"MAHAKAMA"
Showing posts with label MAHAKAMA. Show all posts
Na Karama Kenyunko - Michuzi tv

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeelezwa kuwa Mwenyekiti CHADEMA, Tundu Lissu, hakuwa na ufahamu wa uwepo wa waandishi wa habari katika mkutano wa chama hicho na watia nia uliofanyika Aprili 3, 2025.

Shahidi wa nne wa utetezi, Brenda Rupia, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, amedai hayo leo Septemba 7, 2026 mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na jaji Fednand Kiwonde na James Karayemaha alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.

Brenda amedai kuwa, Lissu hakuwa ameandaa mkutano huo wala aliyealika vyombo vya habari, akieleza kuwa jukumu hilo lilifanywa na Sekretarieti ya CHADEMA chini ya Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Amesema yeye ndiye aliyeandika taarifa kwa umma na watia nia kuhusu mkutano huo Machi 27, 2025, na kuiweka katika kurasa za chama kwenye mitandao ya kijamii, huku waandishi wa habari wakialikwa kufanya coverage ya mkutano huo.

Kwa mujibu wa Brenda, takribani watu 250 walihudhuria mkutano huo, wakiwemo watia nia, wajumbe wa Sekretarieti, viongozi wakuu wa CHADEMA pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, akiwemo Jambo TV.

Brenda amedai Lissu alikuwa mzungumzaji mkuu katika mkutano huo na alitoa hotuba kuhusu msimamo wa chama wa “No Reforms, No Election”, huku akisisitiza kuwa hakumuona akifanya jukumu lingine lolote katika mkutano huo.

Kuhusu maudhui yaliyorushwa na Jambo TV, shahidi huyo amesema yaliyorekodiwa na chombo hicho yalikuwa mali ya Jambo TV na kwamba Lissu hakuwa mfanyakazi wa chombo hicho wala hakuhusika na kurusha matangazo hayo.

Baada ya ushahidi huo, Mahakama iliahirisha kesi hadi kesho saa tatu asubuhi huku Jaji Dustan Ndunguru akieleza kuwa kesi hiyo imeongezewa siku 14 kuanzia leo kwa ajili ya kukamilisha mwenendo wake.


Na Janeth Raphael - MichuziTv

Upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wake baada ya kuwasilisha ushahidi wa mashahidi 17 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Hatua hiyo imefikiwa leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo, Dar es Salaam, wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza Mahakama kuwa baada ya upande wa Jamhuri kupitia kwa kina ushahidi uliotolewa na mashahidi wake pamoja na hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa usikilizwaji wa kesi, umefikia uamuzi kuwa ushahidi uliopo unatosheleza.

Kwa mujibu wa Katuga, uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani umeifanya Jamhuri kuona hakuna ulazima wa kuongeza mashahidi wengine, hivyo upande huo umefunga rasmi ushahidi wake.

“Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa hapa mahakamani na kuangalia ushahidi wa mashahidi waliobakia, tumechambua na kuangalia hoja zilizowasilishwa mahakamani hapa. Hata hivyo, upande wa Jamhuri tunaona ushahidi ambao tumeutoa ni ushahidi toshelezi zaidi kuleta mashahidi wengine,” amesema Katuga.

Uamuzi huo unaweka kesi hiyo katika hatua muhimu, baada ya upande wa mashtaka kukamilisha uwasilishaji wa ushahidi wake kupitia mashahidi 17.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kufungwa kwa ushahidi wa Jamhuri kunafungua hatua nyingine ya kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo, huku taratibu za mahakama zikiendelea kuamua hatua zinazofuata.



Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akidai hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuchelewesha usikilizwaji wa kesi ya tuhuma za uhaini inayomkabili.

Lissu alidai hayo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani baada ya Jamhuri kufungua shauri la mapitio kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo.

Alidai uamuzi wa Mahakama Kuu wa Februari 24, 2026 haukumaliza kesi ya msingi ya uhaini, hivyo ni uamuzi mdogo usioruhusiwa kukatiwa rufaa wala kuwasilishwa maombi ya marejeo kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Rufani.

Lissu pia alidai DPP hakupaswa kuwasilisha maombi hayo moja kwa moja Mahakama ya Rufani bali alitakiwa kwanza kuandika barua rasmi kwa Jaji Mkuu.

Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga na Job Mrema waliieleza Mahakama kuwa Lissu ametegemea kanuni za mashauri ya madai badala ya jinai na kwamba maombi ya DPP yamewasilishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya Rufani na Kanuni zake.

Katuga alidai Mahakama Kuu ilikataa ushahidi huo kabla haujapokelewa na kupimwa, jambo ambalo lilinyima Jamhuri haki ya kusikilizwa kikamilifu, huku akisisitiza kuwa Mahakama ilipaswa kuangalia uhalali wa notisi ya kuongeza ushahidi.

Mrema naye alidai pingamizi la awali la Lissu halina uwezo wa kuondoa shauri lote na kwamba halijazingatia sheria ya sasa kwa kuwa linahusu mashauri ya madai.

Katika majibu yake, Lissu aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi hayo na iamuru DPP amlipe fidia kwa kile alichodai ni ucheleweshaji wa makusudi wa shauri lake, akisema amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na miezi mitatu huku kesi ikicheleweshwa kwa siku 139.

Katuga alipinga madai hayo akieleza kuwa maombi hayo hayajalenga kuchelewesha kesi na kwamba Mahakama ya Rufani ina mamlaka ya kuhakikisha mwenendo wa Mahakama Kuu unafuata sheria.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi itakapotoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo pande zote zitajulishwa.






Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava, ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuharakisha uimarishaji na usambazaji wa mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi nchini ili kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Akizungumza bungeni leo wakati akichangia mjadala wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/27, Mnzava amesema kuwa licha ya Serikali kuanza hatua za matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ardhi, bado halmashauri chache pekee ndizo zimefanikiwa kufikiwa na mfumo huo, jambo linalochangia kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema mfumo huo unapaswa kusambazwa katika halmashauri zote nchini ili kurahisisha usimamizi wa taarifa za ardhi, kuongeza uwazi katika umiliki wa maeneo na kusaidia wananchi kupata huduma kwa haraka zaidi.

“Mpaka sasa ni halmashauri chache sana ambazo zimefanikiwa kupata mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi. Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo huu unasambazwa nchi nzima ili kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika sekta hii muhimu,” amwsema Mzava.

Mbunge huyo alikiri kuwa utekelezaji wa mpango huo unahitaji fedha nyingi, lakini akasisitiza kuwa umuhimu wa sekta ya ardhi kwa uchumi wa taifa unapaswa kupewa kipaumbele maalum.

Amesema mapato yanayotokana na kodi na pango la ardhi yanaweza kutumika kusaidia kuendeleza mifumo hiyo ya kisasa, huku akiishauri Serikali kuhakikisha sehemu ya fedha zinazokusanywa na Wizara ya Ardhi zinabaki wizara hiyo ili kusaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato zaidi.

“Kazi ya kusambaza mfumo huu nchi nzima siyo ndogo, ninafahamu kutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Lakini kutokana na umuhimu wa sekta ya ardhi, naiomba Serikali mapato yanayotokana na kodi na pango la ardhi yarudishwe kwa kiwango kikubwa zaidi wizara husika ili waweze kuendelea kutengeneza mifumo na kuboresha ukusanyaji wa mapato,” amesisitiza.

