiti moto na kumtishia kuwa wangemfanyia hivi au vile.

Marehemu Alikuwa hamtishi mtu wala hatishiki au kutikisika. Alikuwa ni mtu ambae akishatoa kauli yake, basi hata ashuke malaika gani haibadili abadan. Aliweka msimamo wa kupiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zake zote, jambo ambalo lingemtetemesha mtu mkubwa na mwenye nguvu. Niliwahi kuongea nae na kumwambia “Mwanangu pole pole, wasije wakakudhuru!”. Kauli aliyonijibu ni kuwa amejitolea nafsi yake katika ukweli na haki na chochote kitachomfika ni maktub na hakifutiki. Kweli kilichoandikwa hakifutiki.

Nikiacha hili nitakwenda kwenye utanashati wake ambao ulifika kumponza bungeni kwa kuambiwa na Mheshimiwa Spika atoke nje ya kikao aende akabadili kivazi kwani hakistahili bungeni. Bila kinyongo Marehemu alitoka na tabasamu na akaenda akafanya kama alivyoamriwa. Binafsi wakati huo mimi nilikuwa katika maeneo ya Bunge Dodoma. Kivazi kilichomponza hakikuwa cha uchi au kuvunja heshima, kilikuwa na kidokezo cha kofia ambapo kwa sharia za bungeni tulizorithi kwa wakoloni, kilipaswa kiendane na uvaaji wa gloves na ndipo kiwe kimetimia. Marehemu Amina alitoka nje na akavua kofia ile na kurudi bungeni. Alifika hata kufanyiwa usaili na stesheni moja ya runinga na ilipoletwamada hiyo Marehemu alicheka na kusema kuwa hiyo ilikuwa ni changa-moto ya ukomavu wake na zaidi ya yote ilikuwa ni funzo la kupitia kanuni kabla kutenda jambo.

Wacha niwambie unafiki wa sisi watu. Kwenye runinga nimeona watu wanalia karibu ya kugaragara na kutiririkwa na machozi wakimsifia Marehemu. Jamani wengine katika hao ni wale ambao walichekelea Marehemu alipoamriwa kutoka nje kwa ajili ya kivazi chake, wengi ya hao walidiriki kumbeza na kusema kuwa pale ni pahala pa kazi na si pahala pa fashen na ubishoo. Wengi wetu ambao wakati umeshatupita kushoto na jua limekuchwa tulijisahau kuwa nasi kwa wakati wetu tulipiga vimini na kutesa mjini. Wengi ya wale ambao bado ni vijana walijawa na wivu wa kutomiliki vivazi vya “designer goods” vya Marehemu Amina, au ki maumbile kutopendeza kama yeye. Wivu na choyo vilitutawala na tukasahau kuwa “kila ndege anaruka na ubawa wake na nyota ya mwenzio usiisafiire”.

Kila mtu ana mapungufu yake. Kwa sasa, ilivyo khulka ya binaadamu, utasikia sifa tu atakazo mwagiwa Marehemmu Amina. Kashfa zitatulia kwa wengi wetu kwa ile dhana ya “Never speak evil of the dead”. Bwana Shigongo alisema katika makala yake ya Ijumaa iliopita kuwa anasitisha kuandika mengine kemkem ya Marehemu Amina na kashfa zake kwa vile ni mgonjwa kitandani. Aliahidi kuwa atatuletea uhondo huo baada ya kupona Marehemu Amina. Naomba nimnukuu marehemu bibi yangu ambae alikuwa ndio mentor (muongozi au dira) wangu. Alipokuwa katika “sakarati-l-mauti” nilikuwa namsomea na kumuombea dua huku nikilia na kumwambia “Bibi utapona”. Alinitupia macho akanijibu “Nikipona nimepona, nikifa nimepona”. Nami namuomba bwana Shigongo aliemsakama Marehemu hata wakati alipokuwa mgonjwa mahtuti kitandani, asitunyime conclusion ya uhondo wa hadithi yake tamu maana sasa Mhe. Amina AMEPONA na ni rukhsa kwake kutumalizia makala yake na asituache na shauku na duku duku la kutaka kujuwa kulikoni.

Kwa makala hii namuombea marehemu Amina malazi pema peponi, Mungu amsamehe madhambi yake, ampe kauli thabit, ampe kitaabu chake kwa mkono wa kulia, malaika wema wawe marafiki na wapokezi wake kaburini, apate nuru katika kaburi lake, liwe linatoa harufu ya rehani nasumini na mawaridi, awe mkono wa kulia wa Bwana Mtume siku ya Kiama pamoja na Ma-abrar wema, awape subira wazee wake, mwanawe, marafiki zake na kila aliempenda na aliependwa na Marehemu.

