Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mohamed Aboud Mohamed akitoa taarifa kuhusu kilele cha Sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi Zanzibar mbele ya waandishi wa habari huko Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar.

Zaidi ya Shs. Million 700 zinatarajiwa kutumika katika kuadhimisha Sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi Zanzibar ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12 Mwezi huu huko katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar

Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari leo huko ofisini kwake Vuga, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed amesema kuwa fedha hizo ni kwa makisio tu lakini taarifa kamili ya matumizi hayo itatolewa baada ya kukamilika kwa sherehe hiyo

Amesema kuwa sherehe za mwaka huu zitakuwa ni tofauti kidogo tu ukilinganisha na miaka iliyopita kwani wanafunzi hawatoshirikishwa wakiwa wamevaa sare zao kwani imeonekana kuwa wananchi wengi watahudhuria sherehe hizo.

Amesema kuwa Kiwanja kilichokuwepo kwa sasa hakikidhi haja ya kuweza kuwachukua wananchi wanaokadiriwa kuzidi uwezo wa uwanja huo ambao ni watu 15 Elfu tu.
Hata hivyo Waziri Aboud amesema kuwa Wanafunzi hawakatazwi kuja kusherehekea wakiwa wamevaliwa nguo zao kama wananchi wa kawaida

Akizungumzia suala la Sherehe hizo kuitwa za Mapinduzi wakati Zanzibar inaendesha Chaguzi zake kwa njia za kidemokrasia, amesema kuwa Neno Mapinduzi ni kitu ambacho kilichowagomboa wananchi wa Zanzibar kwa hivyo Serikali imeona iko haja ya neno hilo lienziwe kwani Mapinduzi ndiyo yaliyowagomboa Wananchi wa Zanzibar kutoka katika makucha ya Wakoloni.

Aidha amewapongeza wananchi wa Zanzibar pamoja na waandishi wa habari kwa mashirikiano yao makubwa ambayo wameyaonesha katika kusherehekea sherehe hizo za miaka 48 ya Mapinduzi tangu kuanza kwake tarehe 4 mwezi huu.

Waziri Aboud ametoa wito kwa wanachi kuhudhuria kwa wingi katika sherehe hizo ambazo milango yake itafunguliwa kuanzia saa 12 za asubuhi siku ya kilele

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. hivi milioni 700 kwa ajili ya sherehe ya mapinduzi kuna tija kweli, na nini chafanyika kutumia pesa yote hiyo? Hatuna shughuli za maendeleo kutumia pesa hiyo. Nawakilisha.

    ReplyDelete
  2. bora hizi hela mngenunua boti mpya na kujenga madaraja Zanzibar kwetu basi..

    ReplyDelete
  3. kauli ya maana ya mapinduzi ya zanzibar inatofaotiana sana kati ya viongozi wetu. Hebu semeni kweli kwa kauli moja isiyo na migongano ili nasi wananchi wa kawaida tuamini dhamira nzima ya Mapinduzi.

    Kutafautiata kwenu munatupa wasiwasi ya kuwa hata nanyi hamuelewi dhamira ya ukweli wa Mpinduzi ya 12 Januari 1964

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...