Na Moshy Kiyungi,Tabora.


Mafanikio yoyote ya mwanaadamu hupatikana baada ya kukabiliana na changamoto nyingi, ambazo wengine hushindwa kuvumilia wakaishia kukata tamaa.

Rashidi Pembe ni mmoja kati ya watu waliokumbana na matatizo mengi, likiwemo la kufanya kazi ya ukuli maeneo ya Manzese, jijini Dar es Salaam.

“Kaka usinione hivi, mimi nimebeba mizigo ya abiria wanaotoka Mbeya na mikoa mbalimbali pale Manzese, hadi nikateguka shingo, jamani maisha ni kiboko…”

Haya ni baadhi ya maneno ya mwanamuziki huyo, wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa makala hii, nyumbani kwake Mwananyala, Dar es Saalam.

Pembe alisema hakuna silaha kubwa kwa mwanaadamu kama kutokata tama. Yeye baada ya kusota kwa kipindi kirefu, hivi sasa akiwa na wanamuziki wenzake, wanamiliki bendi yao waliyoipa jina la Orchestra Mark International.

Kufuatia muziki mzuri wa Kimataifa wanaopiga, wamewahi kupata mkataba mnono wa kupiga muziki Ughaibuni, ulioweza kuwafuta ‘jasho’ wanamuziki hao.Pembe alieleza kuwa maisha yake yalianzia baada ya kuzaliwa mwaka 1957, mkoani Pwani.

Baba yake mzee Pembe Rashid, alikuwa mzaliwa wa kijiji cha Kuruwi, tarafa ya Mzenga, wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani wakati mama yake Bi. Frida Abel, mzaliwa wa kijiji cha Mihugwe, wilayani humo. Wote walikwisha tangulia mbele za haki.

Katika mahojiano hayo Rashidi Pembe alielezea historia ya maisha yake akisema."Nilianza kusoma shule ya msingi Chanzige iliyoko Kisarawe mwaka 1963, mama alikuwa Daktari, alihamishwa kwenda kuhudumia huku na kule, nasi ndio tulikuwa tukiishi na mama kwani wakati huo alikuwa amekwisha tengana na baba.

Mama alipenda sana nisome, ila baba hakuwa na msisitizo sana wa shule, sijui kwa kuwa alikuwa mbali na sisi, maana huduma ilikuwa kwa mbinde kidogo…”.Mwaka 1966 mama yake alihamishwa toka hospitali ya Kisarawe, akapelekwa hospitali ya Vikindu, nao wakalazimika kuhama kwenda kusoma hapo Vikindu, iliyopo wilaya hiyo ya Kisarawe wakati huo akiwa darasa la Nne.

Pembe alifaulu mtihani wa kuingia darasa la tano, mwaka 1967, akaingia shule ya kati hapo Vikindu. Huko ndiko alikokutana Joseph Benard wakiwa darasa na dawati moja.Joseph Benard ni mwanamuziki anayepuliza saxophoni katika bendi Mlimani Park Orchestra.

Joseph ambaye hivi sasa anaitwa Yusuph Benard, alikuwa ni mpiga filimbi bingwa shuleni kwao. Pembe alitamani sana aweze kupuliza ala hiyo, akamua kumuomba amfundishe.Pasipo kusita Yusuph alimfundisha kupuliza filimbi wakawa wote wapiga filimbi katika bendi ya shule.

“mwana 1968 nikiwa darasa la sita niliugua, mkono ulikuwa haukunjuki sijui ilikuwa ni nini. Hospitali ya Muhimbili waliamua wauvunje, nikakataa, wakanifukuza hosptalini hapo…” alisema Pembe.

Hakutaka mkono wake kuvunjwa halafu uungwe tena, akihofia kuwa atakuwa kilema wa mkono kutokukunja tena.

Kwa mapenzi ya mungu, mkono huo ulikunjuka siku hiyohiyo jioni, baada ya kusota kwa takriban mwaka mmoja. Pembe alikuwa akiugulia kwa maumivu makali, ukiwa umevimba na kwa kipindi chote hicho, alikuwa haendi shuleni.

