Na Profesa John Mbele
Mwaka huu, wanafunzi niliowaleta Tanzania kutoka Marekani wamepata fursa ya kujifunza kuhusu u-Islam kutoka kwa wahusika wa dini hiyo. Nilitaka wapate fursa hiyo, ili wapate mwanga angalau kidogo kuhusu dini hiyo, na pia waifahamu Tanzania kama nchi yenye dini mbali mbali, na waweze kujua tunavyoishi pamoja. 

Mimi kama m-Kristo, ninaweza kuelezea masuala ya u-Kristo Tanzania kwa kiwango cha kuridhisha. Vile vile, kutokana na juhudi zangu za kujielimisha kuhusu dini mbali mbali, ningeweza kutoa maelezo kuhusu u-Islam, kama ninavyofanyaninapofundisha fasihi.

Lakini niliona ni muhimu kuwapa wanafunzi hao fursa ya kukutana na kujifunza kutoka kwa viongozi wa dini ya ki-Islam. Fursa nzuri ilijitokeza tulipokuwa Kalenga, mkoani Iringa, kwenye Makumbusho ya Mkwawa. Hiyo ilikuwa ni tarehe 11 Agosti. Baada ya ziara ya makumbusho, niliona msikiti, nikamwambia mkurugenzi wa makumbusho, ndugu Nicholaus Kulanga, kuwa ningependa kuonana na imam wa msikiti, ili anisaidie kuwaelimisha wanafunzi wangu kuhusu u-Islam. Mkurugenzi aliahidi kututambulisha.

Siku ya pili, alasiri, tulienda tena Kalenga, tukapata fursa ya kuongea na Imam Zuberi Suleiman. Nilimweleza lengo na madhumuni yangu, yaani kuwapa wanafunzi wangu fursa ya kuelewa kidogo kuhusu u-Islam, kwani fursa za aina hiyo ni nadra Marekani, na wa-Marekani wengi hawaelewi chochote au wana mawazo potofu kuhusu u-Islam.

Imam, anayeonekana pichani amevaa kanzu na kofia, alivutiwa na ombi hilo, akatuongoza hadi kwenye msikiti wa mwanzo wa Kalenga. Wakati anajiandaa kuongea nasi, alimwita pia mwenzake, ambaye ni Ustaadh Maneno, akajumuika nasi.

Imam na Ustaadh walitoa maelezo ya chimbuko la u-Islam na misingi yake kwa ufasaha kabisa. Hata mimi ambaye ninaelewa mambo kadha wa kadha kuhusu u-Islam nilipata mwanga mpya. Imam alinionyesha kitabu kiitwacho "Tafsiri ya Sehemu ya Kumi ya Mwisho ya Qur'an Tukufu." Nilivutiwa na kitabu hiki, na nitakinunua.

Sote tulifurahi kupata fursa hii ya kuongea. Nilijisikia vizuri pale Imam na Ustaadh waliposema wamefurahishwa kuwa nafahamu mengi kuhusu u-Islam. Wakati tunaagana, Ustaadh Maneno aliwapa majina mapya hao wanafunzi: huyu mvulana jina lake ni Abdi Karim na huyu dada jina lake ni Bi Aisha. Jambo hili lilitufurahisha wote, tukacheka kwa furaha. Niliwaeleza hao wanafunzi heshima ya majina hayo katika u-Islam, na kuanzia siku ile nimekuwa nikiwaita kwa majina hayo.

Tumejenga uhusiano mzuri hapo Kalenga. Mwakani, Insh'Allah, natawapeleka wanafunzi wengine hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Umefanya vyema prof.

    ReplyDelete
  2. Hi Prof,
    Sio siri mimi ni mfuatiliaji mkubwa wa mijadala yako na huwa ninauamini sana uwezo wa elimu, kwani katika dini ya kiislam Mtume wetu Muhamad anasema, "Wasomi ni kama warithi wa mitume" (M/Mungu ni mjuzi zaidi), hapo Mtume anamaanisha kuwa wasomi wanaweza kuuongoa umma kutokana na elimu yao na kujua kwao ikiwa kutatumika vyema, nakutokana na hivyo huwa naipenda mijadala yako kwakuwa huwa naamini inatoka kwa mtu msomi. Pili nimefurahishwa sana kuwapeleka hao wamarekani kwa huyo shekh, tena kwa uelewa wangu mdogo tu yaonekana huyo shekh ni muelewa na mwenye busara sana kwani hapo naona amekaa na wageni wake kitako bila kuwabagua. Napenda nikujulishe ya kuwa mimi ni msomi mzuri kiasi wa uislam na nimeusomea ktk nchi za kiarabu wakati nasoma degree yangu ya kwanza ya Computer Science, lkn sio siri nilikuja kugundua kuwa uslam ni dini moja nyepesi sana na nzuri sana hususan ukifundindwa na watu wanauijua vyema dini hiyo na misingi yake.

