Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeyatupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na viongozi tisa wa CHADEMA akiwemo mwenyekiti wake Freeman mbowe, baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na upande wa jamhuri.
Uamuzi huo umetolewa leo Julai 20 na 
 Jaji Rehema Sameji  wa Mahakama Kuu baada ya kusikiliza pingamizi hilo la upande wa jamhuri kupinga maombi hayo kwa madai ni batili na kuomba yatupiliwe mbali.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Rehema  amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa kuwa haijaelekezwa ipasavyo.

Amesema mahakama imekubaliana na a pingamizi la awali la kudai kuwa, maombi hayo yamewasilishwa kwa kutumia kifungu cha sheria ambacho siyo sahihi na kuwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo na kuyatupilia mbali.

Jaji Rehema amesema pamoja na pingamizi hilo la upande wa mashtaka, hata kifungu walichotumia upande wa utetezi kupeleka maombi hayo hakipo kisheria kwa sababu kilifanyiwa marekebisho.

 Mapema, upande wa utetezi kupitia wakili wao Peter Kibatala aliwasilisha maombi kupinga uamuzi kuhusu mwenendo wa shauri lao na kuomba marejeo.

Hata hivyo, upande wa jamhuri uliomba mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo kwa kuwa amri ndogo ambazo hazimalizi kesi huwezi kuombea marejeo na yamewasilishwa chini ya kifungu ambacho si sahihi cha kifungu cha 372 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)  kitu ambacho hakipo kabisa.

Mbali na Mbowe, washitakiwa  wengine ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Washitakiwa wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee,   Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime mjini, Matiko.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 12, ambapo wanadaiwa kuwa  walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu katika maeneo ya Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na  barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.

Wanadaiwa kuwa Februari 16,mwaka huu katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washitakiwa hao wakiwa na wenzao 13 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...