Mama yake Bi. Frida mwaka huohuo wa 1968, alihamishwa kupelekwa katika hospitali ya Sotele, baadaye tena akapelekwa katika hospitalia ya Kisiju.Baada ya kukosa masomo kwa mwaka mzima, mama yake alimshauri arudie tena darasa la nne, kwenye shule ya Kisiju, ambayo ilikuwa mpya haikuwa na darasa la tano na sita.

Alisema kuwa wakati akiwa mdogo, alipenda sana ngoma, ilikuwa Mdundiko ukipita, mama yake alikuwa akiwaambia dada zake wamkamate.“Walifanya hivyo kwa kuwa nilikuwa naifuata ngoma ya Mdundiko nisijue waendako, mwisho wake nikuwa napotea” alisema Pembe

“mimi sikuwa napenda shule kabisa, kwenda ilikuwa hadi kwa viboko, kila siku nilipambana na mama hadi nilipomaliza darasa la saba mwaka 1972” alisema.Rashid Pembe hakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, hivyo mama yake alimpeleka kwa mjombawe aliyekuwa akiishi Dar es Salaam, akatafute kazi.

Alifanikiwa kupata kazi katika kiwanda cha nguo cha Kilimanjaro Textile, kilichokuwa kinatengeneza Khanga na Vitenge hapo Gongolamboto jijini humo.Mara alipoanza kazi mwaka 1973, aliwekwa kitengo ambacho walikuwa wa wakishughulikia Pamba. Wakawa wanaziba pua kwa vitambaa, ili wasiathirike kutoka katika pamba wanazosindika kwenye mashine.

Pembe akiwa kazini humo, aliwashuhudia vijana wenzake wadogo, wakiwa wameshika mafaili na kuzunguka huku na kule na wengine wakiwa ofisini.
Akatamani kuwa na kazi kama ya hao vijana, ikabidi aulize mbona wale wana kazi nzuri, akajibiwa kuwa wale wamesoma hadi Kidato cha nne.

Nguli huyo akaikumbuka kauri ya mama yake akimsihi asome sana, baadaye ataiona faida yake.Rashidi Pembe akajutia ‘ujinga’ wake wa kutopenda shule, lakini kipindi hicho tayari akafahamu umuhimu wa elimu.

Akaona hakuna njia ya kujikwamua ila kwenda shule, hivyo alimuomba kaka yake amtafutie shule.Kaka yake akampeleka shule ya Ufundi ya Bagamoyo, iliyokuwa inamilikiwa na Umoja wa Wazazi (TAPA) wakati huo, hadi alipohitimu kidato cha nne mwaka 1978.

Wakati akiwa shule, Pembe aliipenda sana bendi ya Safari Trippers, iliyokuwa ikiongozwa na Marijani Rajabu, pale Princes Bar, ilikuwa Mnazimmoja jijini Dar es Salaam.Akiwa likizo alikuwa akienda kuwaangalia wanamuziki wa bendi hiyo wakifanya mazoezi.

“Mimi nilikuwa nadhani muziki mtu anajuwa kupitia kipaji alicho zaliwa nacho, wala sikufahamu kuwa ni lazima mtu ujifunze. sasa pale nilimshuhudia Abdallah Gama akipiga gitaa huku akiwa na umri mdogo sana.Hata nilipokuwa shule alikuwa tayari nilikuwa na gitaa, jambo ambalo kaka yake aliyekuwa akimsomesha, alikasirika mno akamuamuru aliuze gitaa hilo, Rashid akakataa.

Brother akanifukuza nyumbani kwake, akaamua kwenda kwa dada yake. Lakini shemeji yake naye akamtamkia kuwa hawezi kuishi na watu lukuki nyumbani kwake.Rashidi Pembe akaondoka kwa kaka yake, akawa analala nje ya soko la Kariakoo.

Kuanzia hapo ndipo aliyaona machungu ya maisha ya shida. “nilitamani kufa lakini sikuuza gitaa langu. nilikubali yote, nikaanza kubeba mizigo ya abiria wanaotoka mbeya na mikoa mbalimbali pale Manzese hadi nikateguka shingo. Jamani maisha ni kiboko…” alisema Rashidi Pembe

Alimuamini sana Mungu, akiamuomba amuondoshee yale mateso aliyokuwa akiyapata hadi amalize shule.Wakati huo Kaka yake aligoma hata kumlipia karo ya shule, baba yake akawa anamlipia.

