Sasa wakisema tunapiga kura hapa pame kaa vipi, ndivyo anavyoonekana kusema, Brigedia General Charles Muzanizanila kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ ) akiwa katika majadiliano na Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Justin Seruhere. Dkt. Seruhere na Brigedia General Muzanizanila wanaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa mwezi mmoja wa nchi Wajumbe wa majadiliano kuhusu Mkataba wa Biashara ya Silaha ( ATT). viongozi hawa wawili kama ilivyokuwa kwa wajumbe wengine, walijikuta wakitafakari hatima ya maendeleo ya mkutano huu, baada ya kutokea mkwamo uliosababishwa na nchi ya Misri kuamua kuwasilisha hoja siku ya kwanza ya kuanza kwa mktano huo ( jumatatu) hoja ya kutaka Ujumbe wa Palestina uruhusiwe kushirika mkutano huo kama nchi kamili na si mtizamaji (observa)
Wajumbe wa mkutano wa majadiliano kuhusu mkataba wa biashara ya silaha ( ATT) wakiwa katika mkanganyiko wa kutoa jua nini hasa kilikuwa kikiendelea baada ya kuahirishwa kuanza kwa majadiliano kutona na mvutano mkali wa kidiplomasia uliosababishwa na hoja iliyowasilishwa na Misri kutaka Palestina ishiriki kama nchi kamili. Palestina ilishikilia msimamo huo kiasi cha kuufanya mkutano huo kushindwa kuanza kwa wakati. lakini hatimaye suluhu ilipatikana na Palestina ikaruhusiwa kushiriki kwa asili mia kwa mia.

Na Mwandishi Maalum

Licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kuufungua rasmi mkutano wa nchi wajumbe wa majadiliano kuhusu kuanzishwa kwa mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Silaha Duniani ( ATT). Majadiliano rasmi ya mkataba huo yalikwama kuanza kwa siku mbili baada ya kutolewa hoja ya kutaka Palestina ishiriki katika mkutano huo kama nchi na si muangalizi ( Observa).

Hoja hiyo ambayo iliamusha malumbano na mabishamo kati ya Palestina na nchi za Magharibi iliwasilishwa siku ya jumatatu na nchi ya Misri.

Mkutano huo muhimu sana kwa mustakabari wa biashara ya silaha na kwa usalama wa maisha ya watu, ulitakiwa kuanza rasmi siku ya jumatatu lakini hali haikuwa hivyo baada ya Misri kuwasilisha hoja hiyo.

Baada ya kushindikana kuanza siku ya jumatatu, mkutano uliahirishwa hadi siku ya jummane, hata hivyo mkutano ukashindwa kuanza kwa muda uliopangwa kutokana na kutofikiwa kwa muafaka wa hoja ya kutaka Palestina ishiriki kama nchi kamili.

Hatimaye mkutano ulianza kwa Ban Ki Moon kutoa hotuba yake ambayo aliwasihi wajumbe wa mkutano huo kumaliza tofauti zao kidiplomasia ili mkutano huo muhimu uweze kuanza.

Hata hviyo baada ya Ban Ki Moon kutoa hotuba yake na kuondoka, hali iliendelea kuwa ya sintofahamu kutokana na pande zinazohusika kuendelea kuvutana na kutofikia muafaka wowote.

Taratibu na sheria za mkutano huu wa kimataifa unaojadili maadalizi ya mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha zinaeeleza kwamba washiriki wa mkutano huo ni nchi za jumuia ya kimataifa bila ya kujali kwamba nchi hiyo ni Mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Palestina inajulikana kama nchi mtizamaji kutokana na kwamba bado haijatambuliwa au kukubaliwa kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Na kwa sababu hiyo imekuwa ikishirika mikutano ya Umoja wa Mataifa kama nchi mwangalizi na kwa taratibu za umoja wa mataifa nchi mwangalizi haipewi haki stahili za kujadili, kuchangia au kutoa maoni kama ilivyo kwa nchi ambayo ni mwanachama. Na kama ikipata fursa ya kuzungumza basi huzungumza mwisho kabisa baada ya nchi wanachama kuzungumza.

Mvutano huo wa aina yake, ambao hatimaye suluhu ilipatikana kwa waandaaji wa mkutano huo kukubali kuipatia Palestina hadhi ya kushiriki mkutano huo kama mwanachama. Na kuepusha uwezekano wa kuipigia kura hoja hiyo

Kufuatia kumalizika mwa mvutano huo, majadiliano rasmi yalianza siku ya jumanne saa moja usiku.

