Na Estom Sanga - TASAF 

Ujumbe wa Maafisa wa Serikali ya Nigeria wapatao 33 umeanza ziara ya siku Nane nchini kujifunza namna Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF unavyotekeleza majukumu yake kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini-PSSN. 

Akiwakaribisha Maafisa hao, Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF ,Bwana Amadeus Kamagenge amesema Mkakati wa Serikali ya Tanzania kupambana na umaskini kupitia TASAF umekuwa na mafanikio makubwa na umeamsha ari ya wananchi kuboresha maisha yao. 

Bwana Kamagenge amesema mkazo mkubwa umewekwa katika uhamasishaji wa Walengwa kushiriki kwenye kazi za uzalishaji mali huku sekta ya elimu na afya hususani kwa watoto kutoka katika kaya za Walengwa zikipewa msukumo mkubwa zaidi kwenye shughuli za Mpango. 

Aidha Mkurugenzi huyo wa Miradi wa TASAF amesema mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa shughuli za Mpango yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na ushiriki wa Walengwa na Mchango mkubwa wa Serikali na Wadau mbalimbali wa Maendeleo. 

Kwa upande wao Maafisa hao kutoka nchini Nigeria wamesema uamuzi wa kuja Tanzania kujifunza umetokana na taarifa walizonazo juu ya mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Tanzania kupitia TASAF imepata kwa kuzifikia Kaya za Walengwa na kuzihudumia kwa mafanikio makubwa katika kupunguza kero ya umaskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao ni wa aina yake kupata kutekelezwa barani Afrika. 

Ujumbe huo wa Maafisa kutoka Nigeria, mbali na kupata maelezo ya shughuli za TASAF katika Ofisi ndogo za Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam pia utapata fursa ya kutembelea Unguja ambako utakutana na Maafisa wa Serikali na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kisiwani humo . Hii ni mara ya Pili kwa Maafisa wa serikali kutoka Nigeria kutembelea Tanzania kujifunza namna TASAF inavyotekeleza majukumu yake kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF,Amadeus Kamagenge(aliyesimama) akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha Maafisa wa Serikali kutoka Nigeria ambao wako nchini kujifunza utekelezaji wa shughuli za TASAF. Kulia kwake ni mkurugenzi wa Fedha wa TASAF Bi. Chiku Thabit.
Baadhi ya Maafisa wa Serikali ya Nigeria wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF katika ofisi ndogo zilizoko jijini Dar es Salaam wakisikiliza maelezo ya utekelezaji wa Shughuli za TASAF wakiwa katika ziara ya mafunzo ya namna Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unavyotekelezwa.
Mmoja wa Maafisa wa Serikali ya Nigeria (aliyesimama) akizungumza kwenye kikao cha kuukaribisha Ujumbe huo ikiwa ni mwanzo wa ziara ya kujifunza shughuli za TASAF zinavyotekelezwa.
Baadhi ya Maafisa kutoka Nigeria wakimsikiliza Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF (hayupo pichani) katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Ndogo ya TASAF jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Watendaji wa TASAF wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Nigeria ambao wako nchini kwa ziara ya mafunzo ya namna Mfuko wa Maendeleo ya Jami – TASAF unavyotekeleza majukumu yake kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...