Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

MCHUNGUZI Mkuu Wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyita( 44), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya sh. Milioni 200

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali Mkuu Paul Kadushi amedai mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa, Februari 9, 2019 huko Upanga, mshtakiwa Batanyika, alishawishi na kuomba rushwa ya Sh. Milioni 200 kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham kwa lengo la kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi inayomkabili Hasham, wakati akijua kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea katika Ofisi ya Takukuru.

Imeendelea kudaiwa kuwa, Februari 10, 2019 katika eneo la Sabasaba, mshtakiwa Batanyita alipokea USD 20,000 kutoka Faizal Hasham ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hussein Hasham.

Pia, February 13, 2019, katika ofisi ndogo za Takukuru zilizopo Masaki, mshtakiwa alishawishi rushwa ya USD 50,000 kutoka kwa Thangvelu Vall, ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya kukwepa kodi inayomkabili Vall.

Katika shtaka la nne, Februari 14, 2019 katika barabara ya Haile Selasie karibu na Merry Brown, mshtakiwa alishawishi rushwa ya USD 20,000 kutoka kwa Thangvelu Vall, kama ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya kukwepa kodi inayomkabili Vall, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.

Aidha Februari 10, 2019, mshtakiwa Batanyita anadaiwa kutakatisha USD 20,000 kutoka kwa Hasham, wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la rushwa.

Pia imedai, Februari 19 2019, katika duka la kubadilishia fedha la Village Super Market huko Oysterbay, mshtakiwa kwa lengo la kuficha chanzo cha fedha USD 7000, alizopewa, alibadilisha fedha hizo na kupata fedha za kitanzania kiasi cha Sh milioni 16 wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao La kosa tangulizi la kosa la kuomba rushwa.

Katika shtaka la mwisho imedaiwa, Februari 19, 2019 eneo la Chamazi, mshtakiwa alitumia fedha alizopewa kwa njia ya rushwa, kununulia kiwanja eneo la Chamazi, kwa gharama ya Sh15,8000,000, wakati akijua fedha hizo ni zao tangulizi la kosa la kuomba rushwa.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.Kwa mujibu Wa upande mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado unaendela na mshtakiwa amerudishwa rumande. Hadi Agosti 23, 2019 kesi hiyo itakapotajwa tena.
 MCHUNGUZI Mkuu Wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyita( 44), akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya sh. Milioni 200


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...