*Asema dhamana ya uongozi haimpi kiongozi kuwa na haki kuliko raia, ahimiza amani na kudumisha uhuru na umoja.

Na Leandra Gabriel, Michuzi Tv

LEO Oktoba 8, Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amefungua kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha baba wa taifa lililobeba mada kuu ya "Urithi wa Mwalimu Nyerere katika Uongozi, Maadili, Umoja na Amani katika Ujenzi wa Taifa" kongamano lililofanyika katika chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali na vyama mbalimbali vya Siasa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Dkt. Kikwete amesema kuwa kumkumbuka Mwalimu Nyerere ni jambo analostahili na hiyo ni kutokana na mambo mengi aliyoyafanyakwa nchi, barani Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

" Mwalimu ni mkombozi wetu kwa kuwa alitukomboa kutoka kwa ukoloni, ni ngumu kuacha kazi yenye mshahara lakini mwalimu aliacha kazi yake na kuwa Rais wa TANU kazi ambayo haikuwa na mshahara na kujitoa kwa ajili ya kudai uhuru ambao hujui utapata au la na hujui utaupata lini, na alitumia maneno yenye umaarifa na uhodari ambao umetufikisha hapa" Ameleeza Dkt. Kikwete.

Amesema kuwa siku zote Mwalimu alisisitiza kutokubaguana kwa makabila na dini pamoja na kusisitiza utu miongoni mwetu.

"Dhamana ya uongozi haikufanyi uwe na haki kuliko raia wengine, kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi bali kutekeleza majukumu yako kwa weledi kutakufanya uwe bora zaidi" Ameeleza.

Aidha amesema kuwa Mwalimu aliwapenda sana vijana na kutambua umuhimu wa vijana na aliwapa fursa ya kujifunza uongozi wa juu na hiyo ni kutokana na nafasi ya vijana katika taifa;

" Lazima tuwape vijana nafasi katika ujenzi wa taifa tuwape nafasi, mawazo hayapigwi rungu bali mawazo yanashindwa na mawazo yaliyo na nguvu zaidi" ameeleza.

Vilevile amesema kuwa urithi tulioachiwa na Mwalimu ambao sasa ni tunu zinazotutambulisha  tuzitunze ili nchi yetu iendelee kuwa na amani.

Awali akieleza historia ya Chuo hicho Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wamekuwa wakipambana na ujinga kwa kutoa mafunzo ya uongozi, maadili, uzalendo na utawala bora hali iliyopelekea Chuo hicho kuwa kitovu cha uongozi, maadili na uzalendo.

Amesema kuwa Chuo hicho kimejipanga kutoa mafunzo ya muda mfupi ya uongozi kwa taasisi mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo ya muda mrefu ya uongozi katika ngazi za shahada mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho Stephen Wasira amesema kuwa licha ya makongamano hayo lazima pia mitaala ya elimu iangalie zaidi suala la kujua historia ya nchi ili kuweza kujenga uzalendo.

" Huwezi kuwa mzalendo kwa kuifia nchi usiyoijua hivyo lazima elimu iwaandae vijana kupitia mitaala ya elimu na hiyo ni pamoja na wataalamu wa historia kuandika vitabu vya ukombozi vitakavyotoa maarifa kwa kizazi cha sasa na baadaye" ameeleza Wasira.

Amesema kuwa kama Mwalimu alivyotumia lugha ya Kiswahili bila mkalimani na sisi hatuna budi kukitunza na pamoja na kuimarisha uhuru na umoja ambavyo ni misingi ya kujivunia.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa kwanza, Waziri Mkuu na Spika mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Makamu wa Rais wa awamu wa nne Dkt. Gharib Bilal, Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally,  Mama Fatma Karume, Chifu Wanzaki Nyerere pamoja na viongozi mbalimbali vya vyama na Serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...