    asante sana Prof na endelea na moyo huo huo

    Muddy (muddynice20@gmail.com)

    ReplyDelete
  3. Mzee wa BunjuSeptember 08, 2011

    Allah atakujazi, haya ndio yanayotakiwa, hata mimi niliwahi taembelea cathedro moja kubwa na ya kale sana kama miaka 500 nyuma huko Ubeligiji katika mji wa GENT, japo muislam lakini nilifurahi kupata historia ya kanisa


    Mzee wa Bunju

    ReplyDelete
  4. HUYO DADA MBONA HAJAJISTIRI?.....UDHUUUUU!!!

    ReplyDelete
  5. Ahsante sana Profesa kwa moyo wako kuwaunganisha biaadamu wote bila kujali itikadi zao.wewe ni kati ya wasomi wachache ambao hawajathirika na tamaduni za kimagharibi.kwa elimu yako siku zote ungekuwa kama wasomi wengine kuamini kila propaganda za magharibi dhidi ya dini zingine ni ukweli, ila umeamua kufanya utafiti wa vitendo nasi wafuasi tunakuelewa.MUNGU AKUZIDISHIE NA SIKU MOJA UTAIUNGANISHA DUNIA KATIKA TAMADUNI NA DINI TOFAUTI.inshaaala

    ReplyDelete
  6. Prof Mbele umeonyesha kwamba kuwa waumini wa dini tofauti haina maana kwamba udharau yale ya wenzako. Siku zote huwa kuna vitu vya ziada unajifunza ambavyo vinaweza kukusaidia katika maisha yako.

    Hongera sana kwa hiyo approach uliyochukuwa na natumaini wanafunzi wako pamoja na hao maimamu wote wamefaidika kwa kubadilishana mawazo.

    ReplyDelete
  7. Msingi wa maisha ya Watanzania hususani tofauti za dini tangu mwanzo ni ukosefu wa kudharau dini ya mwenzako. Sifa hiyo iliwajaa watanzania tangu utotoni. Prof Mbele kaonyesha jinsi gani watanzania tulilelewa na jinsi gani tunathamini dini au mtazamo wa kidini wa jirani yetu. Sifa hiyo inafaa iendelezwe kwa vizazi vijazo na kudumishwa, ingawa inaonekana kama kuna dalili vizazi vya sasa vinaingiliwa na wachache na kutaka kutuharibia sifa hiyo.

    ReplyDelete
  8. Hongera sana Prof. kwa kazi nzuri. Mchango wako katika jamii ni mkubwa sana . Kitendo hicho kitawafanya hao wageni wavunje stereo type. Maana wazungu wengi hawajui mengi kuhusu Uislam na wengine huogopa hata kumkaribia muislam kwa kuhofia kudhurika kwa namna yoyote ile au hata kupoteza maisha yake.Uislam ni dini ya amani sana na dini inayojali sana mahusiano mazuri na watu au jamii zenye itikadi tofauti na za kiislam. Na ndiyo maana Mtume Muhammad (S.A.W) aliwahusia wafuasi wake kwenda mpaka China kutafuta elimu pamoja na kuwa alikuwa akijua kuwa watu wa huko sio waislam. Dini ya kiislam haina ubaguzi wa namna yoyeto ile. na kuna mengi mazuri sana ndani yake ambayo wengi hawayajui. Kalenga Boy

    ReplyDelete
  9. Ahsante Prof. umenileta nyumbani kabisa ( I prayed in that masjid early this year) Keep up the good job na wahehe wanasema " Gendelege ludodi ulukafu luladenyeka!!!!"
    Kalenga Boy
    Boston

    ReplyDelete
  10. profesa mbele anaonyesha mfano wa jinsi wat wakielimika kiukweli wanaweza kutoka gizani bila taa wala bila kuambiwa na mtu pita huku. elimu ni mwanga na uhuru, profesa yuko huru sasa kwa elimu yake. niambie maprof wangapi wanaweza haya? kazi kupunja marks wanafunzi wa dini nyengine.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...