Na Said Mwishehe,Michuzi TV

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu nchini Tanzania, Benjamin Mkapa ametuma ujumbe mzito kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa kuzitaka ziweke mfumo mzuri wa kuwasilisha michango kwa wakati kwa ajili ya jumuiya hiyo ili ziweze kutekelezeka majukumu yao kikamilifu huku akisema ni lazima zijitegemee badala ya kuwa tegemezi.

Hayo ameyasema leo Agosti 15,2019 akiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alikuwa anaongoza Mhadhara wa wazi ambao limeandaliwa na Taasisi ya Uongozi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)pamoja na SADC kwa ajili ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya Jumuiya.

Hivyo wakati anazungumza kwenye mhadhara huo uliohudhuria na watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi,wasomi, sekta binafsi, viongozi wastaafu na wanafunzi wa vyuo vikuu Mkapa amesema ili Jumuiya hiyo iweze kutekeleza vema majukumu yake iko haja kwa nchi wanachama kutoa michango waliyojiwekea kwa wakati.

Pia amesema katika nchi za SADC na Afrika kwa ujumla kuna rasilimali za kutosha na za kila aina, hivyo haoni sababu ya nchi hizo kuendelea kutegemea msaada kutoka kwa wahisani katika kutekeleza baadhi ya majukumu yake.

"Malengo na matarajio ya SADC ni kufanya mapinduzi ya kila sekta ili kuchochea uchumi wa nchi na wananchi pamoja na kusimamia amani ya nchi na kanda kwa ujumla.Iwapo kutakuwa na mikakati inayotekelezeka na inayoakisi malengo na matarajio ya SADC nchi wanachama zitaacha kuwa tegemezi.Kwa miaka 14 ambayo nimekuwa nje ya SADC kimaamu bado naona changamoto ni zilezile za siku nyuma hazijapata ufumbuzi,"amesema Mkapa.

Amefafanua kuna changamoto kubwa ya soko la nje, umaskini, ubora hafifu wa bidhaa, teknolojia na miundombinu duni, hivyo ni jukumu la Jumuiya hiyo kuweka mikakati ya kutafuta changamoto hizo huku akibainisha SADC ina historia ndefu kwa nchi za Kusini hasa kisiasa, kiuchumi na kijamii lakini bado haijagusa jamii kwa upana wake na hivyo lazima ni wabadilike.

Wakati huo huo amesema pamoja na mipango iliyopo juhudi zinahitajika katika kuwekeza kwa vijana na teknolojia ili kwenda na kasi ya dunia."Teknolojia imewehukua nafasi kubwa kwenye sekta ya viwanda hivyo hakuna sababu ya kubakia katika mifumo ya kizamani,"

Akizungumzia elimu kwa vijana wa Jumuiya hiyo amesema elimu inasaidia kichochea ubunifu na ujuzi na hivyo kuondoa changamoto ya uhaba wa ajira kwa vijana hao.Kwa upande wake Mkuu wa Program Benki ya Dunia (WB), Tanzania, Gilead Teri ameeleza kwenye mhadhara huo kwamba sekta binafsi ipo tayari kushiriana na nchi za SADC ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo amezungumzia umuhimu wa kujikita katika kuendelea kuonesha miundombinu na elimu.Wakati huo huo Katibu Mkuu wa SADC, Dk.Stergomena Tax yeye amesema jumuiya hiyo imejipanga katika kuweka mipango madhubuti kwa lengo la kujitegemea na kuinua uchumi kwa nchi wanachama.

Akizungumza katika mhadhara huo Katibu Mkuu mstaafu wa SADC, Dk. Simba Makoni amesema kunahitajika mikakati ya kuifanya jumuiya hiyo ijulikane kwa wananchi wake na kwamba bado jamii inaamini jumuiya hiyo ni ya viongozi wao jambo ambalo linaweza kusababisha sintofahamu kwa siku zijazo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya Ulinzi Shule ya Wits ya Afrika Kusini, Profesa Anthoni van Nieuwkerk amesema SADC imefanikiwa katika eneo la ulinzi, usalama na demokrasi na kwamba ni wakati wa kujikita kwenye maeneo ambayo yatabadilisha wananchi.

Mzee Joseph Butiku wakati anazungumza ametumia nafasi kusisitiza umuhimu wa elimu ambayo itamsaida aliyesoma kujiajiri badala ya kulalamika kutokuwa na ajira na kufafanua kuwa idadi kubwa ya vijana ambao wamesema,hivyo ni wakati wa kutumia elimu yao katika fursa zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo.
 Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamini William Mkapa akihutubia katika mhadhara uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) uliokuwa ukizungumzia historia ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), mapema leo Agosti 15, 2019. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...