Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imesema
imejipanga kuhakikisha kuwa majadiliano ya ushirikiano kwa manufaa ya wote
(Smart Partnership Dialogue) yanafanikiwa, yanakuwa endelevu na
manufaa kwa nchi kwa muda mrefu ujao.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipokua akiongea na waandishi wa
habari kuhusiana na matayarisho ya mikutano ya kitaifa na ule wa kimataifa
kuhusiana na majadiliano hayo hapa nchini.
“Tunafanya mambo
mengi kuhakikisha majadiliano haya yanafanikiwa,” alisema balozi Sefue jijini
Dar es Salaam hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maandalizi ya mikutano hiyo miwili muhimu.
Alisema serikali
inashirikiana kwa karibu sana na nchi zote ambazo zimewahi kuwa mwenyeji wa
majadiliano haya kupata uzoefu wao na kuyazingatia katika maandalizi hayo
pamoja na kuwa mahusiano ya karibu na Sekretarieti ambayo iko mjini London.
“Tunashirikiana na
wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika eneo ambalo Mhe. Rais
amelichagua kuwa mada kuu ya majadiliano haya ambalo ni namna ya kutumia
teknolojia kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema.
Alifafanua kwamba
kama nchi, Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa majadiliano haya yanafanikiwa
na yanakua ya manufaa.
Haya ni
majadiliano yanayolenga kutoa fursa kwa jamii kukaa pamoja na kuzungumzia
maswala mbalimbali ya maendeleo.
Kwa hapa Tanzania,
chombo kitakachosimamia na kuratibu majadiliano haya kitaifa ni Baraza la Taifa
la Biashara (TNBC) wakati Wizara ya Mambo ya Nje ina jukumu la kuratibu mkutano
wa kimataifa kuhusu majadiliano hayo hapa nchini mwezi Mei, 2013.
Mchakato wa
majadiliano haya ulishazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete tangu Mei, 2012.
Akizungumzia
jukumu hilo la TNBC, Balozi Sefue ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya
utendaji ya baraza hilo alisema chombo hicho kina uzoefu wa kukutanisha makundi
mbalimbali, kujadiliana kwa uwazi na kukubaliana jinsi ya kuendesha mambo
katika nchi kwa faida ya serikali na wafanyabiashara.
“Katika utaratibu huu
wa majadiliano kwa manufaa ya wote tunahusisha makundi mengi zaidi na hivyo
baraza litatumia uzoefu wake kuratibu majadiliano hayo kitaifa,” alisema.
Majadiliano ya
kimataifa yanasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje.
Mkutano wa mwezi
Mei, 2013 ni mwendelezo wa mikutano kama hii ambayo imeanza kiasi cha miaka
kumi na tano iliyopita na ikianzishwa na Jumuia ya Madola kupitia taasisi yake
inayoitwa Commonwealth Partnership for Technology Management na kwa ushiriki
mkubwa wa aliyekuwa waziri Mkuu wa Malaysia, Dkt. Mahathir Mohamad.
Tayari TNBC
imeshaanza kuendesha semina za uhamasishaji zenye lengo la kutoa ufahamu kuhusu
majadliliano ya kitaifa kabla ya yale ya kimataifa.
Kitaifa,
majadiliano haya yatahusisha makundi mbalimbali yakihusisha serikali,
wanasiasa, wafanyabiashara, wasomi,wafanyakazi, vijana, wasanii na wakulima
ambao watakaa pamoja na kujadili maswala mbalimbali yanayohusu biashara na
maendeleo.
Makundi haya yatapata
fursa hiyo kupitia mabaraza ya mikoa na yale ya wilaya ya TNBC ambako
madajiliano hayo yatafanyika kuanzia huko hadi ngazi za kitaifa kabla ya
majadiliano ya kimataifa mwezi Mei.
Makundi yote yatapata fursa ya kujadili na kutoa
mapendekezo yao.
majadiliano ya wana-Mtwara na serikali kuu DSM kuhusu gesi kuchochea viwanda mkoani Lindi na Mtwara lini?
ReplyDeleteMajadiliano ya serikali na wananchi wa sehemu zenye migodi na serikali kuu DSM lini?
Mdau
Mikindani