NA Suleiman Msuya,Morogoro 
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe amesema elimu ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) ikisambazwa nchini kote misitu itakuwa endelevu na kuepusha nchi kuingia katika jangwa. 

Dk. Kebwe aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 18 wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) uliofanyika mkoani Morogoro. 

Alisema iwapo elimu ya USM itasambaa kwa kila mwana jamii ni dhahiri rasilimali misitu itakuwa salama kwa muda mrefu hivyo ni imani yake kila kiongozi atatoa kipambele. 

Mkuu huyo wa mkoa alisema uhifadhi misitu ni jambo ambalo haliepukiki hasa katika kipindi hiki kwa kuwa madhara yakutohifadhi yameshaonekana jwa sasa. 

“Napenda kutumia nafasi hii kuziomba mamlaka husika ili elimu ya USM ifikie kila kiongozi katika nchi kwani takwimu za kuharibiwa kwa hekta 469,000 kila mwaka ni dalili za jangwa na Morogoro pekee inaharibu hekta 150,000 sawa na asilimia 48 ya uharibifu wote,” alisema. 

Alisema iwapo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) itaweka taratibu ambazo zitaelekeza njia mbadala ya kukabiliana na uvunaji wa miti kwa sababu ya kaa hali itakuwa salama. 

Dk. Kebwe alisema kinachoonekana kwa sasa ni kukosekana kwa maelekezo sahihi ambayo yatasababisha sheria kusimamiwa kikamilifu. 

Alisema katika mkoa wake atahakikisha wasaidizi wake wanasimamia rasilimali misitu kwa weledi huku ikifaidisha jamii zaidi ambayo inazungukwa na misitu hiyo. 

Mkuu huyo wa mkoa alisema iwapo kila mkoa utatembea na dhana ya kuhakikisha jamii inanufaika na rasilimali hiyo ni wazi kuwa ulinzi utakuwepo na dhana ya uchumi wa viwanda itaonekana moja kwa moja. 

Mwenyekiti wa Mjumita Taifa, Revocatus Njau alisema wao wamejikita katika kutoa elimu ya usimamizi shiriki wa misitu baada ya kugundua jamii kubwa haina uelewa. 

Njau alisema pamoja na elimu pia wanahakikisha jamii inamiliki misitu inanufaika nayo kwa kufanya shughuli za kiuchumi kwa kufuata sheria za nchi. 

“Kwa miaka 18 tumekuwa tukitoa elimu ya utunzaji na unufaikaji kupitia rasilimali misitu, ila ipo changamoto kwa baadhi ya watendaji wa vijiji na kata kushirikiana na waharibifu wa misitu hali ambayo inatudisha nyuma,” alisema. 

Kwa upande wake Ofisa Misitu Mwandamizi kutoka Tamisemi Rogasian Lukoa alisema Serikali inajipanga kuhakikisha elimu ya USM inasambaa kwa kila mwanajamii ili kuwa mlinzi sahihi wa rasilimali hiyo. 

Lukoa aliwataka watendaji wa Serikali kuanzia ngazi za vijiji kushirikiana na taasisi kama Mjumita, Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Jamii Tanzania (TFCG) na wengine ili kuhakikisha misitu inakuwa endelevu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...