Marehemu Amina namfananisha na Princess Diana wa Uingereza alivyoandamwa na mapaparazi wa ulaya hadi akato(ka)lewa roho yake. Wema, Utanashati,ukarimu, ukweli, huruma, usaidizi na mengi mazuri ya Princess Diana yanafanana na yale ya Mrehemu wetu. Vifo vyao vinatafautiana mazingira lakini vinafanana sababu nazo ni kuandamwa kwa hili na lile. Tarehe pia zinapishana kidogo kama mwezi tu kufikisha miaka kumi kamili.

Diana alikuwa ni Princess wa Uingereza ambae ana andamwa hadi leo miaka 10 baada ya kifo chake. Marehemu Amina ni Princess wetu Tanzania. Natumai Paparazzi wenzangu tutakuwa na hishma za Ki Afrika na utu wa Ki Tanzania na tutamwacha marehemu apumzike kwa amani baada ya kumpa Bwana Shigongo nafasi ya mwisho ya kutueleza yaliyobaki juu ya Marehemu Amina. Baada ya hapo tutamwachia Mungu atamhukumu kwa amali zake nzuri, na zikiwa mbaya atamsamehe.

Naomba kumaliza kwa kunukuu maneno ya Jesus Christ alipowambia Mayahudi walipokuwa wanataka kumpiga mawe Mary Magdalene kwa sabau eti alikuwa mzinzi. Jesus aliwaambi hivi: “Let that among you with no sin cast the first stone”. Yaani naanze kati yenu yule asie na dhambi kutupa jiwe la kwanza. Jee tupo kati yetu tulio malaika bila dhambi? Tukumbuke kuwa mtu akimyooshea mwenziwe kidole kimoja, basi vidole vine vinamgeukia yeye na kumsuta. Upo Bwana Shigongo?


Buriani mwanangu Princess Amina. Mungu akulaze pema peponi Amin.

Wakatabahu

Mahfoudha Alley Hamid

E mail:
umimah@zanlink.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 15 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 01, 2007

    Hivi Michuzi hizo makala za Shigongo kuhusu maisha ya Amina Chifupa ilikuwaje, kama makala hizi zilianza kabla Amina hajafariki, yeye binafsi alizikubali? mbona hapa haieleweki, itakuwaje mtu akutukane kwenye magazeti na wewe umchekelee tu bila kuchukua hatua yoyote.

    Tunaomba update ya hiyo mzee

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 01, 2007

    Michuzi tunaomba basi angalau kwa kifupi tukandamizie highlights za hiyo makala ya Eric Shigongo.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 01, 2007

    Mimi maoni yangu namuonea huruma sana huyu mbunge kwa vile nafikiria kuwa amelipa madhambi ya watu wengine kwa maisha yake. Amefariki mapema na kosa sio lake lakini kosa naliona ni la nchi yetu na priviledges zake. Kweli ninafikiri ni vilio vya watu wengine vimemuondoa huyu dada.

    Ukiangalia maisha yake na elimu yake shuleni tuseme ukweli alikua sio mtu wakufika hapa alipo kwa mda mfupi huu. Kuna watu walifaulu vizuri sana tu shuleni lakini kutokana na priviledges alizokua nazo na jila kubwa alilobeba basi kila milango ya mambo yake yeye ilikua inafunguliwa kiurahisi rahisi tu. Utakuta kuna nafasi alizipata kiurahisi kwa vile yeye alikua mtoto wa fulani lakini mwingine aliyenyimwa hiyo nafasi alikua anastahili na alikua anashida sana lakini hakupewa. Machozi ya masikini na mnyonge hayaendi bure.

    Watanzania vikirieni hivyo mnapotoa au kufanya mambo mfanye kwa haki mnasababisha vijana wa watu wanaondoka bado wakiwa wadogo. Kama mngefuata sheria kweli wasingeondoka bado wadogo hivi kiajabu ajabu tu.

    kweli alikua mchapakazi lakini baada ya kupata hiyo kazi.

    Hii yote ni toka mwanzo wa ulimwengu adamu alilaaniwa na wengine tukalaaniwa hiyo hiyo ka ajili yake.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 01, 2007

    RIP Amina,lakini mama mbona unajiharibia jina lako hivyo kuliweka kidhungu?ninavyojua jina lako ni,
    UMI Mahafuz Ali Hamid sio ndio kiswahili sanifu kwa nini jina lako ulifanye la kidhungu?????