Mnzava ameeleza kuwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea, sekta ya ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali zinazotokana na umiliki na matumizi ya ardhi, hivyo Tanzania nayo inaweza kunufaika zaidi iwapo itawekeza vya kutosha katika mifumo ya kisasa ya usimamizi wa ardhi.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa juhudi zake za kuongeza makusanyo ya mapato na kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi, huku akiitaka Serikali kuendelea kuiwezesha wizara hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

“Tunaona kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Ardhi katika kuongeza makusanyo ya Serikali. Sasa ni wakati wa Serikali kuendelea kupeleka fedha zaidi kwa wizara hiyo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuendelea kulitumikia taifa,” alisema.

Kauli ya mbunge huyo imekuja wakati ambapo Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa ardhi na upangaji wa matumizi bora ya maeneo nchini.


Na Karama Kenyunko - Michuzi Tv

Wafanyabiashara watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni wakikabiliwa na tuhuma za makosa ya Uhujumu Uchumi, wakidaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh milioni 120.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutekeleza makosa hayo katika mipaka ya Sirari mkoani Mara, Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, kwa lengo la kujipatia vibali vya muda vya matumizi ya magari yaliyokuwa yamesajiliwa kwa namba za Afrika Kusini.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani na Wakili wa Serikali, Godfrey Nugu akisaidiana na Rozalia Rutagwerela, washtakiwa hao wametajwa kuwa ni George Kaiza (35), Hosiana Sanga (31) na Hamu Sanga (26).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila, upande wa mashtaka ulidai kuwa katika kesi namba 11588/2026 inayomkabili George Kaiza pekee, mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka saba.

Inadaiwa kuwa Machi 27, 2026 katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa forodha wa TRA ili kuingiza nchini gari aina ya Toyota Fortuner lenye namba za usajili za Afrika Kusini kwa lengo la kupata kibali cha muda.

Aidha, Februari 25, 2026 katika mpaka wa Sirari mkoani Mara, Kaiza anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa TRA wakati akiingiza nchini gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili za Afrika Kusini kwa lengo la kujipatia kibali cha muda kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa mashtaka ulidai pia kuwa Kaiza aliuza magari hayo kinyume cha sheria huku akijua kuwa yalikuwa yamepewa vibali vya muda na TRA.

Wakili Nugu alidai kuwa Machi 27, 2026 katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza alikwepa kwa makusudi kulipa ushuru wa zaidi ya Sh milioni 84 kwa magari mawili ambayo ni Toyota Fortuner na Ford Ranger yaliyokuwa na namba za usajili za Afrika Kusini, jambo ambalo alifahamu kuwa ni kinyume na sheria.

Hata hivyo, Kaiza hakutakiwa kujibu chochote mahakamani kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu Uchumi. Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kwa upande wa washtakiwa Hosiana na Hamu, wanadaiwa kuwa Januari 25, 2026 katika eneo la Tunduma mkoani Songwe walitoa taarifa za uongo ili kujipatia kibali cha muda na kuingiza nchini gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili za Afrika Kusini.

Inadaiwa kuwa kwa kufanya hivyo, waliisababishia TRA hasara ya Sh milioni 35.5 kutokana na kukwepa kulipa ushuru wa uingizaji wa gari hilo huku wakijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Licha ya dhamana kuwa wazi, hadi wakati Michuzi Blog inaondoka mahakamani, washtakiwa wote walikuwa bado wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili, kuweka fedha taslimu sawa na nusu ya kiasi cha hasara kinachodaiwa kusababishwa au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9, 2026 kwa ajili ya kutajwa.


NA Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imewafikisha Mahakamani  waliokuwa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na watendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), wakikabiliwa na mashtaka ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kwa kujipatia zaidi ya Sh3.5 bilioni kwa njia za udanganyifu.

Hayo yamesemwa  na Wakili wa serikali mwandamizi Godviver Killian leo  tarehe 25 may 2026  baada ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani na  kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya hakimu mkazi Jijini Dodoma  TEMESA wakikabiliwa na mashtaka 9 huku CWT  Mastaka 14.

Dodoma: Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma waliokuwa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) pamoja na watendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), wakituhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu,  uhujumu uchumi, utakatishaji fedha kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh3.5 bilioni

Kwa upande wa CWT, waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa Rais wa chama hicho Leah Ulaya, Makamu wa Rais Suleimani Ikomba, aliyekuwa Katibu Mkuu Maganga Japhet, pamoja na Joseph Misalaba, Nashon Kidudu, Baraka Mbonalibha, Wambura Kihengu, Angelina Wambura na Kampuni ya Pyrate and Industries Company Limited.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 14 ya uhujumu uchumi, ikiwemo kujipatia zaidi ya Sh2.2 bilioni kinyume cha sheria kati ya mwaka 2023 na 2024.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Patrick Mwita amesema washtakiwa hao waliidhinisha matumizi ya fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa tisheti na kofia kinyume na Katiba ya CWT.

Mwita amedai kuwa washtakiwa hao pia walijipatia Sh1.3 bilioni kutoka Kampuni ya Pyrate and Industries Company Limited ili kupitisha zabuni ya ununuzi wa tisheti na kofia hizo kinyume cha taratibu za chama.

Aidha, amewataja wakurugenzi wa kampuni hiyo, Wambura Kihengu na Angelina Wambura, kuwa wanakabiliwa na shtaka la kughushi nyaraka mbalimbali ili kuonyesha kampuni hiyo ilikuwa halali, huku wakifahamu kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria.

"Watuhumiwa wengine watatu ambao ni Selemani Ikomba, Baraka Mbonalibha na Angelina Wambura bado wanaendelea kutafutwa ili waunganishwe na wenzao kwenye kesi hii,” alisema Mwita.

Kwa upande wa TEMESA, waliofikishwa mahakamani ni Lazaro Kilahala, Mathias Rutaguza, Sambayeti Magoko, Kennedy Manene, Peter Bongole, Clavery Busunzu, Mbisho Kibuti, Renatha Juma, Vincent Lutembuka, Michael Assey, Caesar Chambo, Nassor Igangule, Deus Matiku pamoja na Kampuni ya Kentra Tanzania Limited.

Washtakiwa hao wanashtakiwa kwa makosa tisa ikiwemo kughushi nyaraka za ununuzi wa vipuri vya magari na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh1.3 bilioni.

Mwita amesema watuhumiwa wawili, Mathias Rutaguza na Michael Assey, bado wanatafutwa ili waunganishwe katika kesi hiyo.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mkuu Zabibu Mpangule amewaeleza washtakiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha hadi ipokee kibali maalum kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali (DPP).






MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imewahukumu raia wa China XU Fuyu (39) na mfanyakazi wake wa mgahawa wa Kibonge, Blandina Mwalutola (24) wamehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni  sita kwa kushindwa kutoa risiti ya kielektroniki, baada ya kutoa huduma ya chipsi kuku, sahani ya baga, sahani ya wali na vinywaji.

