MRAKIBU Mwandamizi wa Polisi, SSP Gerald Ngiichi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliamuru askari kupiga risasi hewani kwa ajili ya kusambaratisha maandamano ya viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Baada ya kuona njia ya kutumia mabomu ya Moshi imeshindikana kuwatanya.

Amedai baada ya kuamuru risasi zipigwe hewani na utekelezaji kufanyika, kulitokea sauti kubwa ambayo ilifanya waandamanaji wakiongozwa na Mwenyekiti  wa chama hicho, Freeman Mbowe kukimbia ambapo amesema  hakujua kama Mbowe alikuwa na mbio kiasi kile.

Amedai, baada ya waandamanaji kusambaratika, alifanya tathmini na kubaini kuna majeruhi wawili ambapo alikuwepo Akwilina aliyewashishwa Hospitali ya Mwananyamala na baadae kuripotiwa kuwa amefariki.

Ngiichi ambae ni Ofisa Operesheni wa Kipolisi Kinondoni, na shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka katika kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo tisa wa chama hicho amedai hayo leo Aprili 17,2019 alipokuwa akitoa ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, shahidi huyo amedai Februari 16, mwaka jana wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Kinondoni,  kulikuwa na mikutano mikubwa mitatu ya Chama cha Wananchi (CUF) iliyofanyika viwanja vya Vegas Makumbusho, mkutano wa Chadema ulifanyika viwanja vya Buibui Mwananyamala na mkutano wa CCM Uliofanyika viwanja vya Biafra Kinondoni.

Amedai, akiwa kama kiongozi, alihakikisha kila mkutano unakuwa na ulinzi wa kutosha huku wakisimamiwa, lakini viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwaongoza wafuasi wao kuandamana kutoka kwenye viwanja vya kampeni kwenda kwenye ofisi za Mkurugenzi wa Kinondoni ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi.

Amedai, katika mikutano hiyo kila mkutano alipangwa ofisa wa kusimamia mikutano hiyo ya kampeni pamoja na askari wa kutosha ambapo mkutano wa Chadema ulisimamiwa na SSP Dotto, mkutano wa CUF ulisimamiwa na SP Batseba na wa CCM ulisimamiwa na SP Magai.  Lakini kati ya saa 11:30 kwenda saa 12 jioni alipokea taarifa kutoka kwa Dotto kuwa kwenye mkutano wa Chadema kuna dalili za kuwepo kwa uvunjifu wa amani kwa sababu viongozi wanaopanda jukwaani na kuhamasisha chuki na uvunjifu wa amani kwa wananchi.

Amedai, alimuelekeza ofisa huyo kusimamia kwa weredi mkutano huo na kuelekeza askari kuchukua kumbukumbu ya vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na ndipo Baada ya muda mfupi alipigiwa simu na SSP Dotto na kumueleza kuwa viongozi wa Chadema wanahamasisha wananchi kuondoka kwenye mkutano na kwenda kwa Mkurugenzi wa Kinondoni.

Ameongeza, alimwambia SSP Dotto awaonye viongozi hao kwamba kinachoendelea ni mkutano na sio kuondoka kwenda kwenye eneo lingine kwa sababu hawajajipanga kwa ajali ya hilo na kwenda kwenye ofisi za serikali wakati  zimefungwa, haikuwa sahihi lakini walikataa na kuhamasishana kuondoka kwenda barabarani 

Kufuatia hali hiyo niliagiza askari wengine ikiwemo kutoka vikosi vya doria, magari, pikipiki na wa usalama barabarani kwenda kwenye makutano ya barabara ya Kawawa na Mwananyamala kwa ajili ya kuzuia maandamano hayo ambapo Mbowe na wenzake walikaidi amri iliyotolewa kitu kilichomfanya yeye mwenyewe kuamua kwenda eneo la tukio na kwamba alipofika alikuta watu wengi zaidi ya 600 wakiingia barabarani wakiwa wamevalia sare na magwanda ya Chadema huku wakiimba kwamba ‘hatupoi, hatutishwi ‘ wakionekana kuwa na jazba  mawe, chupa za soda, maji na fimbo.

Amedai baada ya kuona hali hiyo, alimuamuru dereva wake awashe king’ora na honi ili wapite kwenye barabara ya mwendokasi na walifanikiwa kufanya hivyo lakini waandamanaji walipoona kuwa ni gari la polisi waliendelea kusogea mbele hivyo alitoa ilani mara tatu ya kuwataka kutawanyika lakini walikataa kutii amri.

‘’Ilani ilani ilani mimi SSP Gerald Ngiichi kwa jina la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkusanyiko huu ambao sio halali mliokusanyika hapa nawaamuru mtawanyike mara moja vinginevyo nguvu itatumika kuwatawanya,’’ alidai kutoa ilani hiyo kwa kutumia kipaza sauti cha kwenye gari analotumia huku akiendelea mbele.

Amedai kufuatia kugoma kutawanyika, pamoja na kutoa ilani hiyo, aliamuru askari waliokuwa na mabomu ya moshi kupiga mabomu hayo lakini hakukuwa na muitikio wa kutawanyika kwa waandamanaji kwa sababu mabomu yaliathiriwa na upepo hivyo moshi ulikuwa ukirudi upande wa askari kitendo kilichopelekea waandamanaji hao kuwarushia mawe na kusababisha kujeruhiwa askari wawili ambao ni PC Fikiri na Koplo Rahim ambao walianguka chini hivyo aliomba askari kutoa msaada kwao.

‘’Baada ya kuona hali hii, niliamuru vikosi vya mabomu kurudi nyuma na vikosi vyenye risasi za moto kusonga mbele kwa ajili ya kupiga risasi hewani ambapo baada ya kupigwa kwa risasi hizo, kulitokea kishindo kikubwa na niliona waandamanaji wakitawanyika ikiwemo Mbowe akikimbia, sikuamini kama alikuwa na mbio kiasi kile,’’ amedai SSP Ngiichi.

Pia alidai baada ya kutawanyika kwa watu hao, walifanikiwa kuwakamata wafuasi 43 na kuwapeleka kituo cha Polisi Oysterbay kwa ajili ya kuwafungulia kesi ya kufanya maandamano isivyohalali.


Mbali ya Mbowe washitakiwa wengine ni Katibu Mkuu Taifa, Dk Vincent Mashinji ,  Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika,  Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji,  Mbunge wa Kawe,  Halima Mdee,  Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda,  Ester Bulaya.

Kesi hiyo itaendelea Mwezi ujao kwa Siku tatu mfululizo. Mei 13, 14 na 15

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...