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 01, 2007

    Hi Bro Michuzi! Kweli kifo cha Amina kimemgusa karibu kila mbongo ndani na nje ya TZ, sasa hebu mh. Michuzi tubandikie tafadhali walao dondoo za bwana Eric wa Shigongo walao tulio ughaibuni tusome nini kilikuwa kinaandikwa na huyo mwandishi. Mama kaeleza yake ila si wote tulopata kuyaona na kuyaoma maneno ya Shigongo.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 01, 2007

    Mama mi mpaka leo siamini kama amina kafariki.nahisi yupo tu. na huyu shigongo huyu nyi mwacheni naye malipo yake atayapata hapahapa duniani.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 02, 2007

    shigongo alikuwa na haki ya kusema kwa amina chochote kama alivyomfahamu, ikiwa ni haki yake ya kusema kama Mtanzania. Amina lazima muelewe alikuwa maarufu na mtu tofauti sana, ilikuwa vigumu kuacha kufuatwa na media, kama alikuwa princess Dianna wa Bongo, ataepuka vipi aliyofanyiwa na mapaparazi Princess dianna wa uingereza?

    ReplyDelete
  8. AnonymousJuly 02, 2007

    Michuzi tutumie hizo dondoo za shigongo tuzisome.Ila kama Shigongo alimtusi Hayati Mhe.Amina mbona yeye ana machafu mengi tuu ambayo anayatenda akiwa kama binadamu.Ajisafishe kwanza kabla ya kumtuhumu mtu yeyote.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJuly 02, 2007

    bwana michuzi mi nimepata hii barua ingine naambiwa imetoka kwa Zitto Kabwe. sina ushahidi. lakini nilivyoisoma imenitoa machozi na kunikumbusha Amina ambae sikumfahamu mbali ya kumsikia tu.

    labda wapeperushie na`wengine wapate kumjua Amina alivyokuwa na hamu ya kufika mbali.

    wasalaam

    XYZ



    AMINA, umetangulia kwa Mola. Umetutoka tukiwa bado tunakuhitaji. Taifa lako ambalo ulianza kulitumikia ukiwa kijana mdogo linakulilia. Nchi imezizima, hakuna anayeamini.

    Safari hii ni yetu sote, wewe umeanza. Msalimie Bibi Titi. Unakumbuka nilikuwa nakwambia kupitia kwako namwona Bibi Titi?

    Wengi wanadhani wanakujua. Umeondoka bila kuwaonyesha kuwa wanakujua ndivyo sivyo. Kila mtu anasema chake kutokana na ama amesikia nini au amekuona katika nini.

    Unakumbuka ulipochaguliwa kuwa mbunge watu walisemaje? Eti hata Amina naye kawa mbunge? Utafanya nini bungeni. Haikukuchukua mwaka ukawaonyesha tofauti. Ukafanya yale ambayo wengi kwa kweli yalitushinda kufanya. Ukaanza vita kubwa na ngumu ambayo hujaimaliza mpaka unaingia kaburini leo. Hata hivyo si lazima umalize vita uliyoianza. Edward Mondlane wa Frelimo alituaga kabla hajaona mwisho wa vita aliyoanzisha ya kumng'oa Mreno Msumbiji. Kina Samora wakamaliza vita hiyo. Umeianza vita, tutaimaliza. Umetupa changamoto.

    Swali lako la mwisho bungeni lilihusu wizi wa mitihani. Hukupata bahati kuliuliza. Uliuliziwa na jirani yako, Ruth Msafiri, wa Muleba Kaskazini. Najua kama ungekuwapo ni aina gani ya swali la nyongeza ambalo ungeuliza. Nilikuangaza kule unakokaa sikukuona. Lakini nilijua utarudi muda si mrefu.

    Amina ulikuwa mwepesi kujifunza na wala hukuona aibu kuomba msaada, tena bila kujali itikadi ya chama ya unayemwomba msaada. Mimi nilikutana nawe kwa mara ya kwanza pale tulipoitwa na Mheshimiwa Spika kuhesabu kura za kumthibitisha waziri mkuu. Tukapeana namba za simu na kupoteana tukiwa tunasalimiana pale tunapoonana tu. Sikutegemea hata siku moja kama utakuwa karibu yangu kiasi tulichofikia. Niseme kweli, hata mimi nilikuwa najiuliza utafanya nini bungeni wewe, nikijisemea kuwa wewe ni kilaza tu.

