aziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akitazama mtoto Ahmed Said akiwekewa vifaa vya usikivu toka kwa Dkt. Tani Austin wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Masuala ya Masikio na Usikivu leo Jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akifuatilia mtaalam akifunga vifaa vya usikivu kwa mtoto Monica Denis kabla ya kuzindua Mpango Mkakati wa Taifa wa Masuala ya Masikio na Usikivu Jijini Dodoma.

“Furaha ilioje kusikia tena” Picha ya pamoja Bibi Tausi Mbonde na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Starkey Hearing Foundation na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kabla ya kuzindua Mpango Mkakati wa Masuala ya Masikio na Usikivu leo Jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kutoka kushoto) akizindua rasmi Mpango Mkakati wa Masuala ya Masikio na Usikivu akiwa pamoja na Bwana na Bibi Bill Austin (waliovaa makoti meupe) kutoka Taasisi ya Starkey Hearing Foundation, kushoto ni Dkt. Grace Maghembe Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya na Daktari Bingwa wa Masikio na Usikivu Dkt Edwin Liyombo (wa pili kutoka kulia)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akifafanua jambo kutoka kwenye kitabu cha Mpango Mkakati wa Masuala ya Masikio na Usikivu leo Jijini kabla ya kuzindua mpango huo
Dkt. Bill Austin (kulia) kutoka Taasisi ya Starkey Hearing Foundation akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Masuala ya Masikio na Usikivu leo Jijini Dodoma aliye kushoto ni mke wake Dkt. Tani Austin.
…………………

NA WAJMW-DODOMA
Imeelezwa kuwa vijiti na pamba za kusafisha masikio zinasababisha kwa kiasi kikubwa magonjwa ya usikivu yanayopelekea kuwa kiziwi.
Hayo yamebainika leo wakati wataalamu wa afya ya masikio na usikivu kutoka taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Healing Care walipomweleza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea mabanda ya utoaji wa huduma za masikio na usikivu kwa wananchi mbalimbali jijini Dodoma.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Ummy amewataka wananchi kulinda masikio yao kwa kufuata ushauri wa madaktari na kuacha tabia ya kutumia vifaa vinavyosababisha matatizo ya usikivu kama spika za masikioni na matumizi ya pamba za kutolea uchafu.

“Tatizo la usikivu ni kubwa katika nchi yetu, katika tafiti ndogo ndogo ambazo zimefanyika zinaonesha asilimia 3 ya wanafunzi ambao wako shuleni wana matatizo ya usikivu kwa kiwango fulani lakini pia takwimu zinaonesha kuwa kila watu 100 wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza, 24 kati yao wanakua na matatizo ya usikivu”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri ummy amesema tafiti zinaonesha pia waathirika wengine wenye matatizo ya usikivu ni wale wanaofanya kazi katika migodi na viwandani hasa viwanda vya nguo ambapo takwimu zinaonyesha asilimia 50 wanakua na matatizo hayo.

Waziri Ummy ameishukuru taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Healing Care kwa kutoa huduma za masikio na usikivu nchini huku akisema Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha miundombinu, kununua vifaa na kuongeza wataalamu wa huduma za masikio na usikivu, kutoka wataalamu bingwa 11 mwaka 2009 mpaka kufikia wataalamu 46 mwaka 2018.

Hata hivyo Waziri Ummy amesema toka kuanzishwa kwa huduma hizi nchini kumesaidia kuokoa kupunguza idadi ya watoto kupelekwa India, ambapo kila mwaka takribani watoto 13 walikua wanapelekwa India kupata matibabu na mtoto mmoja alikua anagharimu Tsh. Milioni 80 mpaka Milioni 100. Lakini kuanzishwa kwa huduma hizi katika Hospitali ya Muhimbili mwaka 2017, watoto takribani 26 wamepata huduma kwa gharama ya Tsh. Milioni 35 na kuokoa fedha za Serikali kwa zaidi ya asilimia 60.


Kwa upande wake muanzilishi wa taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Healing Care Dkt. Bill Austin ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma na vifaa vya masikio na usikivu kwa wananchi ambapo ilianza kutoa huduma hizo Jijini Mwanza na kuendelea kutoa huduma Jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...