Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bi. Blandina Nyoni akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu utekelezaji wa kampeni ya utoaji wa Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Polio watoto chini ya miaka mitano kwa mikoa ya Rukwa na Kigoma litakalofanyika tarehe 4 hadi tarehe 7 mwezi Oktoba 2010. Kulia ni Mganga mkuu wa Serikali Dr. Deo Mutasiwa.

Na. Aron Msigwa - MAELEZO.

Serikali imewataka wananchi wa mikoa ya Kigoma na Rukwa kushiriki kikamilifu katika awamu ya pili ya zoezi la utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa kupooza (polio) kwa watoto walio chini ya miaka mitano litakolofanyika tarehe 4 hadi tarehe 7 mwezi Oktoba, 2010.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bi. Blandina Nyoni amesema kuwa hatua ya kufanyika kwa zoezi la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto katika mikoa hiyo, inafuatia taarifa ya kutokea kwa mlipuko wa Ugonjwa huo katika wilaya ya Kalemie nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mwezi Agosti mwaka huu.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ilichukua hatua za haraka za kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini kutokana na jiografia kati ya Tanzania na DRC ,pamoja na muingiliano wa watu katika maeneo hayo kwa kuihamasisha jamii na viongozi wa ngazi zote mkoani Kigoma na Rukwa na wadau wengine kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo .

Mbali na hatua hiyo amesema, serikali iliendesha zoezi la kutoa chanjo ya polio kwa watoto wote walio na umri chini ya mika mitano kwa njia ya Kampeni , Kuimarisha utoaji wa taarifa za wagonjwa waliopata ulemavu wa ghafla na uimarishaji wa utoaji wa chanjo za kawaida ambapo matokeo ya zoezi la awali yanaonyesha mafanikio kwa kufikia kiwango cha asilimia 90 ya chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano.

Amesema mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) unabainisha kuwa ili kudhibiti mzunguko wa virusi pori vya ugonjwa wa polio ni muhimu kutoa chanjo za ziada kwa njia ya kampeni kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka angalau kwa awamu mbili.

Hata hivyo amefafanua kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo watahakikisha kuwa vitendea kazi kwa ajili ya Kampeni hiyo zikiwemo chanjo na vifaa vingine vinaapatikana katika muda muafaka .

“Kampeni na zoezi la utoaji wa chanjo hii katika mikoa ya Rukwa na Kigoma litafanyika kwa mafanikio makubwa kutokana na kuwepo kwa vifaa muhimu kwa shughuli hiyo ambavyo tayari vimeanza kusambazwa” amefafanua Bi.Nyoni.

Amesitsitiza kuwa chanjo hii ya Polio itakayotolewa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wapatao 703,389 katika mikoa yote miwili ni salama na itatolewa na wataalam wa afya kwa njia ya matone kinywani kwa watoto wote bila kujali kama walipata chanjo hiyo hapo awali au hawakupata.

Ametoa wito kwa wazazi na wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hili kwa kushirikiana na wataalam wa afya watakaopita nyumba hadi nyumba na kuongeza kuwa watoto wote watakaopata chanjo hiyo watawekewa alama maalum katika kidole kidogo cha mkono wa kushoto ili kusaidia ufuatiliaji na uhakiki pamoja na kuweka alama kwenye nyumba zitakazofikiwa kulingana na hali ya chanjo ya watoto waliopo katika nyumba hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...