    Rafiki yangu, na pia rafiki yako kipenzi, Omar Ilyasambe, kwa sasa yupo masomoni nchini Marekani, alinitahadharisha nisiwe kama watu wengine wanaokutafsiri kwa ujumla. Akaniambia nikupe muda wa maongezi na msaada kwa yale ninayoyajua. Urafiki ukaanzia hapo. Urafiki wa kujifunza na kujadiliana mambo mengi ya nchi yetu.

    Nakumbuka ulikuwa unanilaumu kwa kuwa mkali kwa serikali yako ya CCM na kwamba wakati mwingine nazidisha. Nilikwambia ndiyo kazi yangu katika upinzani. Ulinielewa. Tulijadiliana maswali yetu na maswali gani ya nyongeza kuuliza. Tulijadiliana kuhusu masomo yako na masomo gani ya kuchukua katika juhudi zako za kutafuta elimu.

    Tulibishana sana kuhusu ni wapi ukasome shahada yako ya kwanza. Wewe na Omar mkitaka uende kusoma nje, mimi nikitaka usome hapa hapa nchini ili pia ufanye kazi zako za ubunge. Niliwashinda na kweli ukaanza kusoma. Ukajitahidi kusoma kwa bidii sana. Walimu wako watakukosa.

    Amina, ulikuwa na malengo makubwa sana katika maisha yako. Ulianza kujiandaa kuongoza umoja wa vijana wa chama chako katika matayarisho ya kupata mafunzo thabiti ya uongozi. Mapema kabisa ulianza kupambana na vikwazo, lakini hadi unaanza kuumwa, zote uliona ni changamoto tu za maisha ya kisiasa. Siku uliyoanza kuumwa ulikuwa uende Lindi kufanya kazi za vijana, lakini pia kujiandaa na changamoto za uchaguzi mwakani. Masikini umeondoka na ndoto yako. Inauma sana kukupoteza.

    Wakati tunaokujua tukitafakari kuhusu kifo chako, hatuoni tumempoteza mbunge tu, tunaona tumepoteza mpiganaji mahiri. Mpiganaji wa mstari wa mbele katika vita ya kunusuru taifa kutokana na ubadhirifu wa mali za umma. Wakati mwingine tunaona tumepoteza kamanda mwema, mwenye uwezo wa kupata habari zote za adui na kushauri njia bora za kukabiliana na adui.

    Amina, maisha yako yana tafsiri nyingi. Umepitia mambo mengi sana. Ulitaka kuandika kijitabu kuhusu maisha yako ili watu wakujue vizuri. Wakati tunajiandaa kukusanya vya kukusanya, ukawa mgonjwa. Umeondoka kabla hujakamilisha azima yako. Bado watu hawakujui. Tutakamilisha kazi yako ili vizazi vijavyo vijue kuwa kulikuwa na kijana kiongozi mahiri mwenye msimamo thabiti.

    Amina niseme nini kukuelezea wakati tunakupumzisha pumziko la kudumu? Maneno hayaji, vidole vinatetemeka. Tutakukumbuka. Ucheshi wako na umahiri wako katika kuhakikisha unapata unachokitaka.

    Usiku wa tarehe 6, Mei ulinipigia simu kuniambia kuwa Mkwawa anakuita, na kwamba Mwalimu Nyerere ananipa salamu. Mimi naomba uwape salamu. Uwaambie nchi yao ipo inaendelea, na kwamba huna uhakika ndoto yao ya kujenga taifa imara itafikiwa karibuni. Waambie Mkwawa na Mwalimu kuwa siku hizi ili uwe kiongozi ni lazima upande mabegani mwa mwingine na kumwangusha na wala si uwezo wa mtu.

    Amina, nakutuma kwa Bibi Titi, mwambie kuwa juhudi zake za kutaka mwanamke, tena mwanamke wa Kiswahili kuonekana ana uwezo wa kuwa kiongozi, bado zinaendelea, na wewe umeziacha zinaendelea. Umefanya kazi yako, umewaachia kijiti wengine wafanye pia.