Matokeo yalipotoka, Pembe alichaguliwa kwenda kusomea ualimu wa ufundi chuo cha Mrutunguru kilichopo mkoani Mara, akakataa kwenda huko. Baba yake naye akashikwa na ghadhabu, akamwambia hatamsaidia kamwe kwa lolote lile.

Pembe bahati ilikuwa upande wake, mwaka 1979, alienda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), akitumaini kwamba cheti chake cha ufundi Uashi grade 1, kingempatia kazi. Kumbe JKT ni kujitolea, akatoroka kabla hata namba za jeshi hazijatoka.

Baadaye Jeshi la Polisi walikuwa wanahitaji mafundi waliotoka shule, hapo ndipo cheti chake ‘kilimbeba’, akachukuliwa akawa askari Polisi kwenye bohari kuu ya jeshi hilo, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Rashidi Pembe akiwa hapo ndipo alipokutana na TX Moshi William na Kassim Mapili, ambaye akaamua kumchukuwa ili alijiendeleze kupiga gitaa.

Akaomba kubadilishwa Idara Kikosi cha Ufundi na kuingia bendi ya Polisi.

“kwakuwa nilikuwa kama mwanafunzi wa kuendelezwa, marehemu mzee Mayagilo, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Brass band, aliamua kunipa saxophone, niache gitaa.

Sababu ni kwamba kuna mpiga ala hiyo, mzee Abdul Mwalugembe aliyekuwa anakaribia kustaafu. Hivyo niliingizwa shule ya palepale na kuanza kusoma Nota na kuanza kujifunza saxophone mwaka 1981….” alisema Pembe.

Mwaka 1985 alichaguliwa kwenda kufanya kozi ya cheo cha Coplo huko Zanzibar, ambako alifanya vyema akaweza kutunikiwa cheo cha Coplo.

Pamoja na kupata kazi hiyo ya Polisi, yeye hakuwa akiipenda kazi hiyo, lakini jeshi hilo ndilo limenifikisha hapa alipo, hususan kwa masomo ya muziki ambayo yamenifanya kuwa mwanamuziki kamili.

Aprili 1987 Rashidi Pembe ‘aliitosa’ kazi ya Polisi, akaamua kujiunga na bendi ya Vijana Jazz, ambako alipiga muziki hadi mwaka 2005, alipoamua kuacha.Nguli huyo akachukuliwa na Samba Mapangala, mwanamuziki toka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kwenda katika ziara zake za Afrika.

Pembe alipofika mwaka 2006, alimuomba Mapangala aachane naye, akakubaliwa.Alifikia uamuzi huo baada ya kujikuta alikuwa tayari ameutumikia muziki kwa takriban miaka 26, hakuyaona mafanikio yeyote.

Wakati huo kuna baadhi ya wanamuziki waliokuwa wameunda bendi ya Orchestra Mark International, iliyoanzishwa kwa ajili ya kupiga muziki katika hoteli mbalimbali.Pembe akaungana nao, wakaanza kupiga muziki karibia hoteli zote kubwa jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo ya Orchestra Mark International, iliwahi kupata mkataba mnono, uliowapeleka nchi nyingi za Ulaya, zikiwemo za Ujerumani, Misri, Ufaransa na Sweden, ambako walikuwa wakipiga muziki kwa mkataba katika Meli ya Kitalii katika jiji la Stockholm.

Rashidi Pembe hadi sasa anakula ‘bata’ , katika bendi hiyo ambayo wakati wowote alisema itakwenda Ughaibuni kupiga muziki kwa mkataba wa kueleweka.Gwiji huyo alitamka kuwa amekumbana na changamoto nyingi alizokumbana nazo.

“maisha ya muziki ni magumu sana hasa kutokana na mpangilio wa haki za muziki na wanamuziki wa Afrika ni tatizo kubwa ambalo hakuna udhibiti, kitu ambacho ni kigumu kwa maisha yetu sisi wanamuziki…” alisema Pembe.

Kila la heri, songa mbele licha ya changamoto utakazo kumbana nazo. Usiache kukiendeleza kipaji cha muziki alichonacho binti yako.

Mwisho.

Mwandishi wa makala anapatikana kwa namba: 0713331200, 0767331200, 0784331200 na 0736331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...