Na Moshy Kiyungi,Dar es Salaam


Dekula Kahanga ameweza kuyasaka mafanikio hadi kuunda bendi yake anayojulikana kama Dekula band akiwa katika jiji la Stockholm nchini Sweden.

Kabla ya kwenda nchini humo Kahanga alikuwa mpigaji wa gitaa la solo katika bendi ya Maquis Original, iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata, Kindondoni jijini Dar es Salaam, miaka ya 1990.

Dekula ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Vumbi’, aliwahi kutamka kwamba mafanikio yoyote katika maisha ni lazima mtu kuwa na malengo, na dhamira ya dhati, hatimaye kufanya maamuzi magumu.

Alisema baadhi ya maamuzi magumu aliyoyafanya mojawapo ni lile la kondoka katika bendi hiyo ya Maquis Original, na kutokomea kwenda Sweden bila kujua atakuwa mgeni wa nani huko Ughaibuni.

Vumbi alieleza kwamba hivi sasa hajutii maamuzi yake kwakuwa yamempata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kumiliki bendi yake.

Amesema bendi hiyo hupiga muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa Lala Vin, mjini Stockholm nchini Sweden.

Dekula Band ina wanamuziki mahiri toka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo akina Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ ambaye ni mwimbaji na kunengua, Sammy Kasule, ambaye ni injinia pia huimba, kupiga gita la besi, drums na kinanda.

Wengine amewataja kuwa ni Joe Gerald Nnaddibanga, ambaye huimba, kupiga konga na kucheza show, Christina Frank, na Marceline Kouakoua.

Mwenyewe Dekula Kahanga, hulicharaza gitaa la solo na rhythm pamoja na Arne Winald ambae hubofya kinanda.

Safu hiyo kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika kimataifa hadi kupelekea kupata mialiko lukuki ndani na nje ya Sweden zikiwemo nchi za Ulaya, Asia, Marekani, Japan, Falme za kiarabu na Afrika.

“ Hakuna kitu muhimu kama kuwa na mahusiano mema na baadhi ya watu toka nchi mbalimbali ninazotembelea. Nimefikia kuweza kuongea kwa ufasaha lugha tano tofauti za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Lingala na Kiswidish” Anajigamba Dekula ‘Vumbi’.

Historia ya Dekula Kahanga anailezea kwamba alizaliwa mwezi Aprili 02, 1962 katika kijiji cha Lumera, Wilaya ya Kivu Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ni baba wa familia akiwa na mke na watoto watatu. Dekula ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kadhaa wa Mzee Aloyce Obeid Dekula, aliyekuwa mfanyakazi katika serikali ya Zaire iliyokuwa ikiongozwa na rais Mobutu Seseseko.

Alipata elimu ya Sekondari katika shule mbili tofauti za Bukavu na Uvira huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alihitimu kidato cha nne mwaka 1979. Mwaka uliofuatia wa 1980, safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National, na Grand Mike jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa Nundu.

Akiwa huko kwao wilaya ya Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo ilikuwa ikisikika wakati huo na alizitamani sana nyimbo zilizokuwa zikiporomoshwa na bendi za Morogoro Jazz, Jamhuri Jazz, Tabora Jazz, Nyamnyembe Jazz, NUTA Jazz, Mlimani Park, Maquis du Zaire na Orchestra Safari Sound.

Kamwe hatomsahau John Luanda katika historia ya maisha yake, huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha yeye kuingia hapa Tanzania.

Luanda licha ya kuwa mtangazaji wa RTD, alikuwa akimiliki bendi ya Chamwino Jazz.

Aliwachukua toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akiwa na wenzake akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga na Baposta kwa madhumuni ya kuimariisha bendi yake ya Chamwino.

Bendi hiyo wakati huo ilikuwa ikipiga muziki maeneo ya Tandale huko Manzese, jijini Dar es Salaam.

‘Vumbi’, mwaka 1980 alikutana na mwanamuziki Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Viking’ katika ofisi za ubalozi wa Kongo hapa nchini.

Nguza wakati huo alikuwa mpiga gita la solo pia alikuwa ni mmoja kati ya wanahisa wa Orchestra Maquis Comapy (OMACO) na mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Orchestra Maquis du Zaire. Katika maongezi yao, Chimbwiza Nguza alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda kuburudisha kwenye ukumbi wa White House, uliokuwa maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Dekula alikubali mwaliko huo na Weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha kwa muda mfupi.

Walipopanda jukwaani waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi wa muziki waliokuwa wamefurika ukumbini humo pamoja na wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.

Dekula Kahanga baadaye aliitwa na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu Katai ‘Mzee Paul’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’ wakimtaka aandike barua ya kuomba kujiunga na bendi yao kwa mkataba usio na mshahara. Alitakiwa na bendi hiyo ili kuziba nafasi ya Nguza ambaye alikuwa tayari ameanza mgomo baridi. Vumbi alikubali na akajiunga na Maquis du Zaire.

Vumbi anaikumbuka siku mmoja wakipiga muziki katika ukumbi wa Temeke Stereo, alimuona Nguza akiwa amejibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo huku akisikiliza midundo inavyounguruma..

