Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), akipokea taarifa ya Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma, leo. Lugola aliizindua Bodi hiyo Mei 30, 2019 na kutoa miezi miwili Wajumbe wa Bodi hiyo kutembelea miradi mbalimbali ya Magereza Tanzania Bara na kumletea taarifa iyakayoambatana na maoni yao. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, baada ya kupokea taarifa ya Bodi hiyo, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma, leo. Lugola aliifurahia taarifa hiyo na kuwataka Wajumbe hao wahakikishe Magereza inajitosheleza kwa chakula kupitia miradi mbalimbali. Kulia meza kuu ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga. Na wapili kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga, akitoa ufafanuzi baada ya kuwasilisha taarifa ya kipindi cha miezi miwili kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (wapili kushoto). Wapili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, Phaustine Kasike, akizungumza katika kikao cha Bodi hiyo cha kuwasilisha taarifa yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto meza kuu). Kulia meza kuu ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

***********

Na Felix Mwagara, Dodoma (MOHA)

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepokea taarifa ya Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza, na kuwataka Wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Magereza inajitosheleza kwa chakula kupitia miradi mbalimbali inayomilikiwa na Jeshi hilo.

Waziri Lugola aliizindua Bodi hiyo Mei 30, 2019, na kutoa miezi miwili Wajumbe wa Bodi hiyo, kutembelea miradi mbalimbali ya Jeshi hilo na kumletea taarifa ya awali kuhusu miradi hiyo pamoja na maoni yao.

Akizungumza na Wajumbe wa Bodi hiyo baada ya kupokea taarifa yao, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dodoma, leo, Waziri Lugola alisema taarifa walioiwasilisha ameifurahia licha ya kuwa na mapungufu kadhaa ambayo yanahitaji uboreshaji zaidi.

Alisema Bodi hiyo inawataalamu mbaimbali ambao wanaweza wakaleta mabadiliko makubwa ya uzalishaji mali na kuweza kufanikisha Jeshi hilo linajitosheleza kwa chakula kupitia wafungwa mbalimbali waliopo magerezani.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri, ila nawataka mfanye kazi zaidi ambayo itatuwezesha kuona mipango mizuri zaidi katika kulisimamia Shirika hili ambalo bodi yake tuliizindua,”alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka Magereza kutumia wataalamu wa Jeshi kupima viwanja vyao ili kufanikisha maendeleo zaidi na siyo kushirikiana na makampuni binafsi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga, alisema Bodi yake kwa muda wa miezi miwili ilitembelea mradi wa ng’ombe wa nyama Mbigiri, mradi wa maziwa Kingolwira, mradi wa Uhunzi, mradi wa Kilimo Idete, mradi wa kilimo Kiberege na Mradi wa kilimo Isupilo ambapo Bodi hiyo ilifanya tathmini ya mali zilizopo, mipaka pamoja na historia ya miradi hiyo.

“Pia miradi mingine tuliyoitembelea ni mradi wa kilimo Ludewa, mradi wa kilimo na mifugo Kitai, mradi wa kilimo Mkwaya, na pia Bodi itaendelea kutembelea miradi mbalimbali ya Jeshi na kuendelea kutoa taarifa,” alisema Muhuga.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu aliitaka Bodi hiyo, ifanye ukaguzi wa kina wa mali za Shirika hilo kiundani zaidi ili taarifa hizo zije kiuhalisia zaidi na kuleta mikakati imara ya mafanikio.

Baadhi ya maelekezo aliyoyatoa Waziri Lugola kwa Bodi hiyo mara baada ya kuizindua, aliitaka kutekeleza maelekezo ya Rais John Magufuli kuhusu suala la Magereza kujitosheleza kwa chakula na pia bodi ihakikishe maeneo ya magereza yanapimwa na kupata hati miliki kwa kutumia wataalamu wa kupima ardhi wa Jeshi hilo.

Pia aliielekeza Bodi hiyo itembelee Magereza yote yenye miradi ya Shirika, na ifanye mkakati wa kutafuta wawekezaji kama vile wawekezaji kwenye mabwawa ya ufugaji wa samaki, na pia bodi itoe mawazo mapya ili kuondoa kufanya biashara kwa mazoea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...