Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Stephen Kebwe anamsikiliza Mgeni wake baada ya kumkabidhi kitabu kinachoonyesha
maeneo ya Uwekezaji Mkoani Morogoro (Morogoro Region Investment Guide).
Na. Andrew Chimesela - Morogoro
Serikali ya Uingereza imeonesha nia ya kushawishi wawekezaji nchini mwake
kuja kuwekeza hapa nchini hususan katika Mkoa wa Morogoro katika Sekta
mbalimbali ikiwemo Sekta ya Kilimo, viwanda na Madini.
Hayo yamefahamika jana Julai 18 mwaka huu wakati wa mazungumzo
yaliyofanyika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro baina ya Balozi wa
Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke na Dkt. Kebwe Stephen Kebwe
Mkuu wa Mkoa huo.
Awali viongozi hao wawili walianza mazungumzo yao kuhusu miradi ya
maendeleo inayofadhiliwa na Uingereza hapa nchini hususan iliyopo Mkoani
Morogoro ikiwemo miradi ya Elimu - Educationa Programme for Results
(EP forR), ambapo Mhe. Cooke alisema nchi yake imeongeza ufadhili wake
kutoka 34% mwaka 2012 hadi 70/% mwaka 2016.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Stephen Kebwe akimkabidhi Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke kitabu cha Uwekezaji.
Kwa upande wa Afya Balozi huyo alisema katika Mkoa wa Morogoro, Uingereza
imefadhili Vituo vya Afya katika eneo linalolenga Mpango wa Uzazi kwa akina
mama kupitia Mradi wa Population Service International (PSI) ambapo hadi sasa
jummla ya akinamama 9,400 Mkoani humo wamefaidika na huduma hiyo.
Aidha, Viongozi hao wawili walizungumzia ufadhili unaotolewa na Uingereza
katika nyanja za Maji na Usafi wa Mazingira ikiwemo Kampeni inayoendelea sasa
Mkoani Morogoro ya usichukuliepoanyumbanichoo, Mkoa huo ukiwa ni Mkoa wa
Majaribio katika Kampeni hiyo.
Pamoja na miradi mingine mingi waliyoizungumzia , Viongozi hao pia waligusia
miradi ya Sekta ya Kilimo na Miundombinu. Kwa upande wa Sekta ya
Miundombinu upo mradi wa IRAT yaani Improving Rural Access in Tanzania
ambapo Uingereza imefadhili matengenezo ya makaravati ya barabara ya
Chagongwe - Kumbulu iliyopo Wialaya ya Gairo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Stephen Kebwe anamsindikiza mgeni wake, Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke baada ya kukamilisha mazungumzo yao.
Baada ya kumaliza mazungumzo kuhusu miradi inayofadhiliwa na nchi ya
Uingereza, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe
alimshukuru Balozi wa Uingereza kwa Ufadhili wa miradi yote hiyo ukiwemo
mradi mkubwa wa Upimaji na umilikishaji wa Ardhi unaotekelezwa katika Wilaya
za Kilombero, Ulanga na Malinyi kupitia Land Tenure Support Programme.
Dkt. Kebwe ametumia fursa hiyo kumweleza Balozi Sarah Cooke uwepo wa
maeneo mazuri ya uwekezaji katika Mkoa wa Morogoro na akawasilisha ombi kwa
balozi huyo kushawishi wawekezaji walioko nchini mwake kuja kuwekeza Mkoani
Morogoro katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Kilimo, viwanda na uchimbaji wa
madini ya dhahabu na Graphite.
Balozi Sarah Cooke alionekana kushawishika na ombi la mwenyeji wake na
kuahidi kulifanyia kazi haraka huku akiahidi kutafuta muda wa kufanya ziara
katika Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kutembelea miradi wanayoifadhili lakini
pia kutembelea maeneo ya uwekezaji kama alivyokuwa ameombwa na mwenyeji
wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...