Na Greyson Mwase, Kilwa.
Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo ameitaka Tume ya Madini kufanya uchunguzi kuhusu
mgogoro kati ya kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya
Kizimbani inayomilikiwa na Seleman Mohamed na wananchi wa kijiji cha
Hotel Tatu kilichopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Naibu Waziri Nyongo ametoa
agizo hilo leo tarehe 15 Desemba, 2018 katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kijiji hicho wakati wa utatuzi wa mgogoro huo ikiwa
ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Lindi yenye lengo
la kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji
wa madini.
Alisema kuwa, baada ya
kusikiliza pande zote mbili imeonekana kuna haja ya Tume ya Madini
kufanya uchunguzi ili kubaini namna utoaji wa leseni ya uchimbaji wa
madini ya jasi kwa kampuni ya Kizimbani ulivyofanyika kabla ya kufanya
maamuzi kwa mujibu wa sheria na kanuni za madini.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri Nyongo alisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini
haitasita kuwaondoa maafisa madini wakazi wa mikoa watakaobainika kuwa
ndio chanzo cha migogoro kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini.
“ Kama Serikali tunataka
kuhakikisha leseni za utafiti na uchimbaji wa madini zinatolewa kwa
kufuata sheria na kanuni za madini bila kuwepo kwa migogoro ya aina
yoyote, aidha hatutasita kumwondoa afisa madini mkazi yeyote
atakayebainika kuwa chanzo cha migogoro kwenye shughuli za utafiti na
uchimbaji wa madini,” alisema Naibu Waziri Nyongo huku akishangiliwa na
wananchi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akielekeza jambo kwenye sehemu ya kukusanya madini ya jasi iliyopo katika eneo la Hoteli Tatu Wilayani Kilwa mkoani Lindi. Kushoto mbele ni Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia Omari.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia madini ya chumvi katika eneo la Jangwani kwa Chinja lililopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Sehemu ya wazalishaji wa madini ya chumvi katika eneo la Kilwa Masoko lililopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi wakisikiliza maelezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano uliofanyika katika eneo hilo wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...