Na Emmanuel Masaka,Globu ya jamii 

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ametangaza vita na watu wenye tabia za kuwachukuwa watoto yatima,walemavu na waishio katika Maisha magumu kama mitaji ya kujinufaisha watakamatwa na kuchukuliwa hatua Kali za kisheria.

Makonda ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya matokeo ya utafiti wa idadi ya Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kinyume na Sheria hali inayosababisha kushindwa kutumia fursa ya elimu bure iliyotolewa na Rais John Magufuli jambo ambalo Makonda ameapa kulivalia njuga.

Kwa mujibu wa utafiti huo umebaini Mkoa wa Dar es salaam pekee una jumla ya watoto 3,312 wanafanya kazi mitaani na kati ya hao watoto 2,984 walionekana wakifanya kazi nyakati za mchana na 328 wanafanya kazi nyakati za usiku.

"Idadi hiyo ya watoto wanaoishi mitaani ni matokeo ya kukosekana kwa misingi bora ya familia na mmonyoko wa maadili ndio maana niliamua kuunda tume ya kupitia sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa ambayo itasaidia kuweka haki stahiki za watoto,"amefafanua. 

Aidha amewaonya watu wenye tabia ya kuwapatia ombaomba fedha barabarani kuwa ndio wanaohalalisha uwepo wa watu hao ambapo amesema kama mtu anataka kweli kusaidia waishio maisha magumu wapeleke misaada kwenye vituo vilivyopo kwa mujibu wa sheria kwani vituo hivyo vinafuatilia mienendo ya watoto kitabia, elimu na matibabu.

Ambapo ukimpa fedha mtoto barabarani unatengeneza mazingira ya kuwa na fedha ambayo hana uhalali nayo na anapokuwa mtu mzima anakuwa mkabaji,mporaji na kuchoma visu watu wasio na hatia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Babawatoto Center Bwana Mgunga Mwa Mnyenyelwa amempongeza Makonda kwa kutafuta haki ya mtoto alietelekezwa kwani kupitia mchakato huo limewezesha watoto wengi kuingia kwenye mfumo rasmi wa kupata fedha ya matunzo kila mwezi pamoja na bima ya matibabu Bure.

Amesema utafiti huo umefanywa na shirika la Babawatoto Center for Children and Youth.kupitia mradi wa USAID Kizazi Kipya kwenye mikoa mitano ambapo wamebaini nusu ya watoto wa mitaani wanapatikana mkoa wa Dar es salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wanaowatumia watoto yatima,walemavu waishio,mazingira magumu kama mitaji ya kujinufaisha,ameeleza kuwa watu hao wakibainika watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.(Picha na Emmanuel Massaka Globu ya jamii)
Mkurugenzi wa Shirika la Babawatoto Sente,Mgunga Mwa Mnyenyelwa akimkabidhi ripoti ya matokeo ya utafiti wa idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kinyume cha sheria,Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda.
Picha ya pamoja

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...