Na Karama Kenyunko Globu ya Jamii.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia wa China,  Yang Glan maarufu kama Malkia wa meno ya tembo na wenzake wawili kutumikia kifungo cha miaka 17 gerezani kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 13.9.
Mbali na Glan, washitakiwa wengine ni wafanyabiashara Salvius Matembo na Philemon Manase ambao ni  raia wa Tanzania na wote kwa pamoja wamehukumiwa kifungo hicho leo Februari 20, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amesema katika shtaka la kwanza ya kujihusisha na genge la uhalifu, mshitakiwa Glan atatumikia kifungo cha miaka  15, huku washtakiwa Manase na Matembo wote watatumikia kifungo cha miaka 15 gerezani.

Aidha katika shtaka la tatu,  washtakiwa kila mmoja atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya mara mbili ya thamani ya meno hayo ambayo ni zaidi ya bilioni 27 wote kwa pamoja.

Pia Mahakama imeamuru nyumba iliyopo Muheza mkoani Tanga ambayo washtakiwa walikuwa wakiitumia kuhifadhia meno ya tembo itaifishwe na kuwa mali ya serikali.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Shaidi amesema licha ya kwamba washitakiwa ni wakosaji wa kwanza, madhara waliyosababisha ni makubwa katika uchumi wa taifa kwa kujiingizia kipato isivyohalali
Amesema, kitendo walichofanya washitakiwa hao kimelifanya taifa lisiingize kipato kwani linahitaji shule nzuri, barabara na hospitali hivyo hilo ni jambo baya na halikubaliki na kusema shitakiwa Manase na Matembo wamekuwa wasaliti kwa nchi na ndugu zako kwa kuamua kula katika giza na sasa wameletwa kwenye mwanga.

Amesema upande wa mashitaka kupitia mashahidi 11 waliowaleta kwa wameweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa pasipo kuacha shaka.

Kabla ya kutoa hukumu,  Wakili wa Serikali, Salim Msemo aliiomba mahakama kutoa adhabu  kali kwa kwa washitakiwa kwa mujibu wa sheria na kuiomba  izingatie kifungu cha 60 (2) cha Uhujumu uchumi sura ya 200 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002 ambacho kinaeleza kifungo ni miaka isiyozidi 15.

Pia aliomba mahakama izingatie sheria namba 84 (1) cha Sheria ya Usimamizi Wanyamapori 5/2009 kuwapa adhabu ya faini isiyochini ya mara mbili ya thamani za nyara husika kwa washitakiwa wote.

"Kifungu namba 111 (1) c na d na kifungu kidogo cha 2 cha sheria hiyo tunaomba kuleta maombi ya vitu vyote vilivyohusika katika utendajo wa makosa haya ikiwemo shamba lenye nyumba zilizotumika na uhalifu huu, mahakama inaruhusiwa kufanya utaifishaji bila kujali kitu chochote," amedai Msemo.

Washtakiwa kupitia Wakili, Nehemiah Nkoko, wameiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu ndio kosa lao la kwanza na kwamba wanafamilia zinazowategemea.

Amedai mama wa mshitakiwa Matembo alifariki wakati yeye akiwa gerezani mara baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kubomolewa kupisha ujenzi wa barabara ya Kimara, mshitakiwa wa pili, Manase ana watoto wanaosoma hivyo adhabu isitumike kuwanyima nafasi ya kulipiwa ada watoto hao ambao ni nguvu kazi ya kesho.

Pia alidai Glan ni bibi wa wajukuu ambaye ana umri zaidi ya miaka 75 hivyo afya yake sio nzuri na amekuwa akitaka matibabu.

Aidha Nkoko ameiomba mahakama katika kutoa adhabu izingatie miaka mitano waliyokaa washitakiwa mahabusu kwa sababu hawakupenda bali dhamana zao zilizuiliwa.

Pia amedai wanakusudia kukata rufaa.

Hakimu Shaidi amesma aelezo ya onyo ya washitakiwa wote yanaonesha ambavyo walifahamiana kwa muda mrefu na katika utetezi wao hawakupinga ushahidi uliotolewa kuhusu kujihusisha na biashara hiyo," alisema Hakimu Shaidi.

Washitakiwa wote, wanadaiwa,  kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014  walijihusisha na biashara  ya nyara za serikali.
Katika kipindi hicho washitakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 860 vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh.  bilioni  13.9 bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014  kwa makusudi raia wa China, Glan  aliongoza na kufadhiri vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo 860 vya meno ya tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Kwa upande wa washitakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, Kusafirisha na Kuuza Meno ya Tembo kwa nia yakujipatia faida.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...