*Ataka watenge siku tatu hadi nne waende waliko wananchi
*Asema Serikali hii haitaki mambo ya urasimu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wote wa Serikali za Mitaa nchini watenge theluthi mbili ya muda wao wa kazi kwa kuwasikiliza wananchi na kuwahudumia.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“Jukumu la watumishi ni kuwatumikia wananchi, Serikali hii hatutaki urasimu na wala hatutarajii kuwa mtatoa huduma kwa urasimu. Lugha ya ‘njoo kesho, njoo kesho’ siyo ya kwa awamu hii.”

Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wana jukumu la kusimamia agizo hilo kwa kuhakikisha kuwa wanatoa usafiri kwa watumishi hao ili waweze kufika vijijini kwa haraka. “Wakurugenzi wa Halmashauri simamieni zoezi hilo kwa kupanga ratiba na kutoa gari ili maafisa wanne au watano watumie gari hilo kwenda vijijini wakawahudumie wananchi.”

Amesema wananchi wengi hawana uwezo wa kusafiri kutoka vijijini hadi mijini ili kuleta matatizo yao, kwa hiyo wakifanya hivyo, watumishi watakuwa wamewapunguzia matatizo wananchi.Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya kikazi mkoani humo, amewataka watumishi wa idara ya ardhi wapime ardhi kwa wingi na watoe hati mapema ili wananchi wazitumie kuongeza mitaji.

“Pimeni ardhi na kutoa hati ili wananchi wazitumie kukopa na kupata mitaji ya kujiendeleza kiuchumi. Pia muweke mipango mizuri ya ardhi ili kuepusha migogoro baina ya wananchi.Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Kahama kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 15, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea eneo la Viwanda la Bukondamoyo katika Kata ya Zongomela kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kahama Julai 15, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...