Washtakiwa hao walishtakiwa Kinyume na Kifungu cha 97(1)(b) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi [Sura ya 438 Toleo la 2023], kikisomwa pamoja na Vifungu vya 96 na 97 vya Sheria ya Fedha Na. 6 ya mwaka 2024.

Pia imedaiwa walikamatwa, wakati maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiwa katika utafiti na upelelezi kuhusiana na utoaji wa risiti za kielektroniki. Ambapo imedaiwa waliagiza chakula na vinywaji ila walipewa risiti za mkono.

Hukumu hiyo, imetolewa leo Mei 8, 2026 na Hakimu Mwandamizi Mohamed Burhani, baada ya washtakiwa kukiri mashtaka mawili kushindwa kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria za kodi.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Burhani amesema kesi kama hizo lazima adhabu zitolewe ili kuzuia makosa hayo yasitendwe na watu wengine. 

"Kwa mujibu wa sheria sitawapa adhabu ya Magereza nitawaacha huru kwa sababu mmekiri mashtaka yenu, shtaka la kwanza kila mmoja atalipa faini ya Sh milioni mbili na shtaka la pili ambalo linamkabili Fuyu peke yake atalipa Sh milioni mbili." amesema Hakimu Burhani 

Hata hivyo, Hakimu Burhani amewaeleza washtakiwa kuwa wakishindwa kulipa faini hiyo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani. 

Hata hivyo washtakiwa waliweza kulipa faini hiyo na kuachiwa huru.

Mapema akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Salome Assey amedai kuwa Machi 24, 2026 katika Mtaa wa Gerezani, eneo la Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa walitoa huduma za chakula na vinywaji katika Kampuni ya Dicos (Mgahawa wa Kibonge) na kushindwa kutoa risiti ya kielektroniki walipotoa huduma ya chakula ambayo ni sahani moja ya baga yenye thamani ya Sh.13,000.

Katika shtaka la pili, inadaiwa kuwa tarehe hiyo na mahali hapo mshtakiwa Fuyu alishindwa kutoa risiti ya kielektroniki alipotoa huduma ya chakula na vinywaji ambayo ni sahani mbili za chipsi kuku, sahani moja ya wali uliochanganywa na mayai, chupa mbili za plastiki za Coca-Cola na chupa moja ya maji ya kunywa ya Kilimanjaro, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi 35,000.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, walikiri kutenda makosa hayo ambayo Hakimu Burhani aliutaka upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali (PH).

Alidai kuwa Machi 24,2026 Fuyu akiwa Meneja wa Kampuni hiyo na Mwalutola akiwa mhudumu walikuwa wanatoa huduma ya chakula na vinywaji kwa wateja na tarehe maofisa wa TRA walipewa kazi kwa ajili ya kufanya utafiti na upelelezi katika mgawaha huo kama wanatoa risiti za kielektroniki.

Ilidaiwa kuwa Ofisa wa TRA, Cecilia Lussa aliagiza sahani ya baga ambayo ilikuwa ni Sh. 13,000 na baada ya kulipa fedha alipewa risiti ya mkono, alipouliza kwa nini hajapewa risiti ya kielektroniki aliambiwa mashine haifanyi kazi ni mbovu.

"Na maofisa wengine wawili Hosea Kasiba na Kisabo Focus walifika katika mgawaha huo, wakaagiza sahani mbili za chipsi kuku, sahani moja ya wali iliyochanganywa na mayai, chupa mbili za Coca-Cola na maji ya Kilimanjaro chupa mbili jumla ilikuwa Sh 35,000, baada ya kulipa walipewa risiti ya mkono, walipouliza walielezwa kuwa mashine ni mbovu,"alidai 

Baada ya hapo walijitangaza kama wao ni maofisa wa TRA, watuhumiwa walikwenda kuripoti Idara ya Kodi kwa kosa la kushindwa kutoa risiti za kielektroniki , ambapo walikiri kutenda kosa hilo.

Hata hivyo, washtakiwa walikili maelezo hayo kuwa ni ya kweli, Mahakama ilipokea vielelezo mbalimbali vya Jamhuri ikiwemo risiti walizozitoa kwa wateja kama kielelezo namba moja.

"Baada ya kusomewa mashtaka yenu mmekiri kosa hilo na PH pia mmekiri kutokana na kukiri kwenu Mahakama inawatia hatiani kwa makosa yote. Je! Jamhuri washtakiwa wanamakosa ya nyuma?,"alisema Hakimu Burhani 

Hata hivyo, Wakili Assey alidai hawana taarifa za nyuma za washtakiwa, kwa hiyo hakimu aliwapa nafasi ya washtakiwa kujitetea kabla adhabu haijatolewa.

Fuyu ambaye ni Meneja Kampuni ya Decos Catering Ltd na Mkazi wa GSM Plaza -Gerezani amedai kuwa yeye ni bosi na pia ni mpishi kwa wakati mmoja, kwa hiyo hawezi kuona kinachoendelea kama risiti za kielektroniki zinatolewa au, ila anakubali kutenda kosa hilo.

Mshtakiwa wa pili,  Mwalutola ambaye ni Mkazi wa Temeke Mwembe Yanga alidai kuwa siku hiyo kweli mashine ilikuwa inasumbua ilikuwa ikiandika 'Illegal', lakini ilipotengemaa waliendelea kutoa risiti za kielektroniki kwa sababu ndiyo utaratibu wao ni siku hiyo tu ndiyo kulitokea changamoto. 

Wakati kesi hiyo inaendelea, Mkalimani Maria Katambo alikuwa akitafsiri kutoka lugha ya kiswahili kwenda Kichina na kichina kwenda Kiswahili kwa ajili ya mshtakiwa Fuyu.

MAHAKAMA Kuu Masijala Ndogo Dar es salaam, imetupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ya kuomba kuunganishwa katika kesi ya mgawanyo wa mali iliyofunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake.

Wengine waliofungua kesi hiyo hiyo ni wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Zanzibar Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu (marehemu).

Wajibu maombi katika kesi hiyo namba 8323 ya mwaka 2025  ambao ni Bodi ya Wadhamini ya Chadema upande wa bara na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Uamuzi huo mdogo umetolewa na Jaji Hamidu mwanga ambaye awali alikuwa akikisikikiza shauri hilo na umesomwa leo Aprili 30, 2026  na Naibu Msajili ya Mahakama hiyo, Hussein Mushi.

Awali, kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa mbele ya Jaji Mwanga kama ilivyoelezwa, huku Lissu aliomba kuunganishwa katika kesi hiyo akidai kuwa kwakuwa kesi hiyo inahusu chama na yeye ndiye mwenyekiti wa chama basi anapaswa kuwa sehemu ya kesi hiyo.

Maombi hayo yalisikilizwa na uamuzi ulipaswa kutolewa Machi 25, mwaka huu lakini kutokana na faili kuitwa Mahakama ya Rufaa Dodoma kesi hiyo ilipelekwa mbele hadi leo.