    Nenda Amina, nenda kapumzike. Umetuonyesha kuwa vijana tunaweza. Tumejifunza, hatutakuangusha.

    source : www.freemedia.co.tz

    ReplyDelete
  10. AnonymousJuly 02, 2007

    tafadhali MICHU tusaidie tulio wengi ambao hatukupata kuisoma hiyo makala ya SHIGONGO tuwekee TUNAKUSIHI SAAAAAAAAAAAAANAAAAAA.
    TUNAISUBIRI KWA HAMU...ASANTE

    ReplyDelete
  11. AnonymousJuly 02, 2007

    DADA AMINA NAKUPONGEZA SANA KWA MANENO YAKO KWANI ULICHOONGEA NO COMMENTS. NAAMINI HATA ULE WIMBO ALIOIMBA LADY JAY DEE WA KUSEMA MMENISEMA SANA JAMANI HAMCHOKI?NAFIKIRI ALIMSAIDIA MAREHEMU AMINA KUWAPA WATU UJUMBE KWANI IT WAS TOO MUCH ANYWAY NAAMINI KIFO CHA AMINA NI CHA MAPENZI YA MUNGU NA KWA BAHATI NZURI MTOTO WA WATU ALIKUWA NA NYOTA KUBWA SANA NDIO MAANA DADA ANAMFANANISHA NA PRINCESS DIANA. JAMANI AMINA AMEKUFA HATUTAKIWI TENA KUMSEMA.

    ReplyDelete
  12. AnonymousJuly 02, 2007

    wadau labda mnasahau,ili bifu la amina na shigongo si la leo wala juzi.actualy amina ni victim wa circumstances,si unajua ugomvi wa tembo nyasi kuumia?mgomvi mkubwa wa shigongo ni clouds fm(ruge na joe kusaga)na huko nyuma walishapelekana hadi kwa pilato. amina alitumiwa na erick kumalizia hasira zake maana ruge na joe kusaga mashine kubwa hivyo hakuwa na gea za kuwaingia?wadau mpo hapo?

    ReplyDelete
  13. AnonymousJuly 02, 2007

    nimependa sana huyo mama alivyonukuyu kuhusu kaburi la mweshiwa kipenzi chetu amina kuwa malaika wazunguke kaburi lake, kutoe harufu za asumini na ./..........kwa kweli yaelekea alikuwa damuni sana, afu kama ni mama wa kiislamu wewe nafikiri mme wako ana raha sana maneno yako ya kinywani ni matamu sana na yanamtoa mtu pangoni. kwa kweli mimi na mvivu kusoma habari ndefu lakini imenivutia nimeisoma mpaka mwisho. nakushauri japo msilamu usomege na biblia yetu siku moja kuna mashairi ya WIMBO ULIO BORA,basi naona utaongeza maarifa mazuri na kauli nzuri, keep it up
    mbilikira@hotmail.com

    ReplyDelete
  14. AnonymousJuly 02, 2007

    weee anony wa july2,2007 5;04;00 pm mbona umetuacha njia panda jamani!!! pliz tufafanulie kiduchuuu yaani inamaana shigongo na amina wametoka mabli cnc amina afanye clouds fm!!?? mmmh hii sasa kali,watu wanaficha makucha mpaka wakorofishane ndo yanafunguka! pliz tudokeze kidogo cz naona michu hataki kutupa dondoo hata za magazeti ya eric mwenyewe.

    ReplyDelete
  15. AnonymousJuly 03, 2007

    MIE NAMSHANGAA BWANA MICHUZI ANAVYOIBANIA HII ISSUE YA BWANA ERICK SHIGONGO. KWA KUMKUMBUSHA TU BWANA MICHUZI, NAOMBA ATAFUTE GAZETI LA IJUMAA LA WIKI YA KWANZA NA WIKI YA PILI YA MWEZI JUNI. KWENYE FRONT PAGE ALIANDIA "waraka wa shigongo kwa amina chifupa", WARAKA HUO ULIKUWA NA SEHEMU YA KWANZA NA YA PILI, KWA MAANA WIKI MBILI MFULULIZO. WIKI YA TATU, NAFIKIRI BAADA YA KUSHAURIWA NA WAUNGWANA KUWA AACHE KUTOA HUO WARAKA, NDO AKASEMA ANASITISHA, NA BAADA YA SIKU KADHAA AMINA AKATUTOKA DUNIANI.

    KWA KIFUPI ALIAMUA KUMKASHIFU AMINA, UKIACHA ILE TABIA YAKE YA KUANDIA HABARI MBALIMBALI ZA AMINA, HIYO KWAKE ALIIFANYA MAALUM, KUMKASHIFU.

    MICHUZI KWA MSAADA HUU, WATAFUTIE WAPENDWA HABARI KAMILI YA HILI.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...