MAREHEMU GEORGE FREDERICK MBOWE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu George Frederick Mbowe aliyefariki nyumbani kwake usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 29 Februari, 2012 kutokana na ugonjwa wa Kiharusi.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu George Mbowe enzi za uhai wake kama mchapakazi hodari aliyelitumikia Taifa lake kwa uzalendo, uaminifu na uadilifu mkubwa katika sehemu zote alizowahi kufanya kazi ikiwa ni pamoja na katika Utumishi wa Umma.

“Enzi za uhai wake, nilimfahamu Marehemu George Frederick Mbowe kama mtu aliyejituma kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yake na mchapakazi hodari”, amebainisha Rais Kikwete katika salamu zake.  Amesema sifa hizo alizionyesha alipokuwa katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) na hata katika nyadhifa za Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Mwenyekiti wa PSRC na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Rais Kikwete ametoa pole nyingi kwa familia ya Marehemu George Mbowe kwa kuondokewa na mhimili muhimu wa familia, na amewahakikishia wanafamilia kwamba yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwani yote ni mapenzi yake Mola.

Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipumzisha roho ya Marehemu George Frederick Mbowe mahali pema peponi, Amina.
  
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
01 Machi, 2012


NB: Msiba upo nyumbani kwa marehemu Plot. No. 94, Msasani, Old Bagamoyo Road jijini Dar es salaam  karibu na nyumbani kwa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Misa ya kumuaga marehemu itafanyika ijumaa saa nane mchane katika kanisa la Anglican St Alban. Heshima za mwisho zitatolewa pia nyumbani siku ya Ijumaa saa 12 jioni. Mazishi yatafanyika Dodoma siku ya Jumapili saa kumi jioni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kitu ambacho huwa sielewei ni kwani nini taarifa hizi za kiswahili zinakuwa na header paper za kiingereza? Kurugenzi ya Ikulu vipi?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...