Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Madini wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanatekeleza kwa haraka maagizo yaliyotolewa na Rais John Pombe Magufuli ikiwemo kuanzisha masoko ya madini kwa lengo la kukabiliana na changamoto za utoroshwaji wa madini na migogoro kwa wachimbaji wadogo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini kwa lengo la kukabiliana na changamoto hizo ili kuongeza tija katika sekta ya madini.

“Kwa muda mrefu Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza kuhusu Sekta ya Madini kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu, sekta hii imekuwa na changamoto licha ya jitihada mbalimbali kuchukuliwa kuhakikisha changamoto hizo zinaondolewa kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya madini” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kutokana na umuhimu wa masoko hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi hao kuhakikisha kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini zinakamilika haraka kwa lengo la kusaidia wadau kupata soko la uhakika huku serikali ikinufaika na mrahaba na tozo mbalimbali.

“Nyote mtakubaliana nami kuwa kukamilika kwa kanuni hizo kutasaidia wananchi kupata masoko ya uhakika ya madini na wakati huo huo serikali kunufaika na mrahaba na tozo mbalimbali zinazotozwa kwa mujibu wa sheria” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa kuwa pindi kanuni hizo zitakapokuwa tayari zifikishwe kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya kwa lengo la kuhakikisha makundi yote yanakuwa na uelewa wa kutosha na hatimae kuzisimamia kikamilifu kwa kushirikiana na Tume ya Madini.

“Ofisi ya Rais- TAMISEMI kupitia Wakuu wa Mikoa na Maafisa Tawala wa Mikoa wakishirikiana na Wizara pamoja na Tume ya Madini hamna budi kuhakikisha mnaandaa utaratibu ambao utawawezesha Wakurugenzi katika Halmashauri husika kutoa maoni yao katika kuanzisha masoko hayo na maoni hayo yawasilishwe Wizara ya Madini haraka kupitia Tume ya Madini ili yaweze kuzingatiwa kwenye kanuni zilizoandaliwa” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewatakwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la Ulinzi na Usalama wa masoko hayo katika Mikoa yao.“Serikali inategemea kuwepo na hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo hayo ili kuwahakikishia wafanyabiashara, Wachimbaji na wananchi kwa ujumla usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini hayo” amesisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo mbalimbali yaliyotolewa yenye lengo la kuboresha mchango wa sekta ya Madini nchini.

“Tanzania ni moja kati ya nchi zenye uzalishaji mkubwa wa madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu na vito ambapo kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalumu wanayoweza kufanyia biashara ya madini hali iliyochangia kuwepo kwa utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha Serikali mapato stahiki” ameeleza Waziri Biteko.

Waziri Biteko amesema kuwa, Ili kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati ya wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali ili kuandaa rasimu ya kanuni za kuanzisha na kusimamia masoko ya madini nchini.

Hivyo, amewaomba Wakuu wa Mikoa, Maafisa Tawala wa Mikoa, Maafisa Madini, Wakaazi wa Mikoa na Wadau kwa ujumla kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kutimiza ndoto za muda mrefu za Wachimbaji wadogo, Wafanyabiashara wa Madini, Wadau na Watanzania wote kwa ujumla kufikia malengo hayo na kufanikisha sekta ya madini nchini
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...