Katika uamuzi huo Mahakama imekataa kumuunganisha Lissu katika kesi hiyo kama mwenyekiti wa Chama lakini kwakuwa ameyapeleka kwa matakwa yake na si kwa nafasi yake hivyo hana maslahi ya moja kwa moja kwani cheo hicho kinaweza kukaliwa na mtu yeyote

Mahakama imeeleza kuwa Lissu anaweza kutokea kwenye kesi hiyo kama shahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi na si kama moja ya wajibu maombi

Akizungumza nje ya Mahakama Wakili wa chadema , Dkt. Rugemeleza Nshala amedai kesi hiyo kwa sasa imehamishiwa kwa Jaji David Ngunyale na inatarajiwa kutajwa Mei 13,2026.

"Kurudi kwa kesi hii kunaenda sambamba na kufuata maagizo ya mahakama ya Rufaa ya kumtaka Jaji huyo kuangalia kama maombi hayo yalipelekwa ndani ya muda au laa.

“Madai yanatakiwa yaletwe ndani ya miaka sita tangu kuanza kwa migogoro katika uamuzi wa leo wa Jaji Mwanga wakili wa upande wa walalamikaji alisema kwa msisitizo kwamba mgogoro ulianza mwaka 2016, hivyo jaji Ngunyale atatusaidia kuangalia ni muda gani kati ya 2016 hadi 2025,” ameeleza Dkt. Nshala.

Akizungumzia kesi ya uhaini dhidi ya Lissu,  Dkt Nshala bado hawajajua itapangwa lini kwa sababu kesi hiyo ipo katika Mahakama ya rufaa ambayo ndo inatarajiwa ipange mara nyingi hupangwa kwa muundo wa vikao, hivyo msajili wa Mahakama ya rufaa ndiyo atajua ipangwe lini,” amedai Dkt Nshala.




SHAHIDI wa tisa katika kesi hiyo, Ofisa wa Jeshi la Polisi ASP Geofrey Lutufye (47), ameieleza Mahakama kuwa vijana wawili waliokamatwa walikiri kushawishika na maneno ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, na kuamua kuunga mkono wito wa kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akishirikiana na Jaji James Karayamaha na Jaji Ferdinand Kiwonde, shahidi huyo alieleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa katika kijiwe cha bajaji eneo la Mrombo, Arusha.

ASP Lutufye alidai kuwa Aprili 3, 2025, akiwa kwenye doria na kikosi chake chenye askari tisa wakitumia gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser, alipokea maelekezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi, ASP Bonny Mgogo, kwenda eneo hilo kufuatilia taarifa za vijana wanaopanga kuzuia uchaguzi.

“Nilipofika eneo la Mrombo nilikuta vijana wakila njama za kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” alidai.

Alisema waliwakamata vijana wawili waliotajwa mahakamani kama P4 na P7 na kuwapeleka Kituo cha Polisi Murieti mkoani Arusha kwa hatua zaidi.

ASP Lutufye alieleza kuwa wakiwa njiani aliwahoji watuhumiwa hao kuhusu tuhuma hizo.

“Niliwauliza kwa nini wanahusika kula njama za kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025. Wote walikiri kuwa wanamuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kutokana na kauli aliyoitoa mtandaoni kwamba atazuia uchaguzi, ataleta uchochezi na atakinukisha,” alidai shahidi huyo.

Mahakamani hapo, alieleza kuwa aliagizwa kuwapeleka watuhumiwa hao katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa na baadaye kuanzisha jalada la uchunguzi lenye namba ARS/D/CID/B/40/2025.

Aidha, alidai kuwa alipokea maelekezo ya kuwahoji zaidi watuhumiwa hao, maelekezo ambayo aliyatekeleza kwa kushirikiana na askari wengine, huku yeye akiandika maelezo yake ya ushahidi Aprili 18, 2025.

Kabla ya kueleza tukio hilo, ASP Lutufye aliitambulisha Mahakama kuhusu taaluma na uzoefu wake, akisema alihitimu mafunzo ya awali ya polisi katika Chuo cha Polisi Moshi Aprili 28, 2003 na kumaliza Novemba mwaka huo. Pia alipata mafunzo ya nyota ya kwanza mwaka 2013 katika chuo hicho, na baadaye mafunzo ya cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Polisi katika Chuo cha Polisi Dar es Salaam (Police Academy), aliyohitimu Novemba 2023.

Alisema ana uzoefu wa miaka 15 katika majukumu ya upelelezi, akianzia Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam kama askari wa kawaida (general duty), kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita na baadaye Mkoa wa Arusha, ambako kwa sasa ni kiongozi wa kikosi cha Anti Robbery.

Shahidi huyo alieleza kuwa majukumu yake ni pamoja na kufanya doria, kukamata watuhumiwa, kufanya upelelezi na kuwafikisha mahakamani.... Kesi inaendela
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAKAZI wawili wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka kwa zamu msichana mwenye umri wa miaka 24.

Pamoja na kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile msichana huyo pia walimpora simu aina ya Samsung na kumwibia fedha zake Sh70,000.

Hata hivyo, katika hukumu ya kesi hiyo namba 10374/2025 iliyotolewa mji mdogo wa Orkesumet na hakimu wa mahakama ya wilaya hiyo Nicodemo washtakiwa watatu kati ya watano hawakuwepo mahakama hapo.

Hakimu Nicodemo amewataja washtakiwa Meshack Paulo (23) na Ibrahim Ibu (24) ambao ni wachimbaji wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani walimbaka, kumlawiti.

Amesema washtakiwa hao na wenzao watatu Februari 4, 2025 kwa pamoja walimbaka msichana huyo ambaye ni muhudumu wa bar ya Feri mwenye umri wa miaka 24.

Ameeleza kwamba wakati msichana huyo usiku huo wa saa 8 akitoka kazini akitembea kwenda nyumbani alimuona mshtakiwa wa kwanza Meshack akiwa na pikipiki kisha akampakiza.

Amesema alipakia pikipiki hiyo na walipofika na eneo la karibu na kanisa la Ngurumu ya Upako wakati akipelekwa nyumbani walisimamishwa na watu wengine wanne wakawa watano.

Ameeleza kwamba aliwatambua watu hao kutokana na mwanga wa nishati ya umeme iliyokuwa kwenye eneo la kanisa hilo wakaanza kumkaba.

Ameeleza kwamba katika ushahidi wake msichana huyo akadai kuwa mshtakiwa wa kwanza Meshack alimziba mdomo kisha wakambaka kwa zamu.

Amesema pia washtakiwa hao wakamnyang'anya simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh600,000 na fedha Sh70,000.

Katika utetezi wao mshtakiwa namba moja Meshack alikubali kuwa eneo la tukio ila hakushiriki ubakaji na mshtakiwa wa pili ameeleza kwamba hakuwepo kwenye tukio hilo.

Hata hivyo, hakimu Nicodemo akisoma hukumu hiyo ameeleza kwamba mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu miaka 30 kwenda gerezani.


UPANDE wa Mashtaka katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vanilla International, Simon Mkondya maarufu Dkt. Manguruwe, umedai kuwa unatarajia kusoma hoja za awali Novemba 20, mwaka huu.

Wakili wa serikali Titus Aaron amedai hayo leo Novemba 18, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kuomba muda wa nyongeza kufuatia kubaini kuwepo kwa wadai wengine zaidi ya 100 ambao ni sehemu ya ushahidi na wanapaswa kuongezwa kwenye hati ya mashtaka.

