Na Mwandishi Maalum, Songe, Kilindi, Tanga

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa kamwe Serikali yake haifanya jambo lolote ama kuchukua hatua yoyote ya kuhujumu ama kudhoofisha shughuli za mashirika ya dini, viongozi wa dini ama madhehebu yoyote ya dini nchini.

Aidha, Rais ametaka taasisi na viongozi wa dini zote nchini kushirikiana na Serikali katika kuwabaini na kuwabana wajanja wachache ambao wamekuwa wanatumia kivuli cha dini kutumia vibaya misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali kwa taasisi hizo za dini.

Amesisitiza kuwa kamwe Serikali haitatoza kodi vifaa vya kiroho ama huduma za kijamii ambazo zinaendeshwa na dini mbali mbali nchini.

Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo wa uhusiano kati ya Serikali na dini mbali mbali nchini na kuelezea sera ya misamaha ya kodi wakati alipofungua rasmi Hospitali Teule ya Wilaya ya Kilindi, Mkoani Tanga, leo, Jumamosi, Juni 27, 2009 mjini Songe.

Rais amesema kuwa uhusiano mzuri kati ya Serikali na dini mbali mbali nchini ni wa jadi na wala uongozi wake kamwe hauwezi kufanya jambo lolote ama kuchukua hatua yoyote kuharibu uhusiano huo.

“Lakini karibuni kulitokea kutoelewana kuhusu malipo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye baadhi ya shughuli za taasisi za dini. Nia ya Serikali haikuwa kuharibu uhusiano wetu wa jadi, bali kuwabana wajanja wachache wanaotumia vibaya misamaha hiyo ya kodi.

“Hata hivyo, tumefanya kikao cha pamoja kati ya Serikali na dini na sasa tunaelewana. Sote tunakubaliana kuwa lipo tatizo, tena tatizo kubwa, la watu wachache wajanja wanaotumia misamaha ya kodi vibaya na kuyapaka tope taasisi na viongozi wa dini. Vile vile, sote tumekubaliana kuwa lazima tushirikiane katika kumaliza tatizo hili,” amesema Rais.

Amefafanua kuwa pande zote mbili zinakubaliana kuwa lipo tatizo la matumizi mabaya ya misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali, kwamba kazi hiyo inafanywa na watu wachache na kuwa Serikali na dini zitashirikiana kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kwa kuwadhibiti wajanja hao.

“Kuna shirika la dini limepata kuagiza magari madogo 33 na yakaingizwa nchini bila kulipiwa kodi, lakini baada ya muda mfupi hata gari moja likawa halionekani likifanya kazi. Kuna kanisa moja lina gari moja tu, lakini kila mwaka limekuwa linapata msamaha wa kodi kuingiza nchini matairi 45,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Vifaa vingi vya ujenzi vinaingizwa nchini bila kulipiwa kodi, lakini vinaishia vikijenga nyumba za watu binafsi, siyo nyumba ya padre ama ya sheikh.”

Rais Kikwete amesema kuwa kuruhusu wajanja wachache kutumia vibaya misamaha hiyo ya kodi ni jambo ambalo linavunja heshima ya Serikali yenyewe na hata ya viongozi na taasisi za dini.

“Dini ndiyo kipimo cha juu kabisa cha uadilifu katika maisha ya binadamu. Tukiruhusu misamaha hii kutupata tope, wananchi wanaweza kupoteza imani kwa mashirika na taasisi ya dini, na wananchi wakipoteza imani katika viongozi na taasisi za dini watakuwa hawana mahali pa kukimbilia,” amesema Rais.

Amesisitiza Rais: “Tusiwape fursa wajanja wachache kutumia jambo hilo jema kuvunja heshima yetu …tukiliruhusu hili, heshima ya viongozi wa dini itakuwa shakani.”

Rais amesema kuwa wakati umefika sasa kumalizana na suala hilo la msamaha ya kodi. “Katika siku za karibuni yamekuwapo maneno mengi, kila mtu akisema lake…wa Bakwata wakisema hili, wa TEC wakisema lile… wa CCT wakisema lao, wa Pentekoste nao wakisema ya kwao.”

Amesema Rais, “mmoja akisema Serikali hii inawabana Wakristo, mwingine akisema Serikali hii ni ya makafiri …inawabana Waislam. Haya yote siyo ya kweli. Na maadamu sasa tumeelewana na kukubaliana kuhusu hili basi nawaombeni viongozi wa dinia tuache kuwapotosha waumini wetu.
"Hili ni tatizo letu sote, tushikiane kulimaliza kwa nguvu za pamoja", amesisitiza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 28, 2009

    Mimi nauliza, Je kama hao wajanja wanaotumia taasisi za dini kukwepa kodi wakabainika kuwa ni baadhi ya mafisadi ambao serikali inawalinda Mzee JK atawachukulia hatua? Au ndio itakuwa blah....blah..blaah..kama tulivyozoea

    ReplyDelete
  2. kaka hamna cha Padri wala sheikh au askofu ukikubali taasisi yako itumiwe na hao wajanja ina maana nawe wala ten percent kwahiyo nawe ni mwizi kwa nini ukubali mwizi ni mwizi tuuuuuuuuuuuuu kaka ni tu.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 29, 2009

    kama serikali ilmebaini kuna wajanja walitumia vibaya misamaha wakamatwe tu, hata kama ni mashekh au mapadri wote ni waovu tu wasionewe haya.haiwezekani mtu nje ya taasisi hizo akajinufaishe lazima alishirikiana na viongozi wa dini.pia sikuelewe kwa nini viongozi wa dini au vyombo vya habari vilitumia muda mwingi bila kufafania vitu vilivyoingizia kodi,badala yake wakatupotosha kama vile hata vifaa vya ibada,elimu na afya! kumbe ni magari, mitumba na vifaa vya ujenzi tu.hapo inaonekana kulikuwa na mianya ya biashara.jamani hivi sisi tumuamini nani?

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 29, 2009

    ni pale makusanyo ya kodi yanapotafutwa adi basi...kwa kuweka kodi mpya

    miaka yooote iyo mlikua wapi kuliona hili la mashirika ya dini??

    kodi zenyewe hatuona +ve impact kwa nchi hii...

    tit for tat...ukitaka kula shurti uliwe kidogo-mnawakamua mashirika nyie mwala so nao wala!!!!

    na vijana wenu wakiingia ktk system nao wale tu

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 30, 2009

    JK , wewe ndio rais una nguvu zote unawajua wajanja wachache wanaotumia tax excemption vibaya wachukulie hatua lakini usiwahukumu watu 99% ambao wanafuata sheria, wewe ndio rais unalalamika badala ya kutumia power yako tuliokupa kwanini? huu ndio unaitwa USANII rungu tumekupa unalo mkononi tumia acha kulalamika

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...