Na Wankyo Gati, ARUSHA 
 UPANDE wa Jamuhuri umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi  ya jijini Arusha kuiondoa kesi ya kujifanya Afisa usalama wa Taifa  na kujipatia chakula  katika hotel moja ya kimataifa jijini Arusha inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa huo  Bw.
Lengai ole Sabaya. 
Akitoa ombi hilo Wakili wa Serikali Bi. Grace Madikenya mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha, Mhe. Gwantwa Mwakuga, alisema upande wa Jamhuri hauna nia ya kuendelea na kesi hiyo sababu shahidi mmoja muhimu yupo nje ya nchi kwa miezi 18. 
 “Sasa tumeona tutamtesa mteja wetu. Hivyo kwa nia njema kabisa tumeamua kuiondoa mahakamani kesi hii, maana miezi hii 18 ni  mwaka mmoja na miezi sita,”alisema. 
 Ombi hilo lilipingwa vikali na Wakili wa utetezi, Bi. Edna Haraka na kuiomba mahakama hiyo iendelee na kesi hiyo, kwa madai kuwa upande wa mwendesha mashitaka unatumia Mahakama kama kichaka cha kumnyima haki mteja wao na kumnyanyasa. 
Alisema upande huo hauna nia njema na mshitakiwa na kwamba kitendo cha kuiondoa kesi hiyo mahakamani sio mara ya kwanza ni mara ya pili, ambapo ya kwanza waliomba hivyo na mahakama ilipofuta walimkamata mteja wao na kumnyima dhamana. 
“Sasa leo tupo katika kusikiliza shahidi wa tatu na badala ya kuleta shahidi walileta maelezo ya shahidi na leo wanakuja na stori ya kuiondoa ili waendelee kumyanyasa mteja wetu. Hapana! Ofisi hiyo ya Mwanasheria Mkuu inatumika vibaya kwa kivuli cha Mahakama,”alisema Edna
Wakili huyo alisema serikali ya sasa inasisitiza mpango wa kuharakisha mashauri kusikiliza wa BRN, sasa wakati inafanyika hivyo wengine wanachelewesha kwa sababu zao. 
Hakimu Gwantwa Mwakuga baada ya kusikiliza pande zote mbili, alisema atatoa uamuzi Aprili 28 mwaka huu, ya  kama anakubali shauri liondolewe au la. Bw.  Lengai anakabiliwa na shitaka la kujifanya Afisa Usalama wa Taifa na kujipatia huduma ya chakula na malazi kwenye Hotel ya kimataifa ya Highway ya jijini Arusha.
Kutoka maktaba: Aliyekuwa Mwenyekiti  wa UVCCM mkoa wa Arusha Bw. Lengai Ole Sabaya (katikati) na wakili wake na wakitoka mahakamani siku za nyuma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...