Shauri hilo lenye namba 31523/2024 lilipangwa kutajwa leo kwa ajili ya kusomwa hoja za awali, lakini shughuli hiyo iliahirishwa baada ya Jamhuri kueleza kuwa kumekuwa na walalamikaji zaidi ya 100 ambao hawakuingizwa kwenye hati ya mashtaka.

Wakili Aaron amedai kuwa maelezo ya walalamikaji hao ni sehemu ya rekodi ya shauri na wanatarajiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa, hivyo hawatakiwi kuingizwa kwenye hati baada ya ushahidi kuanza kusikilizwa.

Amedai kuwa hatua inayofuata ni kuongeza idadi ya wadai pekee kwani upelelezi umeshakamilika.

Upande wa utetezi ulipinga hoja hiyo ukidai kuwa shauri limefikishwa mahakamani tangu Novemba 5, 2024, na kwa kipindi chote hicho Jamhuri ilikuwa ikisema upelelezi haujakamilika.

Hata hivyo, wiki iliyopita walieleza kuwa upelelezi umekamilika na kuwapatia nyaraka kama taratibu zinavyoelekeza.

Utetezi ulidai kuwa kuongezwa kwa wadai hao sasa ni ishara kuwa upelelezi bado haujakamilika, hivyo wakaomba shauri liendelee kama ilivyopangwa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Nyaki aliiahirisha kesi hadi Alhamisi, Novemba 20, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali na kuuagiza upande wa Jamhuri kuhakikisha umeweka taarifa za nyongeza katika hati ya mashtaka.

Mbali na Dk Manguruwe, mshtakiwa mwingine ni aliyekuwa mkaguzi wa kampuni hiyo, Rweyemamu John kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kujipatia zaidi ya Sh milioni 90 kwa kununua viwanja tisa katika eneo la Idunda, Mkoa wa Njombe.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, makosa hayo yanadaiwa kutendwa kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam. Washtakiwa wanadaiwa kufanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kupata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizoweka na kujipatia Sh milioni 92.2 kutoka kwa watu 19.

Inadaiwa kuwa kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 1, 2023, Dkt. Manguruwe alijipatia viwanja tisa katika eneo la Idunda mkoani Njombe akijua kuwa vinatokana na makosa ya upatu. Mshtakiwa John yuko nje kwa dhamana, huku Dkt. Manguruwe akiendelea kushikiliwa mahabusu kutokana na shtaka la utakatishaji fedha.
MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeahirisha kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hadi itakapopangiwa kikao kingine (session).

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga kuiomba mahakama ahirishe ili waweze kupata muda wa kujibu mapingamizi yaliyowasilishwa na Lissu akipinga shahidi wa siri kuongea akiwa haonekani.

Mapema, Wakili Katuga alidai mahakamani hapo kuwa leo Novemba 12, 2025 kesi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na wanaye shahidi, lakini shahidi huyo ni mmoja kati ya wale ambao mahakama ilitoa amri ya wao kutoa ushahidi kwa siri.

Hata hivyo, shahidi huyo ambaye alikuwa haonekani alipoitwa mahali alipokuwa amesimama na akaulizwa kama anasikia, ilisikika sauti ndani ya ukumbi wa mahakama kutokea kwenye boksi kubwa la mbao ikisema, “Ndiyo nasikia.”

Lissu alinyoosha mkono mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, akidai kuwa hakubaliani na shahidi wa siri.

Lissu alitumia hoja saba kupinga utaratibu huo akijikita katika tafsiri za kanuni za ulinzi wa mashahidi, lakini pia akirejea uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi katika ombi lililotolewa na Jamhuri mapema wakati kesi hii inaanza juu ya kwamba baadhi ya mashahidi wao watakuwa wa siri.

“Kwa mujibu wa kanuni hizo, kizimba maalum ni eneo ambalo shahidi haonekani na mtu yeyote isipokuwa majaji. Lakini hapa, majaji wenyewe hawawezi kumuona shahidi jambo ambalo halikubaliki kisheria,” alisem Lissu.

“Hicho kiboksi siyo kizimba cha kisheria. Huyo shahidi haonekani hata kwa majaji,” alisema Lissu.

Pia amedai kuwa hakuna sehemu inayoonyesha majina ya mashahidi wanaotakiwa kulindwa yalipelekwa kwa Jaji, kwani ni lazima Jaji aridhike kwamba huyu ni shahidi na maisha yake yako hatarini kweli.

Aidha, alieleza kuwa amri ya ulinzi wa mashahidi iliyotolewa Julai 2025 haikutoa ruhusa ya kutumia kiboksi hicho, na kwamba kanuni mpya za ulinzi wa mashahidi haziwezi kutumika kwa kesi iliyoanza kabla ya kutungwa kwake.

Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga aliomba kuahirishwa kwa shauri hilo ili kupata muda wa kujibu hoja za Lissu, akisema hoja hizo ni nyingi na zinahitaji uchambuzi wa kina.

Na Mwandishi Wetu
MAWAKILI wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, John Heche katika shauri la kushikiliwa kwa kiongozi huyo, wameiomba Mahakama iwape siku tatu kwa ajili ya kufanya utafiti na kujipanga kujibu pingamizi za upande wa Jamhuri.

Mawakili hao wakiongozwa na Selemani Matauka akisaidiana na mawakili Fredrick Msacky, Paul Kisabo, Neema Salum, Dorice Kafuku na Maduhu William, waliwasilisha mahakamani ombi kwa niaba ya Heche kuwataka wajibu maombi kumfikisha mahakamani au kumwachilia kwa dhamana.

Wajibu maombi ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspector General of Police - IGP), Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu (Dar es Salaam - ZCO), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (RCO), Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Kiongozi wa Mawakili hao, Matauka, aliomba siku hizo Novemba 10,2025 mbele ya Jaji Obadia Bwegoge baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Agatha Pima, kuieleza Mahakama kuwa wamewasilisha pingamizi la awali na pia wameshawapatia taarifa ya pingamizi waleta maombi.

"Upande wa wajibu maombi tulipewa nafasi ya kujibu kiapo kinzani, kwa sababu juzi ilikuwa Jumapili, waleta maombi tuliwapa taarifa ya kiapo leo (jana), lakini pia kabla hatujaendelea na kiapo kinzani, tumeleta pingamizi la awali," alidai Wakili Pima.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Matauka alidai kuwa ni sahihi kwamba maombi yaliyokuwa mbele yake yaliitwa kwa ajili ya kusikilizwa na kwamba nusu saa iliyopita ndiyo alipewa taarifa hiyo ya kiapo kinzani na wajibu maombi.

"Ni maombi yetu kwa upande wa waleta maombi kwamba kwa sababu kuna pingamizi la awali, tungepewa nafasi ya kufanya utafiti na kujipanga. Naomba iahirishwe kwa ajili ya kwenda kujiandaa kujibu hoja za pingamizi, tunaomba siku tatu ambayo ni Novemba 13, 2025," aliomba Matauka.

Jaji Bwegoge aliuuliza upande wa wajibu maombi kuhusiana na ombi hilo, ambapo Wakili Pima alidai kuwa hawana pingamizi na kwamba wapewe muda wa kujiandaa.

