Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara akizindua mojawapo kati ya madarasa manne ya elimu ya awali kati ya madarasa 30 yanayojengwa katika wilaya za Misungwi na Ukerewe mkoani Mwanza. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Magaka, wilayani Misungwi jana. 
Mkurugenzi Mkazi wa shirika la kimataifa la Children in Crossfire bwana Craig Ferla ambaye aliwezesha kukamilika kujengwa kwa madarasa 4 kati ya 30 yanayojengwa mkoani Mwanza akizungumza kabla ya Naibu Waziri kuzindua mojawapo ya madarasa hayo katika kijiji cha Magaka jana. 
Picha za nje na ndani kuonyesha mandhari ya madarasa yanayojengwa kwa ushirikiano baina ya shirika la Children in Crossfire na Serikali kama linavyoonekana. Jumla ya Madarasa 100 ya aina hii yatajengwa katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dodoma 

………………………….. 

Na Mathew Kwembe, Mwanza 

Serikali imelipongeza shirika lisilo la kiserikali la children in Crossfire kwa mkakati wake wa kujenga madarasa ya elimu ya awali 100 katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ijayo. 
Pongezi hizo zimetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara katika kijiji cha Magaka, wilayani Misungwi wakati akizindua mojawapo kati ya madarasa manne ya elimu ya awali kati ya madarasa 30 yanayojengwa katika wilaya za Misungwi na Ukerewe mkoani Mwanza. 

Mhe.Waitara amesema kuwa kujengwa kwa madarasa hayo ya awali kutachochea ari ya watoto wanaojiunga na elimu ya awali kupenda kusoma na hivyo kupunguza utoro katika maeneo yanakojengwa madarasa hayo. 
Mhe.Waitara ameongeza kuwa kama madarasa yenyewe yanayojengwa ni kama hayo aliyozindua anatumaini kuwa mikoa ya Mwanza, Morogoro, na Dodoma itakuja kuongoza kitaaluma katika miaka ijayo.
 
“Kama madarasa yenyewe ni yale tunaamini mikoa ya Mwanza katika wilaya za Misungwi na Ukerewe, pamoja na mikoa ya Dodoma na Morogoro inapaswa kuja kuongoza kwa taaluma ambayo wanaipata, na tunaamini kuwa watoto wataokuja kusoma katika madarasa haya watakuwa na uwezo mkubwa wa kimasomo,” amesema. 

Amesema madarasa hayo ni ya mfano kwani siyo tu yanaongea, bali pia yanacheka na kutabasamu kwani kona zote za madarasa hayo zimesheheni zana mbalimbali za kujifunzia zinazomuwezesha mtoto siyo tu ajifunze kwa urahisi bali pia apende shule kutokana na kuwa na rangi za kuvutia. 
“Hili darasa kama mlivyoona, nimekutana na madarasa yanayoongea lakini hili darasa linaongea, kutikisika na kucheka, na tabasamu linaongezeka,” amesema na kuongeza: 

“Sasa nilikuwa napiga picha ya madarasa yanayoongea ambayo niliwahi kuonyeshwa pamoja na haya hapa, hongereni sana haya yametia fora.” 
Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa sera ya mafunzo ya elimu ya mwaka 2014, Naibu Waziri amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la watoto wanaojiunga na elimu ya awali kutoka milioni moja mwaka 2015 hadi watoto milioni moja na nusu mwaka 2016. 
Aidha Mhe.Waitara ameziagiza halmashauri kuhakikisha kuwa kila zinapojenga shule za msingi pia zinapaswa kuweka bajeti kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya awali. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa shirika la kimataifa la Children in Crossfire bwana Craig Ferla amesema kuwa shirika hilo katika kipindi cha miaka mitano ijayo limepanga kutumia shilingi milioni mia 700 kwa ajili ya kujenga madarasa 100 ya aina hiyo katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dodoma. 

Naye Mratibu wa mafunzo ya elimu ya awali kutoka shirika hilo bwana Davis Gisuka amesema kuwa mbali na kujenga madarasa hayo pia shirika lake linawezesha kufanyika kwa mafunzo maalum kwa walimu wa shule za awali za serikali ili waweze kumudu kuwapatia elimu watoto wanaowafundisha kupitia mbinu mbalimbali za mafunzo ikiwemo matumizi ya zana rahisi za kufundishia zinazotengenezwa na walimu hao katika shule zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...