Wakazi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na wapendwa wao mwishoni mwa wiki walipata fursa ya  kufurahia pamoja siku ya wapendanao yaani Valentine Day katika hafla maalum inayofahamika kama ‘Mkeka na Mvinyo’.

Hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam, ilishuhudiwa wakazi hao wakijitokeza kwa wingi sambamba na wapendwa wao ili kufurahia siku hiyo maalum ambapo pamoja na vinywaji vingine waliweza kufurahia mvinyo wa aina mbalimbali unaozalishwa hapa nchini.

Mbali na burudani nzuri ya muziki laini kutoka msanii Maximilian Rioba maarufu kwa jina la Milian, kivutio kingine kwenye hafla hiyo kilikuwa ni matumizi ya mikeka ambapo baadhi ya washiriki walipata fursa ya kuketi kwenye mikeka iliyoandaliwa sambamba na meza fupi wakipata vinywaji, vyakula huku wakifuatilia burudani ya muziki iliyokuwa inaendelea.

“Hii ni hafla yetu ya kwanza ya Mkeka na Mvinyo kati ya hafla nyingine nyingi za aina hii zitakazo fanyika SikuKuu ya Pasaka, Msimu wa Sabasaba, na mwisho wa mwaka yaani Likizo Time. Tunashukuru kuona hafla hii imepokelewa vizuri na wadau na  tunawaahidi mambo mazuri zaidi yanakuja kupitia Mkeka na Mvinyo waendelee kutuunga mkono,’’ alisema Bi Caroline Kirwanda Mratibu wa hafla hiyo kutoka kampuni ya Real PR Solutions (RPR).

Aliwashukuru baadhi ya wadau muhimu katika kufanikisha hafla hiyo kuwa ni pamoja na  kampuni ya uzalishaji wa mvinyo ya Alko Vintages ya jijini Dodoma, Hoteli ya Whitesands, Bodi ya Utalii  Tanzania, (TTB), GS 1, pamoja na kampuni ya magazeti ya TSN wazalishaji wa magazeti ya Daily News pamoja na Habari Leo.

Bi Kirwanda aliongeza kuwa hafla hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo utakaozinduliwa hivi karibuni unaolenga kutangaza utalii wa ndani pamoja kuvumbua fursa mbalimbali za kibiashara ndani ya nchini kwa lengo la kukuza uchumi unaofahamika kwa jina la ‘Domestic Tourism Promotion Initiative’ (DTPI).

“Tunahitaji kuhamasisha zaidi matumizi ya bidhaa za ndani ili kukuza uchumi wetu kama taifa,’’ aliongeza  bi Kirwanda.

Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Alco Vintages , Sweetbertha Rwabizi alisema ushiriki wao kama wazalishaji wa  mvinyo wa ndani  kwenye hafla hiyo unalenga kuhamasisha zaidi matumizi ya bidhaa hizo kwa kuwa tofauti na kuuza bidhaa zao pia walipata fursa ya kukutana moja kwa moja na watumiaji wa bidhaa hizo na hivyo kupata mrejesho kutoka kwao huku pia wakijenga uelewa zaidi kwa watumiaji kuhusu vinywaji hivyo.

“Iwapo watanzania watabadirika na kuanza kutumia bidhaa hii ya mvinyo unaozalishwa hapa nchini, inaweza kukuza soko la wakulima kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na bidhaa hii kuzidi kupata watumiaji kadiri siku zinavyokwenda.’’ Alisema.
Meneja Uendeshaji wa kampuni ya uzalishaji wa mvinyo ya Alko Vintages ya jijini Dodoma, Sweetbertha Rwabizi (kulia) akimuhudia mmoja wa  wageni waliojitokeza kufurahia pamoja siku ya wapendanao yaani Valentine Day katika hafla maalum inayofahamika kama ‘Mkeka na Mvinyo’ iliyofanyika katika hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Pamoja na agenda nyingine hafla hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya mvinyo unaozalishwa hapa nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...