"Waleta maombi wenyewe ndiyo wameomba muda, nahisi wanahitaji muda zaidi wa kujiandaa. Mahakama imeridhia ombi lao, na shauri litaendelea Novemba 13, 2025 saa 4:30 asubuhi," alisema Jaji Bwegoge.

Heche anashikiliwa na polisi tangu Oktoba 22, 2025, alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa na Wakili Hekima Mwasipu Novemba 4, 2025, ilieleza kuwa Heche amepewa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi kutoka Kimara hadi Magomeni na kujihusisha na vitendo vya kigaidi maeneo ya Msewe na External.


MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu hadi Jumatano Novemba 12, 2025 baada ya upande wa Jamuhuri kueleza kuwa Lissu ameshindwa kuletwa kwa sababu za kiuslama.

Mapema leo wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issa akisaidiana na wakili wa serikali Mwandamizi Cathbert Mbilinyi alidai mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde kuwa mshtakiwa Lissu hajaletwa leo na walipofuatilia magereza wameambiwa ni sababu za kiusalama.

"Waheshimiwa majaji, kesi leo ilikuwa inakuja kwa ajili ya kuendelea kusikiizwa, kwa shahidi wa upande wa mashtaka, mshtakiwa Tundu lissu hayupo mahakamani na tumewasiliana na mkuu wa magereza amesema ameshindwa kumfikisha kwa sababu za kiusalama." Amedai Issa.

Amedai kuwa kesi ilikuwa iendelee na uslilizwaji Novemba 3 na kutokana na hali ha kiusalama kutokuwa imetengemamaa huko nje ikapangwa leo (Novemba 10, 2025) kwa ajali ya kuendelea na usikilizwaji....kutokana na hali ya Dar es Salaam kutokuwa kwenye utulivu pia mashahidi waliopaswa kufika kutoka Mbeya na Ruvuma wameshindwa kufika kwa ajili ya maandalizi ya usikilizwaji wa shauri hili.

Amedai kuwa,kufuatia hali hiyo hawakuwa wamepata shahidi kutokana na hali ya usalama wa jiji la Dar es Salaam kutokuwa salama kwa asilimia 100, hivyo akomba shauri hilo liahirishwe kwa siku 14 chini ya kifungu cha sheria cha 302 (1) cha CPA

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 12, 2025 kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa. Mahakama imewataka upande wa Jamhuri kuhakikisha siku hiyo wanakuwa na shahidi. Pia imetoa hati ya wito kwa mshtakiwa aletwe mahakamani kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri.
WATU 95 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo uhaini.

Washtakiwa hao wanafanya jumla ya watu waliofikishwa mahakamani hapo kwa siku ya leo ambao wanakabiliwa na kesi za uhaini kuwa 240 ikiwemo Mfanyabiashara Jenifer Jovin ‘Niffer’

Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkuu, Hassan Makube ambaye ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 19, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Awali wakisomewa mashtaka yao, Imedaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi, hadi Oktoba 29,2025 wanadaiwa walikula njama na kupanga kwa siri kufanya kosa la uhaini.

Katila shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa Oktoba 29, 2025, katika maeneo Sinza ndani ya jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliunda nia ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa kutishia mamlaka na kusababisha uharibifu wa mali za serikali.

MAHAKAMA Kuu masjala ndogo ya Dar es salaam imekubaliana na pingamizi la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu la kuzuia vielelezo vya upande wa Jamhuri kuingia kwenye kesi ya uhaini inayomkabili.

Awali Lissu alitoa pingamizi akimpinga shahidi huyo kuwasilisha taarifa ya uchunguzi kama kielelezo akidai kuwa shahidi aliyeletwa na upande wa Jamhuri hana sifa za kisheria kuwasilisha ushahidi huo mahakamani.

Aidha, Mahakama hiyo imesema kwa msimamo wake haikubaliani na Wakili wa Serikali Mkuu Job Mrema kwamba kuna mtego sehemu yoyote na pia haiwezi kuingia kwenye mtego wa kukiuka sheria.

Uamuzi huo mdogo umetolewa Oktoba 23,2025 na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde wa Mahakama hiyo, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na kukubaliana na pingamizi zilizowasilishwa na Lissu.

"Shahidi huyu, licha ya kuwa ofisa mwenye taaluma ya uchunguzi wa picha, hakuteuliwa kama mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (cyber expert) bali alipewa jukumu maalum la kuchunguza na kuhakiki picha mnato zilizowasilishwa kwake kwa maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)," amesema Jaji Karayemaha.

Jaji Karayemaha amebainisha kuwa majukumu ya shahidi huyo yamefafanuliwa wazi katika Tangazo la Serikali (GN) namba 779 la mwaka 2020, mamlaka yake yanahusiana na uchunguzi wa picha na kuandaa cheti cha uhakiki (certificate) baada ya uchunguzi, siyo kuandaa ripoti ya kitaalamu (expert report) kama ambavyo ilifanyika katika kesi hii.

“Shahidi huyu alikuwa na wajibu wa kuandaa cheti cha uthibitisho wa picha baada ya uchunguzi wake, lakini badala yake aliwasilisha ripoti ambayo kisheria haiwezi kutumika kama ushahidi wa kitaalamu,” amesema Jaji Karayemaha.

Pia, Mahakama imekubaliana na hoja za Lissu kupinga kupokelewa kwa taarifa hiyo kwa maelezo kwamba vyombo vilivyodaiwa kuhifadhi picha mjongeo, ikiwemo flashi disk na kadi ya kumbukumbu, vilishakataliwa na Mahakama, hivyo hakuna msingi wa kupokea taarifa inayohusiana navyo.

Amesema kwa kuwa vifaa hivyo vilivyodaiwa kuwa chanzo cha picha havikukubalika kama vielelezo, hakuna sababu ya kupokea taarifa yoyote inayotokana navyo. Hivyo, kielelezo hicho hakiwezi kupokelewa.

"Tunakubaliana na mshtakiwa kutokana na vifaa hivyo kukataliwa, hiyo taarifa inaenda kuelezea nini, tunaipokea kufanya nini, ndiyo maana tunasema tukiwa tunaongozwa na kesi ya Jamhuri dhidi ya Sharifu Mohamed huyu shahidi hana uwezo wa kutoa hii taarifa.

"Kwa hiyo tunaona pingamizi la mshtakiwa lina mashiko na sisi hatutaipokea hiyo taarifa ambayo walitaka kuitoa kupitia shahidi namba tatu," amesisitiza Jaji Karayemaha.

Pia, amesema wakati Wakili Mrema anawasilisha hoja zake alizungumzia suala la Mahakama kuingia kwenye mtego wa mshtakiwa kutokana na pingamizi alizoziwasilisha.

"Kwa msimamo wa Mahakama hatukubaliani na Wakili Mrema kwamba kuna mtego sehemu yoyote na sisi hatuwezi kuingia kwenye mtego wa kukiuka sheria," amesema Jaji Karayemaha.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, Mahakama imeridhia pingamizi lililowasilishwa na Lissu na hivyo kutupilia mbali kielelezo hicho, ikibainisha kuwa shahidi husika hana sifa za kisheria za kutoa taarifa ya uchunguzi wake kama kielelezo katika kesi hiyo.

