Daktari bingwa wa meno kutoka Chuo kikuu cha AJMANI cha Falme za kiaarabu,  Zaid Mohammed Hassan akimfanyia uchunguzi wa meno mwanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe H Juma Hassan katika zoezi la kutoa matibabu yaliofanyika skulini hapo.

Na Kijakazi Abdalla-MAELEZO
JAMII imetakiwa itumie mbinu sahihi ili kuimarisha afya kinywa na meno na kupunguza mzigo mkubwa wa kutibu maradhi ya meno.  

Akizungumza katika kampeni maalum juu ya kujikinga na maradhi yanayoathiri kinywa na meno katika skuli ya msingi Mwanakwerekwe ‘E’, Daktari Dhamana Kanda ya Unguja Muhidin Abdalla Mohammed, amesema wananchi wengi wamebainika kuathiriwa na maradhi ya kinywa na meno.

Kwa hivyo amesema ipo haja ya kuchukua tahadhari ili kupunguza tatizo hilo. Aidha, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuinua uwelewa wa watu ambao hawatoi kipaumbele kwa afya ya kinywa na meno, na hivyo kujikuta wakisumbuka kuhahangaikia matibabu.

 Dkt. Muhidini Abdalla wa meno kanda ya Unguja  akiwapatia elimu fupi wanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe E namna ya kusafisha meno.

Dk. Muhiddin pia amesema hatua ya kufanya kampeni hiyo katika skuli, inalenga kuwapa elimu wanafunzi juu ya namna bora na sahihi za kutunza meno na kupiga mswaki ili waimarishe afya ya meno yao.

Alisema katika umri mdogo, ndipo watoto hupitia mabadiliko makubwa kimwili, hivyo kuwapa taaluma kutawawezesha kufahamu mbinu sahihi za kuimarisha afya na kujikinga wanapokua wakubwa.

Hata hivyo, ameiomba Serikali iongeze juhudi zaidi kufikisha huduma za meno kila eneo ingawa kunahitaji gharama kubwa, lakini akasema kuacha watu waugue bila tiba ni gharama zaidi.

Alieleza kuwa, tangu kuanza kampeni hizo kuelekea maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno kimataifa, zaidi ya watoto 1,000 wametibiwa kwa kushirikiana na madaktari kutoka Ujerumani, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na Wizara ya Afya.

 Daktari dhamana wa Meno kanda ya Unguja alievalia vazi jeupe Muhidini Abdalla akishirikiana na madaktari bingwa kutoka Ujerumani na Falme za Kiarabu wakimng’oa jino mwanafunzi Aisha Makame wa skuli ya Mwanakwerekwe H katika matibabu yaliofanyika skulini hapo.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Mwanakwerekwe ‘E’ Khitiyar Haidhuru Ramadhani,  alisema ujio wa madaktari hao umewapa faraja  wanafunzi na elimu sahihi ya kutunza meno yao.

Aidha aliwataka wazee kujenga utamaduni wa kuwanunulia watoto vitu vinavyoweza kuwaepusha na maradhi ya meno kama vile pipi, biskuti na chokoleti ambavyo huchangia zaidi maradhi hayo.

BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...