Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Serikali imesema kuwa hakuna akiba ya fedha iliyowekwa katika mfuko maalum kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa kwa sababu deni hilo linajumlisha Deni la Serikali na Deni la Sekta Binafsi, lakini Serikali inalipa deni lake pekee bila kuhusisha deni la Sekta Binafsi.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa Akijibu maswali ya Mbunge wa Mtambile Mhe. Masoud Abdallah Salim aliyetaka kujua Deni la Taifa limefikia kiasi gani na namna mchanganuo wa fedha zilizowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni hilo ulivyo.

“Fedha kwa ajili ya malipo ya Deni la Serikali inatengwa kwa kuzingatia taratibu za kawaida za kibajeti kupitia Fungu 22, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Serikali ilitenga kiasi cha Sh. trilioni 1.262 kwa ajili ya malipo ya deni la ndani na Sh. bilioni 685.06 kwa deni la nje”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisema hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu Deni la Taifa limefikia Dola za Marekani milioni 26,161.02 sawa na zaidi ya Shilingi trilioni 59.4

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha Deni la Taifa linahakikiwa ili kujua kama Serikali inakopesheka au la, Dkt. Kijaji alilihakikishia Bunge kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Deni la Taifa litahakikiwa kama nchi nyingine zinavyofanya kwani mkataba wa kuhakiki deni hilo upo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hatua za mwisho.

Waziri huyo alisema kuwa Deni la Taifa ni himilivu na Serikali imekuwa makini katika ulipaji kwa kuhakikisha inalipa kila mwezi madeni katika Taasisi zote ilizokopa hali inayoifanya nchi kuaminika na Taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa

Aidha, Mhe. Kijaji alifafanua kuwa fedha zote zinazokopwa zinapelekwa katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi ili kuendelea kuinua uchumi wa nchi hususani katika kipindi hiki cha uchumi wa viwanda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...