*Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000
* Wapelekwa Masasi chini ya ulinzi wakajibu tuhuma zinazowakabili

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.

Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana jioni (Jumamosi, Januari 7, 2017) baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO – Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.

Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa an wanunuzi wa mnda wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.

“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.

Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuhoji Kaimu Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika Masasi Mtwara (MAMCU) Bwana Kelvin Rajabu kuhusiana na upotevu wa koroshozaidi ya tani 2000 Waziri mkuu alifanya kikao na Bodi ya korosho pamoja na baadhi ya wanaushirika Mamcu kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano Ikulu ndogo Mkoani Ruvuma
Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Zuberi Mwombeji akiwatarifu Maofisa wa Mamcu na Yurap wako chini ya ulinzi wa polisi kuhusiana na upotevu wa korosho tani 2000 kulia mwenye kaunda suti Kaimu meneja mamcu Bwana Kelvin Rajabu anayefuatia Mkurugenzi wa YURAP inayojishughulisha nauhifadhi korosho katika Ghala la BUCO Masasi Bwana Yusuf Namkula anayefuatia Mkurugenzi mwenzake Bwana Ramadhan Nama na Meneja tawi la Mamcu Bwana Lawrence Njozi
Watuhumiwa wakipelekwa kupanda gari la polisi kwa ajili yakuwapeleka rumande
Kaimu Meneja wa Mamcu bwana Kelvin Rajabu akipanda gari la polisi tayari kwakwenda rumande.Picha na Chris Mfinanga .


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...