Benki ya Exim leo imezindua Kituo chake maalum kwa ajili ya kutoa huduma za kubadilisha fedha za Kigeni (Bureau de Change) katika soko la Karikakoo jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kusogeza huduma zake zaidi kwa wateja.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kituo hicho, Mkuu wa huduma ya rejareja wa benki ya Exim, Bw. Andrew Lyimo alisema uamuzi wa kufungua kituo hicho kinachohamishika umekuja kufuatia ongezeko la mahitaji ya sasa ya wateja wanaotafuta huduma za uhakika za fedha za kigeni hususani katika eneo hilo ambalo ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika mashariki na Kati.

"Benki ya Exim imekuwa ikihudumia wateja wengi sana kupitia tawi letu lililopo hapa Karikakoo na uamuzi wa kufungua huduma hii kubadilisha fedha za kigeni imekuja baada ya kugundua kuwa kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma hii na hivyo tumeamua kuchukua hatua mapema ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu,’’ alisema.

Aliongeza kuwa jukumu la benki hiyo litabaki katika kuwezesha jumuiya ya wafanyabiashara kukuza biashara zao huku benki hiyo ikiwasogezea huduma kwa ukaribu zaidi.

“Tunaamini kuwa kupitia kituo chetu hiki kinachohamishika, jumuiya ya wabiashara Kariakoo, itafurahia huduma zetu kwa kuwa wataweza kuuza na kununua fedha za kigeni papo hapo bila gharama yoyote.’’ Alibainisha.

Lyimo alisema kuwa huduma hiyo inaifanya benki hiyo izidi kuimarisha uwezo wake wa kutoa huduma na inadhihirisha kujitoa kwake kwa wafanyabiashara hasa wa kati na wadogo katika jiji la Dar es Salaam na kitaifa kwa ujumla.

“Inafahamika kuwa Kariakoo ni eneo la biashara na ni kitovu cha waagizaji, wafanyabiashara na wasambazaji ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji huu wa uchumi. Benki ya Exim inawahakikishia viwango vya ushindani kwenye soko na ndio maana tunawakaribisha waweze kufurahia huduma za fedha za kigeni kwenye kituo chetu cha hapa Kariakoo na kwenye mtandao wetu mkubwa wa matawi thelathini na mbili. "Aliongeza.

"Ikiwa ni benki ya tano kwa ukubwa hapa nchini na benki ya kwanza ya Tanzania kufungua matawi yake katika visiwa vya Comoros, Djibouti na Uganda, tunasimamia ahadi yetu ya kuboresha mazingira rafiki ya upatikanaji wa huduma za kifedha hapa nchini. Tunaamini kituo hiki kitasaidia kutoa ushirikiano wa muda mrefu na wa manufaa kati ya Exim Bank na wafanyabiashara wa wadogo na wa kati hapa nchini,’’ alihitimisha.
 Baadhi ya wafanyabiashara eneo la Kariakoo wakiingia kwenye kituo kipya  kinachohamishika cha huduma za kubadilisha fedha za Kigeni (Bureau de Change) cha Benki ya Exim katika soko la Karikakoo jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kusogeza huduma zake zaidi kwa wateja. 
Baadhi ya wateja benki ya Exim eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam wakipata huduma ya kifedha kwenye kituo kipya cha kubadilisha fedha za Kigeni (Bureau de Change) kinachohamishika cha cha Benki ya Exim katika soko hilo ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo wa kusogeza huduma zake zaidi kwa wateja. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...