“Nilipomuona, nikaingiwa na hofu kubwa nikijihisi kama ninamvunjia heshima Nguza. Nikaomba nimpishe ili ashike nafasi yake” Anasema kwa kujiamini Dekula Kahanga.

Lakini viongozi wake akiwemo Chibangu Katai ‘Mzee Paul’ na Ilunga Lubaba, walimwamuru aendelee kushika ‘mpini’.

Kwa amri hiyo, ilikuwa kama Fisi aliyeachiwa Bucha kuilinda. Aliweza kuzicharaza kwa umahiri mkubwa nyimbo zote alizokuwa zikipigwa Field Marshal Nguza zikiwemo za Makumbele, Ngalula Seya Malokelee, Karubandika, Mage, Dora mtoto wa Dodoma, Clara, Mwana yoka ya Babote, Nimepigwa ngwala na nyingine nyingi pasipo kutofautisha kati yake na Nguza.

Aliachiwa kulivurumisha gitaa hadi mwisho wa onyesho hata mpiga solo Ilunga Lubaba hakutaka kuligusa siku hiyo. Baada ya hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipo naye hakusita kumpa hogera kwa kazi nzuri.

“Mungu mkubwa, siku hiyo Nyota yangu iling’ara kiasi kwamba hata mimi mwenyewe sikuweza kuamini nilichokuwa nikikifanya jukwaani hapo” Anasema Dekula Kahanga ‘Vumbi’ huku akitabasamu.

Baadhi ya nyimbo lizoweza kupiga gitaa ni katika nyimbo za Makumbele, Ngalula Seya Malokelee, Karubandika, Mage, Dora mtoto wa Dodoma, Clara, Mwana yoka ya Babote, Nimepigwa ngwala na nyingine nyingi pasipo kutofautisha kati yake na Nguza.

Kabla ya hapo gitaa hilo lilikuwa licharazwa na Nguza Vicking.

Baadae bendi hiyo ilisambaratika na kuzinduliwa upya ikiwa na majina ya Maquis Original. Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake katika kumbi za Wapi Wapi’s Bar pale Chang’ombe, Temeka Kata ya 14 kabla ya kuweka makao yake makuu katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazoezi makali katika bendi hiyo, Oktoba 10, 1989 walirekodi nyimbo za Mashoga, Tipwatipwa, Hali Ngumu, Ossa, Marusu, Mangolibo, Kisebengo na zingine nyingi zote hizo akilicharaza gitaa la solo.

Wakati huohuo Maquis Original aliwapata wanamuziki wengine watatu toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwamo waimbaji Bobo Sukari, Fred Butamu na mcharazaji gitaa la solo Kivugutu Moto na Chacho.

Vumbi wakati huo alikuwa na umri ambao unamruhusu kuhangaika kutafuta maisha yenye maslahi mazuri. Hivyo maamuzi magumu yakaanzia hapo Lang’ata baada ya kuamua kuicha bendi ya Maquis Original, iliyompa jina na kuchepukia katika jiji la Stockholm nchini Sweden.

Kabla haja Akiwa Stockholm, Vumbi alianza kuchacharika mitaani akitafuta bendi ya kupiga, hatimaye akakutana na mwanamuzi toka Uganda, aitwaye Sammy Kasule. Mwaka 1993 wakaamua kuanzisha bendi yao ikiitwa Makonde Group.

Mwaka 1999, Dekula Kahanga alifyatua Album iitwayo Bolingo Ekesemi iliyosheheni nyimbo za ‘Dunia kuna mambo’ na ‘mpenzi Asha’

Dekula Kahanga anajivunia kwamba yeye ni mwanamuziki wa kwanza toka Afrika huko Sweden, kufyatua album. Alitoa album iitwayo ‘Dekula Sultan Qaboos’ yenye nyimbo za Sultan Qaboos, Mon Amour, Babylon, Mayanga, Rozina, Mambo leo na Nostalgie nyimbo hizo anasema zinazopigwa mno katika vituo vingi vya redio Duniani.

Ili kupata unafuu wa maisha nchini Sweden, Dekula alilazimika kuomba uraia wa nchi hiyo hivyo ilifuata taratibu zote.

Alichukua maamuzi magumu mengine ya kuukana uraia wa nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kupata uraia wa nchi hiyo.

Hivi sasa yeye na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo ni raia halali wa nchi ya Sweden na wanaweza kusafiri kwenda nchi za Marekani Ulaya Asia na kwingineko pasipo kuomba VISA.

Dekula ametoa mwito kwa wanamuziki chipukizi kujifunza kupiga ala za muziki ili wafikie viwango vya kuwa wanamuziki. Pia amewaasa kuacha kulewa sifa ndondogo pia kuepuka anasa zisizo na tija.

“Nawapenda sana Watanzania, walinipokea, wakanilea, wakanithamini na wakanipenda…” alisema Dekula.

Aidha alisema kuwa anatarajia kutoa zawadi endelevu kwa Watanzania siku za usoni kuanzisha bendi ya vijana, itakayokuwa ikitumia ala za muziki wa kisasa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...