Waziri wa Uchukuzi Mh. Omar Nundu akipiga kengele kama ishara ya kuorodheshwa rasmi kwa shirika la ndege la Precision Air katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi wa Precision Air Bw. Michael Shirima na mwakilishi wa mamlaka ya hisa nchini Tanzania Bw. Godfrey Malekano.

Precision Air PLC leo imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya hitimisho ya Uuzaji wa Hisa katika soko la Awali.

Uorodheshwaji huo uliendana na sherehe maalum uliohudhuriwa na mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Omar Nundu katika ukumbi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, pamoja na muasisi wa shirika hilo la ndege Bw. Michael Shirima, Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Gabriel Kitua na mwakilishi wa Mamlaka ya Hisa Tanzania Bw. Godfrey Malekano.

Akizungumza wakati wa uorodheshwaji huo Waziri wa Uchukuzi Mh. Omar Nundu ameipongeza shirika la ndege la Precision Air kwa kuweza kuwa kinara wa usafiri wa anga nchini hadi kuweza kufikia hatua ya kuuza hisa zake pamoja na kujiorodhesha katika soko hilo la Dar es Salaam.

“Nawapongeza sana Precision Air, na napenda kuchukua fursa hii kutoa ahadi kama serikali kwamba tutajitahidi kuboresha sera na miundombinu yetu ili kuweza kuinua ushindani pamoja na kuwasaidia mashirika kama yenu kuweza kufanya biashara katika mazingira bora zaidi,” alisema Waziri Nundu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Precision Air Bw. Shirima alisema, “Kwanza kabisa, nawashukuru Mamlaka ya Hisa nchini Tanzania na Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kutuongoza na kutulea kwa moyo wa dhati kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchakato huu. Tunaazimia kuendelea kushirikiana pamoja nanyi ili kuweza kutimiza lengo letu la pamoja la kuongeza thamani ya mwenye hisa katika kampuni; hasa hasa kwa wanahisa watarajiwa.”

Bw. Shirima pia aliwashukuru na kuwapongeza wanahisa wapya wa Precision Air; “Awali juu ya yote kuna wale washirika ambao pamoja na kwamba ni wawekezaji wapya, kuanzia leo katika tukio hili watakuwa wanahisa wa shirika hili la ndege. Napenda kusema ahsante na hongereni sana kwa ujasiri na sifa mlioweza kupatia shirika hili.”

Kwa upande wake naye Mkurugenzi Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Gabriel Kitua alisema kwamba Precision Air ni shirika la 18 kuorodheshwa katika soko hilo, inayofanya Soko la Hisa la Dar es Salaam kushika nambari mbili kwa upande wa Afrika mashariki.

Jumla ya wawekezaji 7,056 (Elfu saba na hamsini na sita) walishiriki katika Uuzwaji wa Hisa katika Soko la la Awali (IPO) iliyoanza tarehe 7 Oktoba na kumalizika Novemba 4 2011.

Shirika limekusanya jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 12 ambazo ni asilimia 43.18 ya kiasi kilichoombwa. Kwa kiasi kikubwa walioomba kununua hisa walikuwa wawekezaji wadogo wa ndani pamoja na Mashirika ya Kitanzania kama ilivyokusudiwa.

Shirika pia hapo nyuma liliwasilisha kwa Mamlaka husika mpango wa kifedha kuonyesha jinsi fedha zilizokusanywa zitakavyotumika na mikakati ya kujaza pengo kuhakikisha malengo ya shirika yanafanikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Pamoja na ukusanyaji fedha kuwezesha upanuzi, shirika pia lilikusudia kuongeza umiliki wa umma hasa wananchi wa Tanzania.

“Tunawashukuru wote walioshiriki kama ilivyothibitishwa na wingi wa ushiriki wao na tunafurahi kuwa zoezi la uuzaji wa hisa za shirika umefanikisha malengo yote mawili ya ukusanyaji wa mtaji na kuongeza wigo wa umiliki wa shirika kwa Watanzania,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Precision Air Bw. Alfonse Kioko.

“Ushiriki mkubwa wa Watanzania ni ushahidi wa kutosha kuwa wananchi wanaimani na matumaini kwa shirika lao la ndege. Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia kuwa uwekezaji wao utakuwa wa ufanisi,” Bw. Kioko aliongeza.

“Mpango wa kuongeza vituo vya usafiri na mtandao ulioko utaendelea. Pia shirika limeanzisha mpango kabambe wa kuimarisha huduma zake kwa wateja,” Kioko alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. inform us more

    ReplyDelete
  2. Upo umuhimu kwa wengi kuhamasishwa kuhusu uelewa juu ya uwekezaji wa HISA,

    Kulinga na upokezi uliochini ya kiwango wa Utolewaji Hadharani wa Mwanzo wa hisa hizi (IPO-Initial Public Offering) kinyume na matarajio wakati mpango huu ni wa manufaa saana kwa faida.

    Mfano wale wanaotumia mamilioni ya pesa kwa biashara ambazo hazikui, haziingizi faida kinyume chake zinakata ,kwa kulipia mapango ya juu ya maduka Kariakoo na kwa kwenda China kununua bidhaa za madukani na kufilisika mitaji yao badala ya kuwekeza ktk hisa za shirika makini ,lenye historia ya maendeleo chini ya Bodi makini ya waendeshaji wenye historia ya mafanikio kama Mzee Michael Shirima.

    Hii ni njia iliyokuwa na ahueni kwa kuwa biashara inafanywa na bodi ya Waendeshaji huko na wewe mwekezaji unafuatilia tu mwenendo na ufanisi wa shirika husika PRECISION AIR kwa uwekezaji uliofanya kwao.

    Kwa vile mambo haya yanakuwa watu wengi hawayaamini kama ni njia ya tija tena zaidi ya biashara za kawaida ambapo wakati mwingine zinazaa hasara!

    ReplyDelete
  3. Wadau inafaa watu waelimike badala ya kuunguza muda na kukata mitaji tubadili mtindo wa kuendesha shughuli zetu kwa biashara ya hisa.

    ReplyDelete
  4. Bora uwekezaji wa ndani kuliko kusafiri mfano kwenda China hasara za haraka ni 4 kama hapa chini:

    1.Kutumia pesa za kigeni US$ kwa kwenda kununulia mizigo China au nje ya nchi

    2.Mara nyingi bidhaa zenyewe zinakuwa hafifu kwa ubora ingawa uchaguzi kwa kiwango cha bidhaa kunategemea ridhaa ya mfanya biashara mwenyewe afikapo huko.

    3.Malezi tete ya watoto nyumbani mmoja anaposafiri nje ya nchi kishughuli wakati mwingine akakaa muda mrefu huko.

    4.Muda mwingi unapotea, wengine wanaanguka ktk mahusiano ya ndani na wenza wao kwa penzi la ugenini safarini nje(mifarakano mingi ya wanandoa imetokana na mmoja kusafiri kikazi /kibiashara nje ya nchi)!

    ni fursa muhimu kuangalia upande wa pili wa sarafu kwa kuwekeza kwa tija ndani ya nchi kama ktk mipango hii ya hisa!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...