*Wanajumuiya ya SADC waombwa kutembelea banda la Life and Hope Rehabilitation na kujifunza mbinu za kudhibiti  dawa hizo na kuokoa vijana

Na Erick Picson, Michuzi TV

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa amesema kuwa Tanzania imekuwa ikipewa sifa na nchi mbalimbali duniani kwa jitihada zake za kudhibiti madawa ya kulevya ikiwemo bangi, mirungi na coccaine na kuokoa vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la taasisi ya Life and Hope Rehabilitation Sober House iliyopo Bagamoyo ambayo inayoshughulika na kuwahudumia waathirika wa dawa za kulevya na kupinga vita matumizi ya dawa hizo Majaliwa amesema kuwa jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali zimezaa matunda kwa kiasi kikubwa, elimu inatolewa na hatua zinachukuliwa hali iliyopelekea kupungua kwa kiasi kikubwa kwa tatizo hilo. 

"Tanzania imekuwa ikipokea sifa kutoka nchi nyingi Afrika na duniani kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kudhibiti madawa ya kulevya, nilikuwa kwenye mkutano Uingereza waziri mkuu wa Cameron alinipongeza hadharani kutokana na jitihada tunazoonesha na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupambana na madawa ya kulevya" Ameeleza Majaliwa.

Aidha Majaliwa amezishauri nchi wanachama wa SADC kutembelea banda hilo ili waweze kupata tathimini na mbinu ya kupambana na utokomezaji wa dawa za kulevya ambazo huathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo Emmanuel Mussana Masola ameishukuru serikali kwa kuendelea kupambana na janga hilo linaloathiri jamii hasa vijana na kuiomba kuendelea kupambana na yeyote anayejihusisha na madawa ya kulevya ili kuweza kujenga taifa la vijana wenye nguvu na wachapakazi.

Amesema kuwa wataendelea kutoa elimu zaidi juu ya madhara ya kutumia dawa za kulevya pamoja na kupambana na wasafirishaji wa dawa hizo jambo ambalo hata serikali linaunga mkono, na amewaalika wanajumuiya ya SADC kutembelea banda hilo ili kuweza kujifunza mbinu mbalimbali zitakazowasaidia katika kupambana na dawa za kulevya.

Mmoja wa warahibu kutoka taasisi hiyo ameishukuru serikali kwa kuendelea kusaidia katika kudhibiti tatizo hilo hasa wakati huu ambapo taifa linaelekea kujenga uchumi wa viwanda huku vijana wakiwa nguvu kazi kwa kiasi kikubwa na ameiomba serikali kupambana na njia mbadala zinazotumiwa na vijana Mara baada ya madawa hayo kupigwa marufuku.

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa (katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Emmanuel Mussana (kulia)mara baada ya kutembelea maonesho hayo ambapo amesema kuwa serikali ipo imara katika kupambana na yeyote atakayebainika kujihusisha na madawa ya kulevya, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akimsikiliza mmoja wa warahibu wa dawa za kulevya ambaye anatoa elimu kwa vijana na wanajamii kuhusiana na madhara ya madawa ya kulevya, na wameishukuru serikali kwa kuonesha jitihada za kupambana vikali na madawa ya kulevya,jana jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa (katikati) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa taasisi ya Life and Hope Rehabilitation Sober House Emmanuel Mussana (kulia) ambapo amesema kuwa elimu zaidi inaendelea kutolewa kwa vijana ili kuweza kujenga taifa la vijana wenye nguvu na wachapakazi, kushoto ni Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki profesa. Palamagamba Kabudi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...