Awali, Wakili Mrema alidai kuwa pingamizi la mshtakiwa halina mashiko na pia Mahakama hiyo haifungwi na uamuzi wake uliotoa kuhusu flash disks na kadi ya kumbukumbu (memory card).

"Mshtakiwa alienda mbali kwa kuingilia maudhui ya ripoti na kuanza kuzisoma na kwamba hilo lilishakataliwa na Mahakama ya Rufaa, kielelezo kinatakiwa kiwe safi ndiyo kisomwe, kwa hiyo ni kinyume na sheria," alidai Wakili Mrema.

Baada ya uamuzi huo, Lissu alipewa nafasi ya kumuuliza shahidi maswali ya dodoso kutokana na ushahidi wake aliyoutoa mahakamani wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Thawabu Issa.

Lissu alisoma maelezo yote ya shahidi na kumsomea shahidi maneno 75 ambayo anataka kumuhoji ili ayakanushe, ikiwemo eneo la elimu ya shahidi huyo.
MKAGUZI wa Polisi kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao, PF 22863 John Kaaya (45), ameieleza Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, namna alivyogundua maudhui yenye viashiria vya jinai katika picha mjongeo (video clip) alipokuwa akifanya doria mtandaoni.


Kaaya ametoa ushahidi huo leo Oktoba 9,2024 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, likisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.


Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, Kaaya amesema yeye ni mpelelezi katika dawati la doria mtandaoni, akifafanua kuwa kazi yake ni kufuatilia maudhui katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama YouTube, Instagram, TikTok, Facebook na mingineyo.


Ameeleza kuwa doria hizo hufanyika saa 24 kila siku, kwa siku saba za wiki, kwa mfumo wa zamu unaopangwa ofisini, na lengo kuu ni kubaini makosa ya jinai yanayofanywa kupitia mitandao, kwa kutumia programu maalum za uchunguzi wa kidijitali.


Shahidi huyo amesema kuwaAprili 4, 2025, akiwa zamu kuanzia saa 12:00 asubuhi, alianza kukagua kompyuta yake ya kazi na kujiridhisha kuwa ipo salama kwa matumizi. Baadaye aliingia katika mtandao wa YouTube na kufika kwenye ukurasa wa www.youtube.com/@JamboTv,
ambapo aliona video yenye kichwa cha habari “Tundu Lissu uso kwa uso na wafuasi wa CHADEMA Majimboni: No Reform No Election – Njia Panda.”


Kaaya ameeleza kuwa alivutiwa kuchunguza video hiyo kutokana na idadi kubwa ya watazamaji na maoni yaliyokuwa yakitolewa, na alipoiangalia alibaini maudhui yenye viashiria vya jinai.


Kwa mujibu wa ushahidi wake, video hiyo ilimuonyesha Lissu akizungumza maneno yafuatayo


“Na ninyi mnataka mteuliwe kwenye cheo fulani? Nchi hii kwa hali ilivyo, hili linawezekana? Kama haliwezekani tufanyaje? Mkutano wetu unasema No Reforms, No Election. Wamesema kitu kimoja sahihi hapo. Msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli, ni kweli kwa sababu tumesema tutazuia uchaguzi, tutakinukisha sana sana.”


Baada ya kugundua hilo, Kaaya amesema alimjulisha Mkuu wake wa Kitengo ambaye alimuelekeza kuonana na Naibu Kamanda wa Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam (ACP) George Bagyemu.


Kaaya ameeleza kuwa alipofika kwa ACP Bagyemu na kutoa maelezo kuhusu video hiyo, alipewa maelekezo ya kuandaa taarifa rasmi. Kisha mnamo Aprili 7, 2025, alirudi tena kwa ACP Bagyemu ambaye alimuelekeza kupakua video hiyo na kuihifadhi kwa mfumo maalum.


Shahidi huyo amesema alitumia flash disk mpya kupakua video hiyo kwa mfumo wa MP4, ikiwa na urefu wa saa tatu na ukubwa wa MB 500, zoezi ambalo lilichukua dakika 15 kukamilika. Ameeleza kuwa video hiyo aliambatanisha na fomu ya PF 145 kisha kuiwasilisha kwa ACP Bagyemu kama kielelezo DM, kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu wa picha.


Ameongeza kuwa siku hiyo hiyo, ACP Bagyemu alimwita na kumtaka kumpatia nywila (password) aliyoitumia kulinda kielelezo hicho ili kuruhusu timu ya wachunguzi kuendelea na kazi.


Baada ya Kaaya kumaliza kutoa ushahidi wa awali, Wakili Mrema ameeleza kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa umekamilisha mahojiano yake na shahidi huyo. Lissu naye ameeleza kuwa yuko tayari kuanza maswali ya dodoso, lakini Mahakama ikaahirisha shauri hilo hadi kesho kwa kuendelea na usikilizwaji.




MVUTANO mkali umeibuka katika Mahakama Kuu Masijala ndogo Dar es Salaam kati ya Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Humphrey Polepole juu ya ombi la kutaka Balozi huyo wa zamani aletwe mahakamani.

Shauri hilo la maombi ya amri ya kufikishwa mahakamani limefunguliwa na mawakili wa Polepole, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala kwa niaba yake Polepole.

Mapema leo Aprili 9, 2025 wakili Kibatala ameomba mbele ya Jaji Salma Magimbi kuwasilisha kiapo cha ziada huku akiomba Mahakama itoe uamuzi wa maombi ya upande mmoja Polepole afikishwe mahakamani ili iweze kumuona wakati akisubiri shauri la maombi yake kusikilizwa pande zote.

Wajibu maombi Katika shauri hilo lililoitwa chini ya hati ya dharura, ni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polis Kanda Maalum Dar es Salaam (ZPC)

Kibatala aliieleza mahakama kuwa ingawa baadhi ya wajibu maombi hawakufika mahakamani, wote wamekuwa served kisheria, hivyo maombi yanaweza kuendelea hata bila wao kuwepo.

“Tumetambua kuwepo kwa DPP, lakini wengine wote hawajatokea. Wote hawa wamekuwa served na ushahidi upo mahakamani,” alisema Kibatala, akieleza kuwa hati za wito zilifikishwa kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Mwanasheria Mkuu (AG), Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Kamishna wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (ZCO) na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZPC).
Alisema IGP yuko Dodoma, lakini wito ulitumwa kupitia barua pepe rasmi ya jeshi la polisi (info.phq@tpf.go.tz) saa 5 asubuhi Oktoba 8, 2025. “Kwa amri ya mahakama kutumia teknolojia ya kisasa, tunaamini imemfikia IGP,” alisema.

Kibatala aliongeza kuwa AG na ZCO walithibitisha kupokea barua hizo, huku ZPC akipokea mara mbili

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Nguka aliiomba mahakama kuwapa muda wa hadi Jumanne ijayo ili kuwasilisha kiapo kinzani, akibainisha kuwa maombi hayo yameletwa kwa dharura na hivyo ofisi ya DPP imehitaji muda kufanya mashauriano ya kina na taasisi husika.

“Ni haki ya msingi kwa mjibu maombi kujibu maombi yaliyowasilishwa dhidi yake. Licha ya kwamba yameletwa kwa dharura, haki hiyo haiwezi kunyimwa,” alisema Nguka.

