Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WASANII mbalimbali nchini wamejitokeza kwa wingi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalim Nyerere jijini Dar es Salaam ambako kunafanyika Kongamano linalohusu elimu ya athari za dawa za kulevya.

Kongamano hilo limeandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo kabla ya kuanza rasmi kwa kongamano hilo wasanii wa fani mbalimbali waliendelea kutoa burudani kwa wageni walioko ukumbini hapo.Kwa lugha ya mjini Kongamano la dawa za kulevya linalohusu kuzungumzia athari za dawa za kulevya limenoga.

Mwanamuziki Charles Baba na Kalala Junior ni miongoni mwa wanamuziki ambao wameonesha umahiri wao wa kuimba ambapo mashairi ya wimbo wa Kuachwa ulionekana kupagawisha wageni waalikwa kiasi cha kushindwa kuficha hisia zao.

Charles Baba wakati anaanza kuimba aliamua kutoa burudani ya vichekesho alivyokuwa anafanya lakini alipoamua kuimba shangwe zililipuka ukumbini hapo.

Moja ya eneo ambalo liliwafurahisha walioko ukumbini hapo ni pale alipokuwa anaimba hivi "Kuacha kuachwa ...kuachwa ni shughuli pevu...mbaya zaidi kwa yule uliyempenda...wewe unakonda...yeye ananenepa kwa mawazo..."

Hata hivyo katika kunogesha wimbo huo Charles Baba akasema "Ukitaka kufaidi mapenzi ni vema ukampata mwanamke anayedaiwa kodi ya nyumba." Waliokuwa ukumbini kicheko cha nguvu.

Mbali ya Charles Baba na Kalala kutoa burudani ,wasanii wengine wakiwamo wa mashairi na ngoma za asili walitumia fursa hiyo kuonesha umahiri wao.

Wakati huo huo wanamuziki wa nyimbo za Injili nao hawakuwa nyuma kutokana na kutumia nafasi hiyo kuimba nyimbo za Injili ambazo zilikuwa zinavuta hisia za walio wengi hasa wenye imani ya dini ya Kikristo.Hata hivyo kila msanii alikuwa anatoa ujumbe unaozuia matumizi ya dawa za kulevya.

Mwanamuziki Stara Thomas aliamua kuimba wimbo unaozungumzia athari za dawa za kulevya ambapo kiitikio cha wimbo huo ulisema wasanii bila ya dawa za kulevya inawezekana.Kongamano hilo ndio kwanza limeanza na Michuzi Blog itaendelea kukujuza kila kinachoendelea ukumbini hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...