Mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania, Abel Dugange akizungumza kwenye uzinduzi huo wa mradi wa maji Sangara.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Elizabeth Kitundu akipiga (katikati) makofi baada ya kumtwisha ndoo ya maji kichwani mama wa Kijiji cha Sangara Kata ya Riroda.
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Vrajilal Jituson akielezea namna mfumo wa utiaji maji kwenye mradi huo.
Mkurugenzi wa operesheni wa shirika la Habitat for Humanity, Cyrus Watuku akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi huo.

……………….

WANANCHI 650 wa Kijiji cha Sangara Kata ya Riroda Wilayani Babati Mkoani Manyara, waliokuwa na changamoto ya ukosefu wa maji, wameondokana na kero hiyo baada ya mradi wa maji wa gharama ya sh229 milioni kuzinduliwa. 

Mradi huo wa wenye miundombiu ya kilomita 3.4 unaotoa maji lita 352,800 kwa siku sawa na lita 14,700 kwa saa, unatumia mfumo wa malipo kabla ya huduma kwa njia ya elekrtoniki.

Mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania, Abel Dugange akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo alisema waliingia makubaliano ya kutekeleza mradi huo mwaka jana na Halmashauri ya wilaya ya Babati, shirika la Habitat for Humanity, kampuni ya eWater na taasisi ya fedha ya Unit Trust of Tanzania (UTT-MFI).

Dugange alisema kabla ya kutekeleza mradi huo hali ya upatikanaji wa maji kwenye kijiji hicho ilikuwa asilimia 20 tofauti na lengo la Taifa la asilimia 85 ya huduma za maji vijijini.

“Mradi huu umelenga kuhamasisha ubunifu na kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu na uendeshaji wa miradi ya maji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma endelevu na hakika ya maji safi na salama vijijini,” alisema.

Mkuu wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu akizindua mradi huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti aliwataka wakazi wa eneo hilo kuutunza ili uwe endelevu. Kitundu alisema lengo la serikali ni ifikapo mwaka 2020 asilimia 85 ya waliopo vijijini wawe wamepata maji safi na salama na mwaka 2025 iwe asilimia 95 na mwaka 2030 iwe asilimia 100.

Mbunge wa jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jituson alisema mradi huo ni wa mfano kwani umeanzia Babati kisha wilaya za Korogwe mkoani Tanga na Arumeru mkoani Arusha zikafuata.

Jituson alisema mchotaji anaokoa muda kwani anaweza chota hata usiku na hauhitaji muuzaji wa maji kuwepo katika kituo.“Inaongeza usalama wa fedha kutopotea inayotokana na huduma ya maji, imeongeza nidhamu ya matumizi ya maji na hata tone moja linalipiwa,” alisema Jituson.

Mkazi wa kijiji hicho Magdalena Bayo alisema awali walikuwa wanachota maji umbali mrefu kwenye visima na makorongo ila mradi huu umewasaidia kwani upo karibu nao. 

“Mradi ni mzuri yaani kama vocha ya simu unaingiza tokeni maji yanatoka kadiri unavyolipia ndivyo unavyopata maji na hatutembei umbali mrefu kama awali unaamka alfajiri unapambana na foleni,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...