Hata hivyo uamuzi wa kuiruhusu Palestina kushirikia kwa asilimia mia majadiliano ya mkutano huo, kulizua manung’uniko kutoka nchi ya Holy Sea ( Vatican) ambayo kupitia mjumbe wake ilisema haikutendewa haki kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za mkutano huo ilipashwa nayo kushiriki mkutano ikiwa na haki zote kama nchi mwanachama.

Mjumbe wa Holy Sea alieleza kinagaubaga na huku akinukuu maazimio mbalimbali kwamba sekretarieti ilikuwa inaweka historia mbaya huku ikikiuka maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Holy See ikasema mkutano huu unaojadili maandalizi ya mkataba wa biashara ya silaha, ni mkutano muhimu na nyeti unaogusa maslahi ya kila nchi. Na ni mkataba ambao ukishaandaliwa na kupitishwa utazigusa nchi zote.

Na kwa sababu hiyo akasema mjumbe huyo wa Holy Sea, kwamba ni kutokana na ukweli huo, na kwa kuzingatia kwamba Holy Sea imekuwa ikifuatilia kwa karibu mchakato mzima wa majadiliano ya kuanzishwa kwa mkataba huo, Hivyo basi ilikuwa inastahili kushiriki kwa asilimia mia moja. Na kusisitiza kwamba hoja yake iingizwe kama hoja rasmi katika kumbukumbu za mkutano huo.

Awali akifungua mkutano huo, Ban Ki Moon amesema kwamba ma- milioni ya watu wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na matumizi yasio sahihi ya silaha.

Aidha akabainish kuwa dola za kimarekani Trillion moja hutumika kila mwaka kwaaajili kujilimbikiza silaha za kijeshi.

Kama hiyo haitoshi Ban Ki Moon anasema utafiti uliofanywa kwa nchi za Afrika kati ya mwaka 1990 hadi 2005, nchi 23 za Afrika zilipoteza kiasi dola za kimarekani bilioni 284 kutokana na migogoro ya kivita.

“ Matumizi mabaya na kuto ratibiwa kwa biashara ya silana, kumeongeza mateso kwa raia wasio na hatia ambao wanajikuta kati kati ya mapambano. Tunayaona haya katika mauaji yakiwamo madhara wayapatayo watoto” akasema katibu Mkuu na kuongeza.

Dunia inatuangalia, watu wanatuangalia, wanataka siye tuliokusanyika katika ukumbi huu tuwape matumaini, tuwape matumaini kwamba mwishoni mwa mkutano huu tutatoka na mkataba wa kimataifa kwa kudhibiti biashara ya silaha.

“ Hebu tuutazame ukweli, jukumu lilopo mbele yetu ni kubwa na zito na kuna changamoto kubwa kufikia kile tunachokita. Biashara ya silaha inagusa maslahi ya nchi nyingi”. Akabainisha Ban Ki Moon

“ Nimefurahi sana kwamba ukumbi huu umejaa kupita kiasi, na hili linadhihirisha ni kwa namna gani tunalipa uzito suala hili, tunajukumu nzito, lazima tufike mahali tukubaliane kuto kukubaliana, tuweke kando tofauti zetu, mwisho wa mkutano tutoke na mkataba, mkataba utakaowapa watu matumaini” akasihi Ban Ki Moon.

Hata hiyo duru za kidiplomasia zinatahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba mkutano huu ambao ni wa mwezi mmoja unaweza usitoke na jambo lolote la maana achilia mbali mkataba.

Na hii inatokana na misimamo mbalimbali ya kimaslahi inayooneshwa na mataifa achilia mbali yale yaliyoendelea bali hata yale yanayoendelea na kubwa sana ikiwa ni kulinda maslahi yatokanayo na biashara hiyo.

Mchakato wa majadiliano kuhusu kuanzishwa kwa mkataba wa biashara ya silaha duniani yalianza miaka sita iliyopita baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio lilokuwa likiagiza pamoja na mambo mengine kuanzishwa kwa majadiliano ya kuwapo kwa mkataba huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 04, 2012

    Huyo jamaa hapo anaongea kwa sirisiri anaongea shushushu wa Israel. Anapeleka habari.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...