Kibatala alisisitiza kuwa tayari upande wake unakusudia kuwasilisha kiapo cha ziada kutokana na taarifa mpya zilizopatikana jana Oktoba 8 na leo asubuhi, aoktoba9,2025 akitaka mahakama iruhusu kiapo hicho kiwasilishwe leo ili mjibu maombi wa pili ajibu kwa pamoja vyote viwili.

Katika hoja zake za kisheria, Kibatala alirejea Kanuni ya III na IV ya GN 159 ya mwaka 1930 chini ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), akieleza kuwa maombi ya aina hii yanapaswa kusikilizwa ex-parte (upande mmoja) ikiwa mwombaji anaamini mtu anayehusika anashikiliwa kinyume cha sheria na mamlaka.

Hata hivyo, upande wa serikali ulipinga hoja hiyo, ukidai kuwa mwombaji hakubainisha ni nani hasa anayemshikilia Polepole, jambo linalofanya mahakama ishindwe kutoa amri ya kumleta mahakamani kwa sasa.

“Kiapo cha mwombaji hakioneshi wazi nani anamshikilia. kiapo kinasema anashikiliwa na watu wasiojulikana, jambo linaloleta utata. Haiwezekani mahakama kutoa amri bila kujua nani anashikilia mtu huyo,” alisema Nguka.

Kibatala alijibu akisema kiapo kinaeleza bayana kuwa mjibu maombi wa tano, yaani ZPC, ndiye anayehusishwa na kumshikilia Polepole, hivyo hakuna utata wowote.

“Aya ya 10 ya kiapo inasema nina sababu za kuamini mjibu maombi wa tano(ZPO) anamshikilia mwombaji. Kwa hiyo hoja kwamba hatujasema nani anamshikilia haina mashiko,” alisema.

Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Jumatano ijayo, ikitoa nafasi kwa wajibu maombi kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani, huku waombaji wakiruhusiwa kuwasilisha kiapo cha ziada kabla ya siku hiyo.

Kesi hiyo itaendelea saa nane mchana kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepiga marufuku kurushwa mubashara (live) kwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika hatua ya kusomewa maelezo ya mashahidi (committal proceedings).

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga, baada ya kukubaliana na ombi la upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, uliolenga kulinda usalama na utambulisho wa mashahidi.

Hakimu Kiswaga alisema kuwa hatua hiyo haiwazuii wananchi wala mshtakiwa kusikiliza kesi hiyo, bali inalenga kuzuia kufichuliwa kwa mashahidi wa siri.

“Kuzuia kurushwa mubashara hakumzuii mshtakiwa kusikilizwa, bali kunazuia ueneaji unaoweza kuhatarisha usalama wa mashahidi,” alisema Hakimu Kiswaga.

Kwa mujibu wa amri hiyo, vyombo vya habari au watu binafsi wamekatazwa kuchapisha au kusambaza nyaraka zozote zinazoweza kufichua majina, anuani au taarifa binafsi za mashahidi, isipokuwa kwa ruhusa ya Mahakama.

Uamuzi huu unafuatia agizo la Mahakama Kuu la Agosti 4, 2025, lililotolewa na Jaji Hussein Mtembwa, lililobainisha kuwa mashahidi ambao ni raia lazima walindwe kwa kufichwa utambulisho wao, wakati wale ambao si raia watatoa ushahidi kwa utaratibu wa kawaida.

Baada ya amri hiyo kutolewa, maafisa wa Mahakama Kuu waliokuwa wakirusha mubashara kesi hiyo walilazimika kuzima kamera zao.

Lissu anakabiliwa na tuhuma za uhaini, ambapo inadaiwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, alitoa kauli zinazodaiwa kushawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania.
MAHAKAMA Kuu ya Masijala ya Dar es Salaam imekubali ombi la upande wa Jamhuri la kuficha majina na taarifa nyingine za mashahidi raia wa upande wa Mashitaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Akisoma uamuzi huo leo, Agosti 4, 2025, Jaji Hussein Mtembwa amesema kutokana na uzito wa kosa la uhaini na hofu ya mashahidi kutishiwa, ni haki kwa mashahidi raia kulindwa kwa kutotajwa majina yao, anuani wala mahali walipo katika hatua ya committal, Preliminary Inquiry (PI) na hata wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Jaji Mtembwa amesema kwa mujibu wa kiambatanisho kilichowasilishwa na upande wa mashtaka, kesi inayomkabili mshtakiwa katika Mahakama ya Kisutu inahusu uhaini. Akifafanua zaidi, amesema kwa kuwa mshtakiwa ana wafuasi wengi ndani na nje ya nchi, na kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa na ACP Amini Mahamba kuwa mashahidi hao wanatishiwa na watu wa karibu na mshtakiwa ili wasitoe ushahidi mahakamani, usalama wao unaweza kuwa hatarini.

"Nilichokiona ni kwamba kosa la mshtakiwa ni kati ya makosa makubwa, na pili, mashahidi hawa wanaotarajiwa kwa kiapo cha ACP Mahamba ni kwamba wanatishiwa... Sisi kama Mahakama tukifikia hapo, tutaangalia Sheria inasemaje," amesema Jaji.

Ameongeza kuwa Sheria inaruhusu kuwalinda mashahidi na watoa taarifa, hasa pale ambapo wao au familia zao wako katika hatari ya kudhuriwa, ingawa pia inapaswa kuzingatiwa kuwa mshtakiwa ana haki ya kumuona na kumhoji shahidi.

"Mahakama ina wajibu wa kulinganisha haki zote mbili kwa uwiano kwa lengo la kutenda haki. Nimeamua kukubali maombi ya kuficha mashahidi ambao ni raia tu," amesema.

Hata hivyo, Mahakama imekataa ombi la Jamhuri la kuficha taarifa za mashahidi wote bila kujali uraia, na kueleza kuwa mashahidi ambao si raia wataendelea kutoa ushahidi kwa kawaida na kwa majina yao halisi.

"Kama shahidi si raia, atatoa ushahidi katika hali ya kawaida kwa kuonekana na bila kufichwa jina au taarifa nyingine zinazomhusu," amesema.

Aidha, Mahakama imeiagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuandaa utaratibu wa kuchuja (screen) taarifa zote zitakazowasilishwa mahakamani ili kuondoa zile zinazoweza kufichua utambulisho wa mashahidi raia.

Pia, Mahakama imesema vyombo vya habari havitaruhusiwa kuchapisha au kutangaza taarifa yoyote inayoweza kufichua utambulisho wa mashahidi hao bila kibali cha Mahakama.

"Wakati wa committal, PI na hata wakati wa usikilizwaji, suala la kuchapisha au kusambaza taarifa zenye majina ya mashahidi wa upande wa mashtaka limepigwa marufuku. Haina maana unaficha mahakamani halafu chombo cha habari kinamtaja shahidi. Vyombo vya habari vitaruhusiwa kufanya hivyo tu kwa kupata kibali cha Mahakama," amesema.

Mahakama imekazia kuwa hairuhusiwi kusambaza au kuchapisha taarifa yoyote inayoweza kufichua jina, makazi, ndugu, marafiki au watu wa karibu wa mashahidi hao isipokuwa kwa ruhusa maalum kutoka kwa Mahakama.